Ndugu
Waandishi wa Habari, nimewaita hapa kuzungumza nanyi na kupitia kwenu
kuzungumza na wananchi wenzangu kuhusu taaarifa ya kukamatwa kwa meli
zilizokuwa zimepakia shehena za dawa za kulevya na silaha zikiwa
zinapeperusha bendera ya nchi yetu.
Meli hizo ni:
Kaluba
yenye usajili namba IMO 6828753 iliyokamatwa tarehe 27 Desemba 2017
ikiwa na wastani wa kilo 1,600 za dawa za kulevya huko katika maeneo ya
Jamhuri ya Dominican Republic; na
Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 iliyokamatwa kwa kusafirisha silaha kinyume na Sheria za kimataifa.
Meli
zote mbili zimesajiliwa Tanzania kupitia taasisi yetu ya Mamlaka ya
Usafiri Baharini Zanzibar ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya kusajili meli
za nje.
Hapa
kwetu Tanzania tuna aina mbili za kusajili Meli; usajili wa Meli zenye
asili ya Tanzania na zile zenye asili ya Nje. kwa kuzingatia kuwa
Tanzania ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa na mashirika yake
mbalimbali, siku zote tumekuwa tunaheshimu na kutekeleza kikamilifu
majukumu yetu ya kimataifa yaliyowekwa kupitia mikataba na maazimio
mbalimbali ya vyombo hivyo
Ndugu
Waandishi wa Habari, kwa mujibu wa mkataba wa UNCLOS 1982 kila nchi
imepewa haki ya kufanya usajili wa meli kwa kuzingatia mikataba ya
kimataifa na sheria za nchi husika.Kwa upande wa Tanzania, usajili wa meli za kimataifa unasimamiwa na Sheria Na 5 ya mwaka 2006,
(Kwa
upande wa SUMATRA ina Merchant Shipping Act ya mwaka 2003. Sheria hi
inaruhusu usajili wa meli inayomilikiwa na Mtanzania, au meli
inayomilikiwa kwa ubia kati ya Mtanzania na raia wa nchi nyingine. Kwa
sheria hii ili meli ipate usajili wa SUMATRA na kuruhusiwa kupeperusha
bendera ya Tanzania ni lazima umiliki wa meli uhusishwe na raia wa
Tanzania kwa umiliki wote au kwa ubia lakini ni lazima Mtanzania awe na
hisa nyingi. Vilevile kampuni hiyo ya umiliki lazima iwe ya Kitanzania
kwa maana ya kusajiliwa na kujiendesha kutokea Tanzania hata kama
kampuni hiyo inamilikiwa na watu wasio Watanzania. Na kwa upande wa
Zanzibar kupitia ZMA wana Maritime Transport Act ya mwaka 2006).
Sheria
hii inaruhusu usajili wa meli yoyote hata kama mmiliki wake sio
Mtanzania wala kampuni kuwa ya Kitanzania hivyo basi kutoa fursa kwa
meli ambayo haina umiliki wa aina yeyote wa Tanzania kwa maana umiliki
na ukazi kupewa usajili wa kupeperusha bendera yetu nje ya Tanzania.
Aidha, Sheria hizi huendeshwa sambamba pamoja na Sheria na Kanuni za
Kimataifa.
Ni
vyema tukafahamu kuwa Sheria na Kanuni hizo humlazimu mwenye Meli,
kujaza fomu maalumu ya maombi pamoja na Fomu za “DECLARATION OF VESSELS
NON INVOLVEMENT WITH CRIMINAL ACTS OR OMISSIONS”; na ndipo hatua
nyingine za kufanya uchunguzi wa historia ya meli kupitia International
Maritime websites na vyanzo vingine, tangu Meli ilipotengenezwa hadi
muda inapoomba usajili.
Uhakiki hufanywa pia kupitia mitandao mingine mikubwa mitatu inayotumika duniani kote kupata historia ya meli, Mitandao hiyo ni:
Fleet Moon;
Maritime Traffic; na
iii. Maritime-connector.
Baada
ya ZMA ambayo ndio kisheria imeruhusiwa kusajili meli nje ya Tanzania,
kujiridhisha na maelezo na taarifa zilizopatikana, maamuzi ya kusajili
au kutosajili yanatolewa kupitia Idara ya Usajili.
Ndugu
Waandishi wa Habari, kwa mujibu wa taratibu za Mkataba wa Kimataifa wa
Kupambana na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya, 1988 na Azimio la Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa 1970 (2011).
nchi
zilizosajili Meli zinazokamatwa hutakiwa kutoa kibali kwa Walinzi wa
Mwambao wa Bahari wa nchi husika, na kwa Meli hizi, tulitoa kibali kwa
Jeshi la Mwambao wa Marekani na Jeshi la Mwambao wa Ugiriki kuzikamata
na kuzipekua meli hizo.
