NA WAMJW-DAR ES SALAAM.
WATANZANIA
wanatakiwa kwenda vituo vya kutolea huduma za afya kupata vipimo kutoka
kwa wataalam kabla ya kutumia dawa kwa mazoea ili kuepuka usugu wa
vimelea vya wagonjwa kwenye miili yao na kusababisha vifo vya mara kwa
mara.
Hayo
yamezungumzwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mradi wa kupambana na usugu wa
vimelea kutoka Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) Dkt. Raphael Sallu
wakati wa semina na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es
salaam.
“Tatizo
la kutumia vijiuasumu(Antibiotics) bila ya kupata vipimo na ushauri
kutoka kwa wataalamu wa afya limekua kubwa ambalo linasababisha madhara
ya kiuchumi na uhai kutokana na kuzidiwa na vimelea vya ugonjwa ambavyo
vinakua sugu kutokana na matumizi mabaya ya dawa hapa nchini” alisema
Dkt. Sallu.
Aidha,
Dkt. Sallu amesema kuwa elimu ya kutumia dawa bila ya kupata ushauri na
vipimo kutoka kwa wataalamu wa afya ianze kutolewa kuanzia ngazi za
shule ya msingi na ngazi ya jamii kwa ujumla.
Mbali
na hayo Dkt. Sallu amesisitiza kuwa wanahabari wanatakiwa kuwa
kipaumbele katika kuelimisha umma umuhimu wa kutumia dawa kwa kufuata
ushauri kutoka kwa wataalam kuhusu ugonjwa unaomsumbua pamoja na
matibabu yake.
Kwa
upande wake Mratibu wa Taifa wa Mradi wa kupambana na na usugu wa
vimelea kutoka Shirika la Chakula (FAO) nchini Tanzania Dkt. Bachana
Rubegwa amesema kuwa katika kupambana na tatizo hili kunapaswa kuwepo na
matumizi ya hali ya juu ya chanjo ili kuweza kuepuka utumiaji hovyo wa
dawa bila ya vipimo.
“Katika
kupambana na utumiaji wa madawa bila ya utaratibu mzuri ambao
hauhusishi vipimo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya ni lazima
maabara ya kutambua magonjwa sugu ijengwe nchini kwetu” alisema Dkt.
Bachana.
Hata
hivyo Dkt. Bachana amesema kuwa wazilashaji wa chakula na mifugo
wanatakiwa kutumia dawa zinazostahili na sio kutumia antibiotics katika
mifugo yao pamoja na shughuli zao za kilimo ili kuepusha watanzania
walio wengi kutumia vyakula hivyo vyenye usugu wa vimelea vya magonjwa.
Mbali
na hayo Dkt. Bachana ametoa rai kwa watoa huduma za afya nchini kuacha
kutoa dawa ambazo ni feki,zilizokwisha muda na kuwashauri wananchi
kuepuka matumizi ya dawa yasiyo ya lazima ili kuepuka usugu wa vimelea
vya ugonjwa kwenye miili ya watanzania.
Naye
Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) upande wa kupambana na
usugu wa vimelea vya magonjwa Dkt. Rose Shija amesema kuwa watanzania
wanatakiwa kutumia dawa sahihi na kwa wakati kadri alivyoelekezwa na
mtaalam wa afya ili kuepuka matatizo hayo na kujijengea afya bora.
“Tubadili
tabia katika kupunguza maambukizi kupitia chanjo,kuosha mikono kwa maji
safi yanayotiririka,kuepuka ngono zembe na utunzaji salama wa chakula
na sio kutumia dawa bila ya ushauri kutoka kwa wataalam wa afya ili
kuepuka usugu wa vimelea vya magonjwa mwilini” amesema Dkt. Shija.
Mwakilishi
Mkuu wa mradi wa kupambana na usugu wa vimelea (FAO) Dkt. Raphael Sallu
akiwasilisha mchango wake wakati wa semina na Waandishi wa habari
kuhusu matumizi bora ya Antibiotic, ilofanyika katika ofisi za FAO
jijini Dar es salaam.
Mwakilishi
wa Shirika la Afya Duniani (WHO) upande wa kupambana na usugu wa
vimelea vya ugonjwa Bi Rose Shija akiwasilisha mchango mbele ya wadau wa
habari, pembeni yake ni Afisa Habari wa Wizara ya Afya Catherine
Sungura.
Mmoja
ya wadau wa Habari ambae pia ni mmiliki wa Blog ya Full Shangwe akitoa
mchango mbele ya wadau wenzie wa habari na wawakilishi wa Mashirika ya
kimataifa katika Semina ya kuhamasisha matumizi bora ya antibiotic.
Washiriki wa semina hiyo wakifatilia mada mbalimbali.Picha na Emmanuela Massaka, Globu ya jamii.

Post a Comment