Meneja
Udhibiti Ubora wa Makaa ya Mawe wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania
Limited Bw. Bosco Mabena akielezea moja ya majukumu wayafanyayo katika
Kitengo cha Udhibiti Ubora wa makaa ya mawe yanayochimbwa kutoka mgodi
wa makaa hayo uliopo Ngaka, Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10 Mei, 2017.
Baadhi ya
Malori katika eneo la Kitai Wilayani Mbinga, Mkoani Ruvuma yakiwa
yamepakiwa makaa ya mawe yakifungwa maturubai kwa ajili ya kuzuia makaa
ya mawe hayo kunyeshewa na mvua ikiwemo kuchafuliwa na aina yoyote ya
uchafu wakati wa kuyasafirisha makaa hayo 10 Mei, 2017.
Lori
lililopakia makaa ya mawe katika eneo la Kitai Wilayani Mbinga, Mkoani
Ruvuma likipimwa uzito kabla ya kwenda kufungwa turubai tayari kwa
kuanza safari ya kupeleka makaa hayo kwa mteja wake, 10 Mei, 2017.
Naibu
Meneja wa Mgodi wa Kampuni ya Tancoal Energy Limited (wa pili kulia) Bw.
Edward Mwanga, Meneja Udhibiti Ubora wa Makaa ya Mawe wa Kampuni ya
Tancoal Energy Tanzania Limited Bw. Bosco Mabena (wa pili kushoto),
Afisa Mauzo na Usafirishaji wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania
Limited, Bi. Leahkissa Mwangosi pamoja na Meneja Mawasiliano Shirika la
Taifa la Maendeleo (NDC) (kulia) wakielekea katika eneo la mzani wa
kupimia malori katika eneo la Kitai Wilayani Mbinga, Mkoani Ruvuma 10
Mei, 2017.
Kijiko
kikifanya kazi ya kuchimba makaa ya mawe katika mgodi wa makaa ya mawe
uliopo eneo la mgodi wa Ngaka Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10 Mei,
2017.
Baadhi ya
Wataalam toka Kampuni ya Tancoal Energy Limited, wakiwa wameongozana na
Waandishi wa habari wakielekea sehemu inayochimbwa makaa ya mawe kwenda
kujionea maendeleo ya uchimbaji wa makaa hayo katika eneo la mgodi wa
Ngaka Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma.
Malori
maalum yakibeba vifusi yakielekea kupakia vifusi vya udongo katika eneo
linaloandaliwa kuanza kuchimbwa makaa ya mawe katika eneo la mgodi wa
Ngaka Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10 Mei, 2017.
Kijiko
kikiweka kifusi cha udongo katika lori la kupakia kifusi ikiwa ni sehemu
ya maandalizi ya kuandaa eneo la uchimbaji wa makaa ya mawe katika
mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10 Mei,
2017.
Kijiko
kikiweka kifusi cha makaa ya mawe katika lori la kupakia kifusi mara
baada ya kuchimbwa katika eneo la mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka
lililopo Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10 Mei, 2017.
Mashine
ya kusaga makaa ya mawe katika eneo la mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka
Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma ikifanya kazi ya kusaga makaa ya mawe
yaliyochimbwa 10 Mei, 2017.
Mtendaji
Mkuu wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania Limited Bw. James Shedd
(kushoto) akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu masuala mbalimbali
yanayohusu makaa ya mawe katika moja ya ofisi zilizopo katika mgodi wa
makaa yam awe wa Liganga uliopo Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma 10 Mei,
2017.
KAMPUNI
ya kuzalisha makaa ya mawe nchini, Tancoal Energy Limited imetekeleza
kwa zaidi ya asilimia 100 agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ya kuongeza uzalishaji wa makaa ya
mawe maradufu.
Taarifa
hiyo iliyotolewa jana na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bw. James Shedd
wakati alipokutana na Waandishi wa habari waliotembelea mgodi huo uliopo
eneo la Ngaka katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Bw. Shedd
amesema kwamba, kampuni yake kwa sasa inazalisha kiasi kikubwa cha
makaa ya mawe kukidhi mahitaji ya soko la ndani ya tani 60,000 kwa mwezi
na ziada ya tani nyingine 20,000 ambazo pia zinauzwa katika nchi za
Uganda, Kenya na Rwanda.
