Pages

August 6, 2017

SERIKALI YAOMBWA KUDHIBITI KONOKONO WAHARIBIFU WA MAZAO MKOANI LINDI


Mwezeshaji kutoka Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAB), Dk.Emmarold Mneney (kulia), akitoa mafunzo ya siku moja ya kilimo  kwa wakulima wa Mkoa wa Lindi kwenye Maonyesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Ngongo mkoani hapa jana. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)

Wakulima wakiwa kwenye mafunzo hayo
Utambulisho ukifanyika.
Ofisa Kilimo na Umwagiliaji wa Wilaya ya Kilwa, John Ignas Mkinga, akifungua mafunzo hayo.
Wakulima wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mkulima Jakazi Ali kutoka Kilwa akielezea masoko ya kuuza mazao yao yalivyo na changamoto.
Mkulima Rashid Hassan kutoka Lindi vijijini akielezea jinsi konokono wanavyoathiri mazao yao.
Mkulima Saada Makota kutoka Wilaya ya Nachingwea akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
Betty Milanzi mkulima kutoka Wilaya ya Nachingwea akielezea changamoto za kilimo wanazokumbana nazo.
Mkulima Mwanajumbe Nchuwa kutoka Kilwa akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk. Philbert Nyinondi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA), akiwaeleza wakulima hao umuhimu wa kutumia simu zao kupata masoko ya mazao yao na kuwasiliana na wakulima wenzao katika masuala ya kilimo.



Na Dotto Mwaibale, Lindi

WAKULIMA wa Mkoa wa Lindi wameiomba serikali kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti konokono ambao wametajwa kuwa ni tishio kwa uharibifu wa mazao ya chakula na biashara mkoani humo.

Ombi hilo walilitoa katika mafunzo ya siku moja ya kilimo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika maonyesho ya kitaifa ya wakulima Nanenane yanayoendelea viwanja vya Ngongo mkoani hapa jana.

"Tunachangamoto nyingi katika kilimo lakini kubwa zaidi ni konokono ambao wapo katika mashamba yetu ambao wanashambulia mimea ikiwa michanga na hata tukiwaua wamekuwa wakiongezeka jambo ambalo linatukatisha tamaa" alisema Rashid Hassan mkulima kutoka wilaya ya Lindi vijijini.

Alisema hawajui konokono hao wanatoka wapi na wafanyeje ili kumaliza changamoto hiyo ambayo imekuwa ni kilio kikubwa kwa wakulima wa mkoa huo kwani konokono hao wamekuwa wakila majani ya mmea ambayo ni machanga.

Mkulima Saada Makota kutoka Wilaya ya Nachingwea alisema changamoto waliyo nayo kucheleweshewa kufika kwa pembejeo za kilimo kwa wakati na ugonjwa wa kutu unaoshambulia mikorosho na kuifanya ikauke majani yake kwa juu.

"Pembejeo za kilimo tunaletewa mwezi wa tatu wakati mvua zimeanza kunyesha badala ya mwezi wa Desemba jambo ili linaturudisha nyuma wakulima" alisema Makota.

Mwanajumbe Nchuwa mkulima kutoka Kijiji cha Luato wilayani Kilwa alilamikia bei ya ufuta kushushwa na walanguzi kutoka sh.2000 kwa kilo hadi 1500 kwa mtindo wa choma choma.

Mkulima Betty Milanzi kutoka Kijiji cha Nammanga Nachingwea alisema changamoto nyingine waliyonayo ni wanyama waharibifu wa mazao yao kama nyati, tembo, nguruwe hivyo wakaomba serikali kupitia idara ya wanyapori iwasaidia kumaliza changamoto hiyo.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Jukwaa la Bioteknolojia kwa maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk. Hamalord Mneney aliwataka wakulima hao kubadilika na kulima kilimo chenye tija na kufuata maelekezo ya wataalamu badala ya kuendelea na kilimo ambacho hakina manufaa kwao.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kubadilishana uzoefu na kuona ni jinsi gani sayansi na teknolojia inavyoweza kutumika katika kilimo cha kisasa katika mazao yote ya chakula na biashara yanayolimwa katika mkoa huo.

Mkulima Saada Makota aliomba muda wa mafunzo hayo uongezwe ili waweze kupata fursa zaidi ya kujifunza na kupeleka elimu hiyo kwa wakulima waliowengi katika maeneo yao.


Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Philbert Nyinondi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA), aliwataka wakulima hao kutumia simu zao kutafuta masoko ya mazao yao na kupeana taarifa mbalimbali ili kukabiliana na changamoto wanazo kabiliana nazo katika kilimo.


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...