Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) na Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto).
Na Hamza Temba-WMU-Dar es Salaam
.......................................................................
Wizara
ya Maliasili na Utalii imetangaza rasmi viwango vipya vya malipo ya ada
kwa Mawakala wa kusafirisha watalii nchini baada ya kukamilika kwa
marekebisho ya kanuni ya ada na tozo za biashara ya utalii yaliyofanyika
mwezi Desemba mwaka jana, 2017.
Taarifa
iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudence
Milanzi, imeeleza kuwa baada ya kukamilika kwa marekebisho hayo ya
kanuni, Tangazo la Serikali namba 506 la tarehe 29 Desemba, 2017,
limeweka viwango vipya vya ada kwa mawakala wa kusafirisha watalii (Tour
Operators na Safari Outfitters).
Taarifa
hiyo imeeleza viwango hivyo kuwa ni shilingi sawa na dola za Kimarekani
500 kwa kampuni za wazawa zenye umiliki mkubwa wa raia wa Tanzania na
zinazomiliki gari 1 hadi 3.
"Shilingi
sawa na dola za Kimarekani 2,000 kwa kampuni zenye gari 4 hadi 10,
shilingi sawa na dola za Kimarekani 3,000 kwa kampuni zenye gari 11 hadi
50 na shilingi sawa na dola za Kimarekani 5,000 kwa kampuni zenye
kumiliki gari 51 na kuendelea", imeeleza taarifa hiyo.
Kwa
upande wa kampuni za kigeni zenye umiliki mkubwa wa raia wa kigeni na
zinazomiliki gari 10 hadi 30 zitalipa ada ya shilingi sawa na dola za
Kimarekani 5,000, kampuni zenye gari 31 hadi 50 zitalipa shilingi sawa
na dola za kimarekani 7,500 na na kampuni zenye gari 51 na kuendelea
zitalipa shilingi sawa na dola za Kimarekani 10,000.
Kufuatia
marekebisho hayo, muda wa kutumika kwa leseni za mwaka 2017 za Wakala
wa kusafirisha watalii (Tour Operators na Safari Outfitters) umesogezwa
mbele hadi tarehe 31 Januari, 2018 ili kuwezesha maandalizi ya kuingia
kwenye mabadiliko ya viwango hivyo vipya.
Aidha,
taarifa hiyo imeeleza kuwa maombi ya usajili na leseni za biashara ya
utalii na leseni za waongoza watalii kwa mwaka 2018 kwa wafanyabiashara
wapya na wanaoendelea na biashara yanaendelea kupokelewa.
Waombaji
wote wametakiwa kufuata masharti ya uombaji wa leseni hizo ikiwemo
kuwasilisha nakala za hati za usajili wa magari zilizothibitishwa
kisheria kwa Wakala wa kusafirisha watalii (wapya na wanaoendelea na
biashara) na kivuli cha leseni ya mwaka 2017 kwa wafanyabiasbara wote.
"Ni kosa kisheria kuwasilisha taarifa za uongo na adhabu yake ni pamoja na kufutiwa leseni", imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Desemba
10 na 11 mwaka 2017, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla alikutana na wadau wa sekta ya utalii jijini Arusha kwa
lengo la kuwashirikisha katika mapendekezo ya viwango vipya vya ada kwa
Wakala wa kusafirisha watalii ambavyo vilivyotolewa na Wizara yake.
Mapendekezo ya viwango hivyo yalilenga kuongeza mapato na kuwawezesha
wafanyabiashara wadogo wenye gari kuanzia moja kuingia katika biashara
hiyo.
No comments:
Post a Comment