Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ametoa onyo kali kwa viongozi wa
kisiasa wa Wilaya ya Kiteto kuwa atawachukulia hatua kali wote
watakaosababisha migogoro ya ardhi kwa wananchi.
Akizungumza
kwenye kata ya Njoro, Mnyeti alisema atawachukulia hatua kali wanasiasa
hao kwani yeye siyo mkuu wa mkoa wa maboksi anayeogopa kulowanishwa na
mvua. Alisema alipata taarifa ya baadhi ya wanasiasa
wanaotumia migogoro ya ardhi kwa ajili ya kujinufaisha kisiasa, ila
hatawafumbia macho wanasiasa wa aina hiyo waliopo wilayani Kiteto.
"Tumekuwa
na migogoro isiyokwisha, wewe una shamba lako kwenye kijiji cha Bwawani
kuna mtu anakuzuia kulima hapa Njoro? au ukiishi hapa Njoro kuna mtu
amekunyima kununua nyumba kule Kibaya makao makuu ya wilaya?" alihoji
Mnyeti. Alisema atawashughulikia wanasiasa hao wanachochea
migogoro ya ardhi baina ya watu na watu na kijiji na kijiji ili iwe
funzo kwao na hawatasahau kitendo hicho.
"Wanasiasa
hao wababaishaji, wanaojaribu kuishika serikali sharubu nitakula nao
sahani moja, kwani hatuwezi kukubali hali hiyo ijitokeze na kuacha
kuchukua hatua kwao bila kuangalia vyeo vyao," alisema Mnyeti. Hata
hivyo, alimuagiza mkuu wa wilaya ya Kiteto, mhandisi Tumaini Magessa
kuhakikisha vijiji vyote vinawekewa alama za mipaka ili kuondokana na
migogoro ya ardhi.
Mwenyekiti
wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Lairumbe Mollel ambaye ni diwani wa
kata ya Chapakazi ni mmoja kati ya viongozi wanaotajwa kusababisha
migogoro hiyo wilayani Kiteto alikana kujihusisha nayo. "Mheshimiwa
mkuu wa mkoa afanye uchunguzi wake na atabaini kuwa mimi sihusiki na
uchochezi wa migogoro hiyo ya ardhi zaidi ya kuongoza halmashauri yangu
ya wilaya kupitia nafasi hii," alisema Mollel.
Pia,
mbunge wa jimbo la Kiteto, Emmanuel Papian ambaye naye anatajwa kuhusika
na uchochezi wa migogoro alisema wapinzani wake wa kisiasa ndiyo
wanasambaza habari hizo potofu kwani yeye hausiki. Awali,
mmoja kati ya wakazi wa Njoro Amina Omary alisema wanasiasa hao wamekuwa
mwiba mkali kwao kwani wamekuwa wachonganishi kwa wakulima na wafugaji
kwa lengo la kujipatia kura pindi kipindi cha uchaguzi kitakapofika.
Omary
alisema wanasiasa hao wamekuwa wanawaunga mkono wafugaji wanaoingiza
mifugo kwenye mashamba ya wakulima badala ya kuwakataza ili kuepusha
migogoro isiyo kuwa na tija.
Ramadhan
Juma alimuomba mkuu huyo wa mkoa kuwachukulia hatua kali wanasiasa hao
wababaishaji ili kuepuka kutokea kwa mapigano kama ya miaka iliyopita
ambayo ilichochewa nao na kusababisha mauaji.
Wananchi
wa Kata ya Njoro Wilayani Kiteto, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa
Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza nao, juu ya kuwachukulia hatua
kali wanasiasa wanaosababisha migogoro ya ardhi.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti akizungumza kwenye Kata ya Njoro
Wilayani Kiteto juu ya kuwachukulia hatua kali wanasiasa wanaosababisha
migogoro ya ardhi, kushoto ni mbunge wa jimbo hilo Emmanuel Papian na
Mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Tumaini Magessa.
Wananchi
wa Kata ya Njoro Wilayani Kiteto, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa
Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza nao, juu ya kuwachukulia hatua
kali wanasiasa wanaosababisha migogoro ya ardhi.
No comments:
Post a Comment