Kiongozi wa
Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amekutana na Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Al Azhar cha Misri Sheikh Ahmad Tayyib katika kongamano la amani
duniani ambalo limefanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Cairo.
Akizungumza
katika kongamano hilo, Sheikh Ahmad Tayyib amesema sababu kuu ya kuibuka
ugaidi ni biashara ya silaha na mikataba yenye kutiliwa shaka ya
silaha ambayo hutekelezwa baada ya maazimio ya kidhalimu ya kimataifa.
Kabla ya kuanza hotuba yake, Sheikh Tayyib aliwataka hadhirina kusalia
kimya kwa muda wa dakika moja kwa ajili ya kutoa heshima zao kwa
waathirika wa ugaidi Misri na dunia nzima.
Akizungumza
katika kongamano hilo la amani duniani, Papa Francis alisema amani
haiwezi kupatikana pasina kuwapa vijana mafunzo ya kuheshimiana na
kufanya mazungumzo na majadiliano yenye faida.
Kiongozi wa
Kanisa Katoliki Duniani amesema mustakabali wa jamii ya mwanadamu
utajengeka katika msingi wa mazungumzo baina ya dunia na tamaduni na
kuongeza kuwa kuna ulazima wa kufanyika mazungumzo baina ya dini ili
kufanikisha amani na kukabiliana na malumbano.
Safari ya Papa nchini Misri inafanyika katika mazingira ya ulinzi mkali
ikiwa ni wiki tatu tu baada ya hujuma za kigaidi zilizolenga makanisha
ya Kikhufti nchini Misri.
No comments:
Post a Comment