Pages

January 6, 2018

PROF.NDURU AWAAGA BoT KWA UJUMBE MZITO



*Baadhi ya wafanyakazi washindwa kuvumulia watokwa machozi,
*Mwenyewe asema Gavana Prof Luoga ni mtu sahihi,apewe ushirikiano

Said Mwishehe Globu ya jamii

HATIMAYE Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Profesa Benno Nduru ameagwa rasmi na wafanyakazi wa benki hiyo ambapo baadhi yao wakajikuta wanashindwa kuvumilia kiasi cha kutokwa machozi huku mwenyewe akitumia nafasi hiyo kuacha ujumbe mzito kwa wafanyakazi na Gavana mpya wa BoT, Profesa Floranc Luoga.

WAFANYAKAZI BoT WATOKWA MACHOZI

Wafanyakazi wamesema Prof.Nduru amekuwa Gavana wa BoT kwa miaka 10 na sasa amemaliza muda wake na kukabidhi nafasi hiyo kwa  Prof.Luoga ambaye kwa mujibu wa ratiba ataanza rasmi kazi Jumatatu ya keshokutwa.

Hivyo wafanyakazi wa BoT waliamua kuandaa sherehemu maalumu kumuaga Prof.Nduru na kisha kumkaribisha rasmi Prof.Luoga. Sherehe hizo zilifanyika katika ukumbi uliopo kwenye benki hiyo juzi.

Kwa sehemu kubwa katika tukio hilo wawakilishi mbalimbali wa BoT wamepata nafasi ya kumzungumzia Prof.Nduru namna ambavyo amefanya kazi zake kwa uzalendo mkubwa na alitoa nafasi ya kuwapa nafasi wafanyakazi kila mmoja kuonesha uwezo wake katika eneo analofanyika kazi.

Pia wamemuelezea namna ambavyo amerudisha heshima ya BoT ambayo wakati anaingia ilikuwa imeanza kupoteza heshima.Wafanyakazi hao hawakusita kuelezea namna  alivyomakini na mwenye kutumia weledi kutekeleza majukumu ya benki hiyo kwa maslahi ya nchi na Watanzania wote.

Hata hivyo wimbo rasmi wa kumuaga Prof.Nduru ulisababisha baadhi ya wafanyakazi kushindwa kuvumilia.Maneno yaliyokuwa yanaelezwa dhidi ya namna alivyoishi nao BoT na sasa anawaacha yalikuwa na ujumbe wenye kugusa moyo wa kila aliyekuwepo ukumbini.

PROF NDURU AACHA UJUMBE, AWATOA HOFU 

Akizungumza mbele ya Gavana Mpya Prof.Luoga, wafanyakazi wa BoT na wageni wengine waalikwa,Prof.Nduru ametumia nafasi hiyo kuelezea mengi yaliyofanywa katika uongozi wake na kubwa zaidi akatumia nafasi hiyo kuwataka wafanyakazi hao kujiendeleza kitaaluma kama ambavyo wamekuwa wakifanya siku zote.

Wafanyakazi kusimamia misingi ya majukumu ya kazi zao kwa weledi huku akieleza anaheshimu sana mfanyakazi wa BOT anayependa kujiendeleza kitaaluma.

Akaweka wazi, baada ya kuingia BoT kuna mambo alitamani kuona yanabadilika na hasa la kuwapa viongozi wengine na wafanyakazi nafasi ya kujieleza na kutoa ushauri, kitu ambacho amefanikiwa na sasa viongozi wa benki hiyo kwa nafasi tofauti wanaweza kutoa ushauri na ukasilikizwa.

Ameeleza namna ambavyo kuna haja ya kuendelea kuboresha Huduma za hali bora za kazi kwa wafanyakazi wa BoT na kubwa zaidi kumpa ushirikiano Gavana Prof.Luoga ambaye yeye binafasi anatambua uwezo wake, uzalendo wake na uchapakazi wake kwa maslahi ya Taifa.

