Pages

May 24, 2017

Msajili Wa Vyama Vya Siasa Apongezwa Kwa Kusimamia Sheria Na Kanuni.

Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi akizungumza na Viongozi wa Vyama vya Siasa na watendaji wao wakati wa mkutano wa siku moja uliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam kujadili na kuweka mikakati ya kuondoa mapungufu yanayojitokeza katika kutekeleza Sheria na Kanuni za usajili wa vyama vya Siasa hapa nchini. Kushoto ni Msajili Msaidizi Bw. Sisty Nyahoza na kulia ni Msajili Msaidizi Bi. Piencia Kiure.
Msajili wa vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi akisisitiza jambo kwa viongozi wa vyama vya Siasa (hawapo pichani),wakati wa mkutano wa siku moja na viongozi hao leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Msajili Msaidizi Bw. Sisty Nyahoza.

Msajili Msaidizi Bw. Sisty Nyahoza akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayovihusu vyama vya siasa ikiwemo utekelzaji wa Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992.

Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Chama cha CCK Bw. Renatus Muhabi mara baada ya kumaliza mkutano wa siku moja uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam ikiwa ni utaratibu ulioanzishwa na Msajili wa vyama vya siasa kukutana na viongozi wa vyama hivyo na watendaji wao.

Katibu Mkuu wa Chama cha UDP Goodluck Ole Medeye akipongeza utaratibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa kusimamia sheria na kanuni zinazosimamia vyama vya siasa ikiwemo kufanyika kwa ukaguzi wa mahesabu katika vyama vyao.

(Picha na Frank Mvungi-Maelezo)

……………………..

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imepongezwa kwa kusimamia vyema Sheria na Kanuni zinazoongoza vyama vya Siasa hapa nchini hali inayochochea kukua kwa demokrasia.

Akizungumza katika mkutano wa kawaida wa siku moja iliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa, Katibu Mkuu wa Chama cha UDP Dkt. Goodluck Ole Medeye amesema utaratibu wa kuvisimamia vyama na kuvikagua ili kuhakikisha kuwa vinazingatia Sheria na Kanuni ni mzuri na ni wa kupongezwa.

“Napongeza kwa kazi nzuri ya kukagua hesabu za vyama inayofanywa na mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa vyama vinavyopata ruzuku na visivyopata ruzuku hali ambayo inachochea uwajibikaji katika vyama ” alisisitiza Ole Medeye.

Akifafanua Ole Medeye amesema kuwa Serikali kupitia Msajili wa vyama vya Siasa anafanya kazi nzuri ya kuhakikisha kuwa kila chama kinafuata taratibu na kuomba ofisi hiyo kuendeleza utaratibu wa kukutana na viongozi wa vyama na wale wanaosimamia rasilimali za vyama kwa lengola kuhakikisha kila kimoja kinatimiza na kufuata sheria na kanuni zilizowekwa.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ADA – TADEA, Bibi Ziada Athumani amesema ukaguzi unaofanywa na CAG katika vyama umekuwa sehemu ya elimu kwa watunza hazina na vyama hivyo na hivyo anapongeza utaratibu huo na kuomba ushirikiano zaidi kutoka Ofisi ya Msajili, vyama vya siasa na CAG ili kusaidia kazi ya ukaguzi.

“Msajili wa Vyama vya Siasa ni mlezi na msimamizi wa vyama vya Siasa hapa nchini hivyo tunayo kila sababu ya kumpongeza kwa kuwa anasimamia sheria vizuri , hivyo tumuunge mkono kwa kuzingatia taratibu, sheria na kanuni zilizopo,”alisisitiza Bi Ziada.

Kwa upande wake Msajili wa Vyama vya Siasa Mhe. Jaji Francis Mutungi amesema kuwa Ofisi yake itaendeleza utaratibu wa kukutana na viongozi wa vyama vya Siasa ili kujadiliana na kukumbushana sheria na taratibu zinazosimamia vyama hivyo.

Aliongeza kuwa utaratibu huo unaimarisha uhusiano na vyama hivyo na pia Ofisi yake inapata fursa ya kubaini changamoto zinazojitokeza wakati wa ukaguzi wa hesabu za vyama hivyo hali inayosaidia kuweka mikakati ya pamoja katika kuzitatua kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali.

Pia Jaji Mutungi aliviasa vyama vya siasa kuendelea kuzingatia taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya Siasa.

Kwa upande wake Msaidizi wa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali Bw. Majura Blugule amesema Ofisi hiyo itaendelea kushirikiana na vyama pamoja na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ili kuhakikisha kuwa hesabu za vyama hivyo zinakaguliwa kwa kuzingatia sheria na kanuni.

Utaratibu wa Msajili wa vyama vya Siasa kukutana na vyama hivyo umeanzishwa hivi karibuni kwa nia ya kuangalia changamoto zinazojitokeza kati ya pande hizo mbili na jinsi ya kuzitatua. Takribani vyama 17 vilishiriki katika warsha.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...