Baada ya kupata taarifa za upekuzi hatua za haraka zilizochukuliwa upande wetu ni kufuta Usajili wa Meli hizo.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Tanzania vilevile ni mwanachama wa Mkataba wa
Kimataifa wa Kupiga Vita Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya (United
Nations Convention Against Illicit Traffic of Narcotic Drugs and
Psychotropic Substance, 1988) na pia ni Mwanachama wa Mkataba wa
Kimataifa wa Kupiga Vita
Usafirishaji
Haramu wa Silaha (United Nations Protocol Against Illicit Manufacturing
of and Trafficking in Arms, their Parts and Components and Ammunition,
Supplementing the United Nations Convention Against Transnational
Organized Crime, 2001).
Kwa
mnasaba huu, tunapenda kutoa taarifa kuwa Tanzania imejidhatiti na
imedhamiria kutekeleza majukumu yake yaliyoelezwa katika mikataba hiyo
ya kimataifa,
ikiwemo kushirikiana na mataifa mengine pamoja na mashirika ya
kimataifa katika kupiga vita usafirishaji wa dawa za kulevya na silaha.
Nyote ni mashahidi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
Awamu ya Tano imetangaza vita dhidi ya watu wote wanaojihusisha na dawa
za kulevya na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimekuwa vikifanya kazi
usiku na mchana kuhakikisha vinatokomeza kabisa uhalifu huo.
Hivyo
basi, taarifa ya kukamatwa kwa meli zenye bendera ya Tanzania
zikisafirisha dawa za kulevya na silaha ni kinyume na Sheria za nchi
yetu na zile za kimataifa. Taarifa hizi zimeleta mshtuko mkubwa ndani ya
nchi yetu. hasa kwa kuwa Tanzania imejipambanua kupambana na maovu hayo
kwa kutumia nguvu zote.
Ndugu
Waandishi wa Habari, kufuatia taarifa hizo, Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania aliniagiza kuitisha kikao cha dharura baina ya
viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzungumzia kadhia hiyo.
Jana
Jumatano, tarehe 17 Januari 2018, Viongozi na Wataalamu wa pande zote
mbili wakiongozwa na mimi mwenyewe na Mhe. Balozi Seif Ali Idi, Makamo
wa Pili wa Rais, Zanzibar tulifanya kikao kilichojadili masuala haya kwa
kina huko Zanzibar.
Ndugu Waandishi wa Habari, baada ya majadiliano ya kina kuhusu masuala haya, kikao kilibaini yafuatayo:
Suala la Usajili wa Meli za Nje linafanywa na Nchi nyingiduniani; Kwa mfano katika Bara la Afrika
nchi
zinazofanya usajili wa kimataifa ni pamoja na Liberia, Komoro na Sierra
Leone. Aidha, kwa Bara la Asia, kuna nchi za China na Singapore na kwa
Amerika ya Kusini ni pamoja na Panama.
Ilibainika
kwamba Wenye Meli hupendelea kusajili meli zao nje ya nchi zao kwa
kukimbia uzito wa kodi na sheria zinazobana shughuli zao.
Wakala
aliyekuwa akifanya kazi hii kwa niaba ya ZMA na ambaye ameshavunjiwa
Mkataba bado anaendelea kufanya usajili kwa kuiba Bendera ya Tanzania.
Kutokana na hayo kikao kiliazimia yafuatayo:
Kutoa
taarifa na ufafanuzi wa kina kuhusu kadhia ya meli hizo kukamatwa na
dawa za kulevya na silaha kwa umma wa Watanzania na dunia kwa ujumla ili
kuondoa upotoshaji wa aina yoyote kwa kupitia vyanzo visivyo rasmi. Kwa
sasa ndio natekeleza azimio hili;
Kwa
kuwa uendeshaji wa biashara hii unaonekana kuleta utata na kutia dosari
kubwa kwa Taifa letu na kuharibu sifa njema za Nchi yetu, imeonekana
haja ya kuunda kamati ya pamoja ya wataalam wa SMZ na SMT
itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kupitiwa
upya usajili uliokwishafanyika na kuzihakiki taarifa za meli zote
zilizosajiliwa nchini mwetu, kuangalia mwenendo mzima wa usajili, na
hatimaye kutoa mapendekezo na ushauri kwa Serikali;
Kuanzisha
utaratibu wa kuzifanyia uchunguzi wa kina (due diligence) meli zote
mpya zitakazoomba usajili pamoja na wamiliki wake kwa kushirikisha
vyombo mbalimbali vya Serikali vikiwemo vile vya ulinzi na usalama;
iii.
Kufanya mapitio ya sheria zetu, ili kuzipa nguvu zaidi taasisi
zinazosimamia usajili wa meli. Wakati wa mapitio ya sheria, timu ya
wataalam itaangalia kwa makini kodi zinazotozwa na mchango wake nchini
ili zisiwe kivutio kwa meli zisizokidhi viwango kuomba usajili Tanzania;
Kuendelea
kushirikiana na nchi nyengine kwa kuzipa ruhusa kukamata na kuzipekua
meli zinazopeperusha bendera yetu wakati wote zinapohisiwa kuwa
zinafanya uhalifu, au masuala ambayo haziruhusiwi kwa mujibu wa sheria,
taratibu na kanuni zinazokubalika kimataifa na wakati wa usajili.
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment