Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na waandishi
wa habari katika ukumbi wa Wizara hiyo Mjini Dodoma . Kulia kwake ni
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Aloyce Nzuki.
Na Hamza Temba - Dodoma
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla Januari 25, 2018
mjini Dodoma ametaja majina ya watuhumiwa wa ujangili ambao wengi wao ni
wamiliki na washirika wa Kampuni za uwindaji wa kitalii na kuwapa siku
saba wawe wamefika kwa hiari yao wenyewe katika ofisi za Wizara hiyo
Mjini Dodoma, Swagaswaga House kwa ajili kutoa maelezo kwanini
wasichukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kujibu tuhuma hiyo na nyingine
nyingi zinazowakabili mbele ya kamati atakayoiunda.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa, Dk. Kigwangalla ametaja baadhi ya
tuhuma hizo ambazo ziko kinyume cha sheria na taratibu za uwindaji wa
kitalii kuwa ni uwindaji haramu, uhawilishaji wa umiliki wa vitalu vya
uwindaji pasipo kufuata sheria, udanganyifu kwenye kujaza fomu za
uangalizi, rushwa, uhalifu dhidi ya rasilimali za wanyamapori na
uhujumu uchumi.
Alitaja
tuhuma zingine kuwa ni ukiukwaji wa kanuni za uwindaji (kupiga wanyama
usiku, kuwinda wanyama bila kujali umri, kupiga wanyama nje ya maeneo
waliyopewa), kukutolipa tozo mbalimbali za maendeleo za jamii kwenye
vijiji jirani na maeneo wanaoendesha biashara ya uwindaji, kushindwa
kuendesha ipasavyo shughuli za kuzuia ujangili.
Dk.
Kigwangalla aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni ndugu Pasanis na wenzake
ambao wanamiliki kampuni ya Berlette Safari Corporation Ltd na Ngugu
Shein Ralgi na wakurugenzi wenzake wa kampuni ya Game Frontiers of
Tanzania Ltd.
Wengine
ni Ndugu Howel na wakurugenzi wenzake wa kampuni ya Mkwawa Hunting
Safaris Tanzania Ltd, Ndugu Thomas Fredikin na wenzake wa Kampuni ya
Mwiba Holdings Ltd, Wengert Windrose Safaris Tanzania Ltd na Tanzania
Game Trackers Safaris Ltd, na Ndugu Awadh na wenzake ambao wanamiliki
kampuni ya Uwindaji wa Greenmiles Safaris Ltd.
Aliwataja
washirika wengine kuwa ni Ndugu ni Kwizema, Ndugu Robert, Ndugu Solomon
Makulu, Ndugu Siasa Shaban, Ndugu Hamis Abdul Ligagabile na mtumishi wa
Wizara Wizara ya Maliasili na Utalii, Alex Aguma.
Katika
hatua nyingine Dk. Kigwangalla ametoa Ilani ya siku 30 kwa watu
mbalimbali ikiwemo Mawaziri Wakuu Wastaafu waliovamia kiwanja chenye
hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha wafike kwa Kamishna Mkuu
wa Ardhi waweze kuhakikiwa na kuthibitisha umiliki wao halali ama sivyo
wavirejeshe Serikalini viweze kumilikishwa kwa mmiliki wake halali.
“Natoa
ilani ya siku 30 kwa mtu yeyote ambaye anajua alivamia kiwanja katika
eneo hili ambalo lina hati namba 4091 kilichopo Njiro, Arusha, haraka
sana ajipange kupeleka taarifa zake mbele ya Kamishna wa Ardhi kabla
hatujachukua hatua nyingine za kisheria, hati iliyoko pale ipo katika
jina la Bodi ya Utalii Tanzania japo wao wanadai wana hati nyingine.
“Wengi
wao wamejenga nyumba za kudumu katika eneo lile, na wengine ni viongozi
waliokuwa mawaziri wakuu wastaafu nao wana viwanja katika eneo hilo na
wamejenga nyumba zao katika eneo hilo,” alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema
kiwanja hicho kilichokuwa na ekari zaidi ya 40 kilikuwa kinamilikiwa na
taasisi ya Serikali ambayo ni kampuni tanzu ya Bodi ya Utalii Tanzania
iliyokuwa inajulikana kama Serengeti Safari Lodges na baadae kikauzwa
kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
Wakati
huo huo, Dk. Kigwangalla ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi nchini
kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wanne wanaojihusisha na mtandao wa
ujangili pamoja na kupanga njama zilizopelekea mauaji ya Mhifadhi wa
Wanyamapori Ndugu Wayne Lotter, raia wa Afrika ya Kusini ambaye alikuwa
Mkurugenzi wa Kampuni Pams Foundation, aliyeuawawa eneo la Chole Masaki
Jijini Dar es Salaam mwezi Agosti mwaka jana.
“Natoa
siku saba kwa wenzetu wa jeshi la Polisi wachukue hatua dhidi ya watu
wanne, ambao mimi majina yao ninayafahamu ambao miongoni mwao watatu
wanahusika na kuendesha biashara ya ujangili, na ni watu wakubwa, ni
matajiri wakubwa na wana mitandao mikubwa ya ujangili.
“Ninafahamu
taarifa hizi polisi wanazo lakini hawajachukua hatua za kuwakamata watu
hawa na kuwafikisha kwenye macho ya sheria, muda ni mrefu na sisi
wenye taarifa hizi sasa tumeanza kuchoka kusubiri.
“Hawa
watu wanne walihusika kupanga njama ambazo zilipelekea kusababisha
mauaji ya kikatili ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Palm Foundation, Ndugu
Wayle Lotter mwezi Agosti mwaka jana eneo la Chole Masaki mwezi Agosti
mwaka jana.
“Nataka
ndani ya siku hizi saba wawe wamechukua hatua na kama hawatochukua
hatua manaake tutajua wana vested interest (maslahi) kwahivo tutaenda
kuripoti kwa Amiri Jeshi mkuu ambaye ni Mhe. Rais aliyetutuma kazi ya
kusimamia sekta hii,”. Alisema Dk. Kigwangalla.
Dk. Kigwangalla akizungumza katika mkutano huo mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment