Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma
Serikali
imerejesha hati ya Kiwanja Namba 9331 kilichopo kitalu namba 91
Msalato Dodoma kwa mmiliki wake halisi Bw. Sagaf Omari na Bi Madina
Hassan ambao ni wamiliki halali wa kiwanja hicho kilichouzwa kwa Bw.
Lucas Mlay wa Jijini Dar es Salaam kwa shilingi milioni 35 kwa njia
zisizo halali.
Akizungumza
wakati akimkabidhi hati hiyo Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mhe. William Lukuvi amesema kuwa kiwanja hicho chenye ukubwa wa
takribani hekta mbili na nusu kiliuzwa bila mmiliki halali wa kiwanja
hicho kuwa na taarifa kupitia kwa wanasheria wasio waaminifu waliosaidia
kutaka kufanikisha wizi wa kiwanja hicho.
“Niwatahadharishe
Mawakili wote na wanasheria ambao wanashirikiana na watu wasio
waaminifu kutaka kudhulumu viwanja vya wananchi kuwa Serikali ya Awamu
ya Tano itawachukuliwa hatua kali za kisheria na kwa kuanza tutaanza na
hawa mawakili waliofanikisha mchezo huu wakumdhulumu mama huyu na mume
wake kiwanja chao wanachomiliki kihalali” Alisisitiza Lukuvi
Akifafanua
Waziri Lukuvi amesema kuwa Wizara yake imejiridhisha kuwa nyaraka
zilizowasilishwa ili kubadilisha umiliki wa kiwanja hicho ni za kughushi
na wamiliki halali wa kiwanja hawakuwa na taarifa kuhusu kuuzwa kwa
kiwanja chao hadi walipopata taarifa kwa majirani na kuamua kuchukua
hatua kwa kuwasilisha malalamiko yao katika Ofisi yake.
“Nimechukua
hatua na tayari yule mwanasheria aliyehusika katika kughushi nyaraka za
kiwanja hiki na kukiuza ameshakabidhiwa kwa vyombo vya dola kwa hatua
zaidi hivyo ni vyema watu wote wenye nia yakudhulumu viwanja vya
wananchi masikini wakaacha tabia hiyo mara moja kwani Serikali ya Awamu
ya Tano itawachukulia hatua kali mara moja ili kukomesha tabia hii
”Alisisitiza Mhe. Lukuvi
Kwa
upande wake Bi. Madina Hassan akipokea hati ya Kiwanja hicho
amemshukuru Waziri Lukuvi kwa hatua anazochukua katika kuhakikisha
wanyonge wanapata haki hasa pale panapojitokeza watu wanaojaribu
kudhulumu viwanja vya wananchi masikini .
“Kwa
kweli naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano jinsi inavyotusaidia
wanyonge ili tupate haki zetu hasa katika sekta hii ya ardhi nawaombea
kwa Mungu ili awalinde Viongozi hawa” alisisitiza bi Madina.
Kwa
upande wake mnunuzi wa Kiwanja hicho Bw. Lucas Mlay amesema kuwa
hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya sheria na hakutambua kuwa
hati za kiwanja hicho zilikuwa zimeghushiwa na kuongeza kuwa angetambua
hilo asingelipa zaidi milioni 35 ili kununua kiwanja hicho.
Naye
Msajili wa Hati wa Wizara hiyo Bw. Geofrey William amesema kuwa ni
vyema wananchi hasa katika Mkoa wa Dodoma wakachukua hatua kujiepusha na
utapeli wa viwanja unaoendeshwa na baadhi ya watu hasa kwa viwanja
ambavyo havijaendelezwa kwa muda mrefu.
Aliongeza
kuwa kumekuwa na wimbi la watu kuwasilisha maombi ya kupotelewa na hati
ili kufanya mchakato wa kubadili umiliki wa viwanja ikiwa ni sehemu ya
mbinu zinazotumiwa na matapeli.
Tangu
Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani imekuwa ikichukua hatua
mbalimbali kukomesha vitendo vya kuwazulumu wananchi masikini viwanja,
mashamba na maeneo ya umma ikiwa ni moja ya mikakati yake kuhakikisha
kuwa wanachi wote wanapata haki sawa bila kujali hali ya kipato au
wadhifa.

إرسال تعليق