Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG )wa Serikali ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Prof Mussa J Assad wa pili kutoka kushoto akiwa na
wajumbe wa Bodi ya Umoja wa Mataifa baada kikao cha 71 kinachoendelea
mjini New York Marekani, kikao hicho kinafanyika kwa muda wa siku mbili.
Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG) za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Profesa Mussa Assad ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya
Umoja wa Mataifa (UNBoA), jana tarehe 25 Julai, 2017 ameshiriki
kuidhinisha ripoti za kaguzi za shughuli za Umoja wa Mataifa kwa mwaka
ulioishia tarehe 31 Desemba 2016, kwenye kikao cha 71 cha Bodi ya
Ukaguzi ya wanachama wa Umoja wa Mataifa kinachoendelea Mjini New York,
nchini Marekani.
Katika
kikao hicho, wajumbe wa bodi hiyo walipitia na kusaini ripoti ishirini
na nane (28) za ukaguzi wa shughuli za Umoja wa Mataifa. Kati ya ripoti
zilizoidhinishwa na wajumbe wa Bodi hiyo, ripoti kumi na moja (11)
zilitokana na kaguzi zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu
za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (NAOT) na kuwasilishwa
na CAG, Prof. Mussa Assad kwenye kikao hicho cha Bodi. Aidha, ripoti
kumi na saba (17) zilizosalia zilitokana na ukaguzi uliofanywa na Ofisi
za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali za India na Ujerumani.
Katibu
Mkuu umoja wa Mataifa Bwana Antonic Guterres akizunguza na wajumbe wa
Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Taifa katika kikao cha Bodi kilichofanyika
mjini New York Marekani hivi karibuni.
Ripoti
kumi na moja zilizowasilishwa na Prof. Assad ni kaguzi za Shirika la
Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Idadi ya Watu
Duniani la Umoja wa Mataifa (UNFPA), Shirika la Ujenzi na Misaada la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi wa Palestina na Mashariki
(UNRWA), Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa UNRWA Wakazi (UNRWA – SPF),
Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake
(UN – Women), Mfuko wa Ukuzaji Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF),
Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN Habitat), Shirika
la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Mahakama ya Umoja wa Mataifa
inayoshughulika na Mauaji yaliyotokea Rwanda (ICTR), Mahakama ya Umoja
wa Mataifa inayoshughulika na Mauaji yaliyotokea Yugoslavia ya zamani
(ICTY), Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kupunguza shughuli za mahakama za
kimataifa (IRMCT).
Matukio
mengine yaliyofanywa na Bodi hiyo ni pamoja na wajumbe wa Bodi
kushiriki katika haflailiyowakutanisha na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Mhe. António Guterres. Katika hafla hiyo Mhe. Guterres
aliwajulisha wajumbe wa UNBoA kuwa Umoja wa Mataifa unafanya marekebisho
makubwa ya kimuundo na kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kugatua na
kukasimu madaraka kwenda ngazi za chini ikiwemo ofisi zilizopo kwenye
kanda, kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi bila ya kudhoofisha
udhibiti.
‘UN
inaendelea kufanya maboresho yanayolenga kuimarisha Umoja wa Mataifa
katika nguzo zake zakitendaji ikiwemo kuimarisha amani na usalama, haki
za binadamu, na maendeleo duniani’, alisema Mhe. Guterres. Aidha
alisisitiza kuwa, UN itaendelea kuimarisha usawa na kupinga unyanyasaji
ya kijinsia. ‘hatua kadhaa zimeendelea kuchukuliwa ikiwemo kuimarisha
uwazi na uwajibikaji na pia kuwalinda watoa taarifa za maovu. Ninafahamu
umuhimu wa wakaguzi katika kusaidia kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa
na ni kiungo muhimu cha kutoa taarifa kwa nchi wanachama juu ya
matumizi ya rasilimali za Umoja wa Mataifa’, alihitimisha, Mhe.
Guterres.
Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyekaa katikati Bwana Antonic Guterres
akibadilishana mawazo na wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa
katika kikao cha 71 cha bodi hiyo, kilichofanyika mjini New York
Marekani.
Wajumbe
wa Bodi pia walifanya kikao na Mkuu wa Ofisi ya Sekretariati ya Umoja
wa Mataifa (Chef de Cabinet) Bibi. Maria Luiza Ribeiro Viotti
kilichogusia maboresho yanafanywa katika Umoja wa Mataifa ambapo Prof.
Assad akiwakilisha wajumbe wenzake wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa
Mataifa alimfahamisha Bibi. Ribeiro kuwa wataendelea kutoa mchango
chanya kwenye maboresho yanayofanywa na Umoja wa Mataifa. Aidha, aliomba
Umoja wa Mataifa kuendelea kutoa elimu ya kutosha na kuboresha
mawasiliano kati yake na wafanyakazi wake na wadau ili kufikia mafanikio
yanayotarajiwa.
Prof.
Assad na ujumbe wake kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, ulifanya
mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa
Mhe. Balozi Modest J. Mero, kwenye Ubalozi wa Tanzania uliopo mjini New
York, Marekani ambapo alimshukuru Mhe. Balozi Modest J. Mero na Ofisi ya
Uwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kutoa msaada
mkubwa kurahisisha shughuli za maafisa wa Ofisi ya Ukaguzi. ‘Ninapenda
kutoa shukrani zangu za dhati kwa mchango wenu ambao kwa kweli umekuwa
kiungo muhimu katika kufanikisha shughuli hizi za Ukaguzi wa Umoja wa
Mataifa’, alisema Prof. Assad.
Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano waTanzania Prof Mussa J Assad akisalimiana na Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa Mr Antonic Guterres wakati wa kikao cha 71 cha bodi ya
wakaguzi kilichofanyika nchini Marekani.
Aidha
alifafanua kuwa, Ofisi imefanikiwa kutoa ripoti kwa wakati kwa miaka
mitano mfululizo tangu ijiunge na Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa
mwaka 2012. Mhe. Balozi Modest J. Mero alimshukuru CAG kwa taarifa na
kutoa rai kwa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuendelea kuangalia
fursa za ukaguzi katika medani za kimataifa ili kuimarisha na
kuendeleza ujuzi na uzoefu uliokwishajengeka kwa miaka yote hiyo.
‘Kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri, kwa kweli mnaipa nchi heshima kubwa,
hata hivyo niwashauri kuwa ni vyema mkaendelea kutafuta kazi kwenye
mashirika mengine ya kimataifa ili kuendeleza ujuzi huo’, alisema Mhe.
Balozi Mero.
Bodi
ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa inaundwa na wajumbe watatu, wanaopaswa
kuwa wakaguzi wakuu wa serikali kutoka nchi wanachama wa Umoja wa
Mataifa. Kikao cha mwaka huu kimehudhuriwa na wajumbe wote ambao ni
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali ya India na mwenyekiti wa
Bodi hiyo, Bw. Shashi Kant Sharma, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali ya Ujerumani, Bw. Kay Scheller, na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Mussa J.
Assad.
Tanzania
ni nchi ya tatu ya Afrika kuwahi kuwa mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya
Umoja wa Mataifa iliyoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka
1946. Nchi zingine za Kiafrika ni Ghana na Afrika ya Kusini.
Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonic Guterres akisalimiana na Rais wa
Wakaguzi nchini Ujerumani Bwana Amys C.E Morse katika kikao cha 71 cha
bodi ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kilichofanyka nchini Marekani.
No comments:
Post a Comment