 "Sina shaka na Prof.Luoga, naomba mumpe ushirikiano.Ni mtu sahihi na ataendeleza pale nilipoishia.Sina wasiwasi hata kidogo BoT itafanya vizuri zaidi ya sasa katika kusimamia wajibu wake.

"Najua yanapotokea mabadiliko makubwa, wapo baadhi ya watu huwa na hofu lakini niwahakikishie ondoeni hofu, fanyeni kazi na kikubwa zaidi ni kumpa ushirikiano Gavana Luoga,"amesema Prof.Nduru na kuongeza "Nawapenda sana wafanyakazi wa BoT na nitawapenda daima".

Prof.Nduru akawasisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda tahamani ya sarafu ya Shilingi ya Tanzania, kudhibiti mfumuko wa bei na kusimamia sheria , kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

Akatumia nafasi hiyo kumueleza Prof.Luoga kuwa anawaachia watu wenye moyo wa kujituma katika kazi hivyo awatumie vema kwani kuna wataalamu waliopikwa vema na benki hiyo na kazi yake ni kuwalinda watalaamu hao na kuhakikisha wanapatikana wengine wengi.

"Prof.Luoga BoT tunao mtaji, tuna akiba ya kutosha hivyo ni kuendelea kuilinda na kuiongeza kwani heshima yetu iko katika akiba tuliyonayo inayotuwezesha kufanya kazi zetu kwa muda mrefu  bila kuwa omba omba.Msikubali kuwa ombaomba,"amesema Prof.Nduru.

PROF.LUOGA ASIFU UTENDAJI KAZI WA NDURU

Kwa upande wake Gavana mpya wa BoT, Profesa Luoga baada ya kukaribishwa rasmi na wafanyakazi wa benki hiyo amesema anatambua kazi nzuri iliyofanywa na Prof.Nduru na yeye kama mwalimu anampa alama A ya utendaji kazi uliotukuka na amemaliza kuitumikia nafasi hiyo salama bila ya kuwa na madoa.

Prof.Luoga amesema yeye ni mwenye kujifunza na ataendelea kujifunza kadri anavyoweza na kufafanua kabla ya kuanza majukumu yake Prof. Nduru alimpa vitabu vingi vya kusoma na alivisoma vyote na sasa yupo tayari kwa kazi.

"Kwa kutumia watendaji waliopo na wafanyakazi wote wa BoT ni muda wa mimi na ninyi kutembea pamoja ili kufikia mafanikio ambayo yamekusudiwa.Prof. Nduru anaicha BoT ikiwa kwenye alama A , ni jukumu letu sisi kuhakikisha tunabaki katika alama hiyo hiyo"amesema Prof.Luoga.

Amesema kuna kila sababu ya kutumia namna bora ya kutatua changamoto zilizopo. "Nilichokiona kwa siku chache ambazo nilikuwa napita kwenye korido nikiwa na Prof. Nduru, hakika wafanyakazi wa BoT wanaipenda taasisi yao, watendaji nao wana ari ya kuendeleza mafanikio.Leo nimekaribishwa si siku yangu ya kuzungumza sana"

WAFANYAKAZI WAFURAHIA UJIO WA PROF.LUOGA

Pamoja na mambo mengine wafanyakazi hao kupitia hotuba zilizokuwa zinatolewa zilimuelezea Gavana mpya na wote wamefurahishwa na kuteuliwa na Rais ,Dk John Magufuli kuwa Gavana wa benki hiyo.


Pia wakamkaribisha kwa wimbo maalumu ambao huo uliibua shangwe zaidi kwa wafanyakazi kutokana na maneno yaliyokuwa yakiimbwa na waimbaji wa bendi ya benki hiyo.WAfanyakazi pia waliibua shangwe baada ya shairi lililoimbwa ukumbini kumtaka Prof.Nduru baada ya kumaliza kuitumikia BoT sasa aende akaishi Ifakara kwani hatakuwa fukara.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...