Pages

August 5, 2017

AfDB YAISAIDIA SERIKALI KUWAONDOLEA WAKAZI WA ARUSHA ADHA YA UMEME KUKATIKA MARA KWA MARA




Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Kupoozea Umeme cha Njiro Mkoani Arusha, Mhandisi Lembrice Mollel, akitoa maelezo kuhusu mitambo ya Kituo hicho kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt Nyamajeje Weggoro (kulia) alipotembelea Kituo hicho kukagua mradi wa kusambaza umeme uliofadhiliwa na AfDB, uliogharimu Dola milioni 4.2, Jijini Arusha
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt Nyamajeje Weggoro (wa pili kulia) akipewa maelekezo ya namna mitambo ya usambazaji umeme katika Kituo cha Njiro Jijini Arusha inavyoendeshwa kwa mfumo wa Kidigitali. Mitambo hiyo imefadhiliwa na Benki ya AfDB ukiwa ni mkopo wenye masharti nafuu.
Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Umeme cha Njiro Mkoani Arusha, Mhandisi Lembrice Mollel (kulia) akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki Dkt Nyamajeje Weggoro (katikati) alopotembelea Kituo cha kusambaza umeme cha Njiro Jijini Arusha. Mitambo hiyo imefadhiliwa na Benki ya AfDB. Kushoto ni Meneja wa Mradi wa umeme wa AfDB Mhandisi Florence Gwang’ombe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro (kushoto) akipata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa Kituo cha Kupoozea Umeme cha Njiro, Mkoani Arusha, kuhusu usalama wa mitambo kutakapo tokea dharula. Mitambo hiyo imefadhiliwa na Benki ya AfDB, ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu.




Muonekano wa mitambo iliyofadhiliwa na Benki ya Maedeleo ya Afrika (AfDB), katika kituo cha kusambaza umeme cha Njiro, Mkoani Arusha. Mitambo hiyo imesaidia kupatikana kwa umeme wa ziada wa Megawati 70.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt Nyamajeje Weggoro akizungumza na Msimamizi wa Kituo cha usambazaji umeme cha Njiro-Arusha, Mhandisi Lembrice Mollel na wengine (hawapo pichani) baada ya kutembelea mradi huo na kuridhishwa na matokeo ya mradi huo kwa wakazi wa Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt Nyamajeje Weggoro (kushoto) na Mshauri wake Amos Cheptoo wakionesha kufurahishwa na ufanisi wa mradi wa kusambaza umeme wa Njiro Jijini Arusha baada ya kukagua na kujiridhisha na thamani ya mradi huo uliofadhiliwa na Benki yake kwa gharama Dola milioni 4.2.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

……………………….

Na Benny Mwaipaja, WFM-Arusha

WAKAZI wa Jiji la Arusha wameondokana na na adha ya umeme kukatika mara kwa mara baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme katika Kituo cha kupoozea umeme cha Njiro kilichoko Mkoani Arusha chenye uwezo wa kuzalisha megawati 130.

Hali hiyo inatokana na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB kuwekeza kiasi cha Dola milioni 4.2, ukiwa ni mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili kuongeza uwezo wa Kituo hicho kuzalisha umeme unaotumika kwa ajili ya makazi ya watu, maeneo ya biashara na viwanda.

Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Usambazaji umeme cha Njiro Mhandisi Lembrice Mollel amesema mradi huo umesaidia kuongeza Megawati 130 za umeme ambao umekidhi mahitaji ya Jiji la Arusha linalo hitaji Megawati 60 hivyo kubakiwa na Umeme wa ziada kiasi cha Megawati 70.

Alisema kuwa tatizo la kukatika katika kwa umeme katika mji huo wa kitalii na kibiashara litakuwa historia na kwamba umeme unaozalishwa kituoni hapo unasafirishwa kwenye maeneo mengine yenye uhitaji ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Umeme wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhandisi Frorence Gwang’ombe amesema kuwa lengo la mradi lilikuwa kupatikana kwa umeme wa uhakika na kuimarisha miundombinu ya usambazaji na kupooza umeme jambo ambalo limefikiwa kikamilifu.

Alisema kuwa uboreshaji wa Kituo hicho cha kupoozea Umeme cha Njiro ni sehemu ya utekelezaji wa uboreshaji wa Sekta ya Umeme nchini kupitia mradi ujulikana kama Electricity V, uliofadhiliwa na AfDB kupitia mkopo nafuu wa kiasi cha Dola milioni 8, ukihusisha pia mkoa wa Dar es Salaam, Vituo vya kupooza umeme vya Sokoine na Ilala.

“Mradio huu umelenga kuwahudumia wananchi takribani 8,400 hivyo kukamilika kwa mradi huo ni neema kwa wananchi wengi kwa kuwa utasaidia kuimarisha uwezo wao wa kibiashara ndani ya Jiji la Arusha na maeneo mengine ya nchi” alisema Mhandisi Gwang’ombe

Alifafanua kuwa uboreshaji wa mradi wa Kituo cha Kupooza Umeme cha Njiro umehusisha ufungaji wa transfoma mpya 2 zenye uwezo wa kufua megawati 50 kila moja na nyingine 2 zenye uwezo wa kubeba megawati 15 kila moja, hatua iliyosaidia kuongeza kiwango hicho cha umeme.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), anayehudumia Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, ameelezea kuridhishwa na utekelezaji pamoja na manufaa ya mradi huo utakaosaidia kukuza biashara na kusisimua uwekezaji wa viwanda katika mkoa wa Arusha.

‘Arusha ni mji wa Kitalii hivyo unahitaji kuwa na umeme wa kutosha utakaosaidia katika uwekezaji na ufanisi wa biashara, upatikanaji wa umeme wa uhakika utachochea shughuli za Kilimo na viwanda kwa kasi kubwa’, aliongeza Dkt. Weggoro.

Amewataka wakazi Arusha na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya umeme ili kwenda sambamba na Sera ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Baadhi ya wakazi wa Mji wa Arusha, wakiwemo Bw. Jackson William na Bw. Steven Chitara wamekiri kuwa maisha yao yamebadilika kiuchumi kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa umeme ikilinganishwa na hapo awali.

Wamesema kuwa vijana wengi wamejiajiri kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zinazotegemea uwepo wa nishati hiyo kama kuchomelea vyuma, vinyozi, ufundi wa aina mbalimbali pamoja na wafanyabiashara wakubwa kuanza kuvutiwa kuwekeza mkoani humo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...