Serikali
kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeahidi kutoa
timu ya wataalamu watakao suluhisha mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya
Mkalama Mkoani Singida na Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara.
Naibu
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula ametoa
ahadi hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Singida katika kijiji cha Singa
tarafa ya Kinampundu Wilayani Mkalama ambapo amesema Wizara yake itatoa
wataalamu watakaoweza kutatua mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka
30.
“Kwakuwa
pande zote mbili za Mkalama na Hanang’ zimekutana mara kadhaa bila
mafanikio, nitaleta wataalamu wafike eneo la mpaka ili wataalam hao
wawasomee alama moja baada ya nyingine, kila mmoja wenu afahamu eneo
lake mwisho ni wapi, nadhani hapo tutakuwa tumewasaidia wananchi wetu”,
amesema Dkt Mabula.
Amesema
wananchi wa Kijiji hicho cha Singa wasiwe na wasiwasi endapo baada ya
kuonyesha mpaka wao mashamba yao yakionekana yapo wilaya ya Hanang’
wataruhusiwa kuendelea kuyamiliki ila watatakiwa kwenda kujitambulisha
katika Uongozi wa Wilaya hiyo.
Aidha
Dkt Mabula amesema timu hiyo ya wataalamu itahakikisha inasuluhisha
migogoro yote ya mipaka ya wilaya hiyo ambayo ngazi ya wilaya
imeshindikana kutatuliwa.
Amewashauri
wananchi hao kutouza au kugawa ardhi yao ovyo ovyo kwakuwa ardhi ni
mali na mtaji popote pale hata kama ni vijijini hivyo watunze ardhi yao
na kuiongezea thamani kwa kuipima na kuwa na hati ya umiliki.
Baadhi
ya wananchi wa kijiji hicho walitoa malalamiko kwa Naibu Waziri huyo
huku wakimueleza kuwa mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu umesababisha
baadhi yao kupelekwa mahakamani kwa madai ya kuvamia mashamba.
Mzee
Anaftali Amosi Majii amemueleza Naibu waziri kuwa taarifa za mgogoro huo
zilitolewa muda mrefu na kuongeza kuwa wananchi wamechoka kushitakiwa
kwa makosa ya uvamizi wa mashamba wakati wao wanaamini wanayamiliki kwa
uhalali jambo ambalo linawachelewesha kimaendeleo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama Mhandisi Geofrey Sanga
amesema Wilaya ya Mkalama ina migogoro ya mipaka kwa wilaya tano
zinazowazunguka.
Mhandisi
Sanga ameeleza kuwa Mkalama ina migogoro ya mipaka kati yake na Wilaya
za Mbulu, Iramba, Hanang’ na Wilaya ya Singida jambo ambalo linawafanya
baadhi ya wananchi kukwepa kuchangia shughuli za maendeleo wakidai wao
sio wa Wilaya hiyo.
Wakati
huo huo Naibu Waziri Dkt Angelina Mabula amefanya ziara Wilaya ya
Iramba na kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika masijala ya Ardhi ya
Wilaya hiyo ambapo hakuridhishwa na utunzaji wa nyaraka pamoja na
utendaji usioridhisha unaosababisha wananchi kuchelewa kupata hati za
viwanja.
Dkt
Mabula pia hakuridhishwa na kasi ndogo ya upimaji viwanja na utoaji wa
hati wilayani humo huku akiwataka kuacha kukusanya kodi mbalimbali za
ardhi kwa utendaji wa kimazoea bali wafanye kazi bidii.
Naibu
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula
akizungumza na wataalamu wa ardhi, viongozi na watendaji wa halmashauri
ya Wilaya na Manispaa ya Singida [hawapo pichani], Kulia kwake ni Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi.
Naibu
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula
akizungumza na wananchi wa kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu
Wilayani Mkalama, Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi
Jaksoni Massaka.
Naibu
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula
akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Ardhi wa Wilaya ya Iramba Lugano
Sanga kuhusu utuzanji wa nyaraka za idara hiyo.
Naibu
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula
akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi hati ya kumiliki
kiwanja chake kilichopo Mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment