MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu Mfanyabiashara Shabani Hussein (44)
maarufu kama "Ndama mtoto ya Ng'ombe" kulipa faini ya milioni 200 au
jela miaka mitano baada ya kukiri shtaka la sita la kutakatisha fedha
ambazo ni dola za Marekani 540,000.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi, Mkuu wa mahakama hiyo Victoria Nongwa.
Kabla
ya hukumu hiyo kusomwa, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili
Mwandamizi wa Serikali, Christopher Msigwa alimsomea maelezo ya awali
(PH), Ndama dhidi ya shtaka lake hilo na kukiri.
Hatua
hiyo ya Ndama kusomewa hukumu katika shtaka moja tu la utakatishaji wa
fedha kati ya matano yanayomkabili limekuja baada ya wiki iliyopita
kuomba kukumbushiwa mashtaka yake na kukiri shtaka hilo la utakatishaji
wa fedha.
Akisoma
hukumu hiyo, hakimu Nongwa amesema mahakama imezingatia hoja za upande
wa mashtaka na ule wa utetezi ambapo upande wa mashtaka uliiomba
mahakama kwa mujibu wa sheria ya kutakatisha fedha kifungu cha 13
(a)cha Sheria ya kuzuia utakatishaji fedha, kumpa adhabu kali
mshitakiwa kwa kuwa makosa hayo yanalenga kudidimiza uchumi wa nchi.
Amesema,
mshitakiwa anastahili faini kwa kuwa ameipunguzia garama mahakama
kuhusu shughuli za uendeshaji wa kesi hiyo ikiwemo gharama za kuleta
mashahidi katika shtaka hilo
Ameongeza
kuwa, Sheria hiyo ipo kwa ajili ya kuonesha kuwa makosa kama hayo
hayatakiwi kumnufaisha mkosaji hivyo, atatakiwa kulipa faini ya milioni
200 na asipolipa ataandikiwa hati ya kifungo cha miaka mitano jela.
Kabla
ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili Msigwa alidai hawana kumbukumbu ya
makosa ya nyuma ya mshitakiwa na ni rai ya jamhuri kwamba mahakama
imuadhibu mshitakiwa kuzingatia sheria ya kuzuia utakatishaji fedha.
Wakili
wa utetezi, Wabeya Wakung'i aliomba mahakama impunguzie adhabu
mshitakiwa kwa kuwa ni kosa lake la kwanza, familia yake inamtegemea pia
mshitakiwa hakuonesha usumbufu na kwamba kukiri kwake kosa ni ishara
ya kujutia kosa.
Katika
shtaka hilo la sita, Ndama anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi
2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa Kampuni ya
Muru Platinum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni
hiyo iliyoko kwenye Benki ya Stanbic alijihusisha moja kwa moja kwenye
uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha
hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujiapatia fedha kwa njia ya
udanganyifu.
Katika
maelezo ya awali, Wakili Msigwa alidai Ndama ni mkazi wa Mbezi Beach na
kwamba Mei 14, 2013, Bushoboka Mutamola na Majibu Taratibu walisajili
Brela Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Co. Limited na kupata
hati ya usajili namba 992449 kwa ajili ya kujishughulisha na biashara
ya madini.
Alidai
Septemba 16,2013 kampuni hiyo ilifungua akaunti ya fedha za kigeni
Benki ya Stanbic tawi la Viwanda na kupewa akaunti 9120000085152.
Imedaiwa
kuwa, wakati wa ufunguzi wa akaunti hiyo, Ndama alijitambulisha kama
Mwenyekiti mtiaji saini pekee kwenye benki hiyo ambapo aliwasilisha
nyaraka mbalimbali ikiwemo barua ya utambulisho wa Kampuni, leseni ya
biashara, namba ya utambulisho wa biashara (TIN) ambazo zilipokelewa
mahakamani hapo.
Pia
inaelezwa, Februari, 2014 Ndama na wanahisa wenzake waliingia
makubaliano na Kampuni ya Australia iitwayo Trade TJL PTYL Limited
wakijaribu kuonesha kuwa watauziana dhahabu kilogramu 207 zenye thamani
ya dola za Marekani Milioni 8.2.
Wakidai
watatimiza masharti ya mikataba waliandaa nyaraka za uongo ambazo ni
kibali cha kusafirisha madini kwenda Australia, waliandaa kibali cha
Umoja wa Mataifa kuonesha kuwa dhahabu hizo hazina jinai yoyote namba
28092 iliyoandaliwa Februari 20,2014, kuonesha wamelipa dola za Marekani
331,200 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama kodi ya usafirishaji "
alidai Msigwa.
Pia
alidai Ndama alimtaarifu mlipaji ambayo ni Kampuni ya Trade, kulipa
fedha kupitia akaunti hiyo yenye jina la Muru ambapo baadae kampuni hiyo
iliamini taarifa hizo na kulipa dola za Marekani 540,390 kwa tarehe
tofauti.
Licha ya kukubali mashitaka hayo, Ndama alikana makosa mengine yakiwemo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
baada
ya ndama kukiri shtaka hilo la utakatishaji wa fedha ambalo halina
dhamana, Hakimu Nongwa amemsomea masharti ya dhamana katika mashtaka
mengine yaliyobakia ya kughushi na kutoa nyaraka za uongo, ambapo
ametakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya milioni 600
au hati isiyohamishika ya kiasi hicho.
Kesi hiyo itatajwa tena Juni 16 mwaka huu.
Ndama amebakiwa na mashtaka matano yakiwemo manne ya kughushi na moja la kujipatia fedha kwa njuia ya udanganyifu.
No comments:
Post a Comment