“Kampuni
yetu imeongeza uzalishaji wa makaa ya mawe kwa zaidi ya asilimia 100 na
tayari magari yatumikayo katika ubebaji na uchimbaji wa makaa ya mawe
yako njiani kufika huku katika eneo la mgodi ili kuzidi kuongeza
uzalishaji na hatimaye tani za uzalishaji wa madini haya zitazidi
kuongezeka”, alisema Bw. Shedd.
Kwa
upande wake Naibu Meneja wa Mgodi wa Kampuni ya Tancoal Energy Tanzania
Bw. Edward Mwanga ameeleza kuwa, kampuni ya Tancoal kwa sasa imeongeza
magari yakiyofanya kazi toka 25 hadi 30 ambapo kwa sasa idadi hiyo
imeongezeka hadi kufikia gari 67, na sambamba na ongezeko hilo
wameongeza mizani ya kupimia magari ili pindi itokeapo ongezeko la
magari ya kubeba makaa ya mawe mzani huo utumike kuyapima.
“Kazi
yetu huku ni kupakia kutokana na oda ya wateja wetu na idadi ya gari
zilizokuja na asubuhi huwa tunapewa taarifa ya gari zilizoko njiani na
tunahakikisha kuwa ndani ya saa moja gari hizo ziwe zimepakia makaa yam
awe na kuondoka, hivyo tumeongezaidaid ya magari na pia tumeboresha
mizani na kupanua eneo”, alisema Mwanga.
Kuhusiana
na changamoto zikizoikabili kampuni hiyo amesema kuwa mwanzo wamekuwa
wakikabiliana na changamoto za ikiwemo uhaba wa vifaa, barabara, mvua
pamoja suala la uagizaji wa makaa ya mawe toka kwa wateja ambapo kwa
sasa changamoto hizo zimetatuliwa na hali ya ongezeko la uzalishaji wa
madini hayo imeongezeka.
Kwa
upande wake Meneja Udhibiti Ubora wa Makaa ya Mawe wa Kampuni ya Tancoal
Energy Tanzania Limited Bw. Bosco Mabena amesema kwamba, katika mgodi
wao kuna sehemu ya Maabara ya kisasa ambayo hutumika kuchukua sampuli za
makaa ya mawe na kuzipeleka katika hatua mbalimbali ikiwemo mkaa
ulipochimbwa, katika hatua ya processing na pia mkaa unapokwenda kwa
wateja, hivyo maabara yetu hutumika kuchukua sampuli kwa kila gari ili
kutunza rekodi.
Ameongeza
kuwa mgodi wao una udhibiti mzuri wa makaa ya mawe kwasababu ili
kuhakikisha kuwa mkaa wa mawe uko safi magari yote yanayofika katika
eneo hilo yanakaguliwa ili kuhakikisha kuwa hayana uchafu wowote na
shughuli ya ufungaji hufungwa na wataalam wao maalum ambao ufungaji wao
hauwezi kuchafua mkaa huo kwakuwa taarifa za gari ikiwemo dreva wa gari
na namba ya gari huchukuliwa ili pindi itakeapo taarifa ya uchafuzi wa
mkaa inakuwa rahisi kutambua chanzo.
Kwa
kipindi walipokuwa na mzani mmoja waliweza kupakia gari 50 kwa mzani
mmoja kwa wakati wa mchana na usiku gari 30 hadi 40 ambapo hiyo ni sawa
na wastani wa tani 2,500 kwa siku.“Kwa sasa pindi mizani ilipoongezeka
ongezeko la upakiaji naamini utaongezeka hadi kufikia gari 75 kwa
mchana, na kuanzia 40 hadi 50 kwa usiku kwakuwa bado tuna nafasi kubwa
ya kufanya hivyo na pindi magari yatakapozidi kuongezeka basi tutatumia
mizani yote miwili”, alisema Mwangosi.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilinith Mahenge ametaja
baadhi ya changamoto zilizoikabili Kampuni ya Tancoal na namna jinsi
Kampuni hiyo ilivyotekeleza agizo la Serikali ambapo amekiri kuwa kwa
sasa kampuni hiyo inafanya vizuri katika kuhakikisha kuwa madini hayo
yanazalishwa kufikia malengo yaliyoagizwa na Serikali.
“Tancoal
walikua na changamoto ikiwemo ubovu wa barabara, uhaba wa vifaa vya
uchimbaji makaa lakini kwa sasa wamejitahidi kuzitatua changamoto hizo
na mimi mwenyewe nimekwenda kukagua na kujionea baadhi ya vifaa
walivyoongeza na ninaamini zile tani elfu 60 kwa mwezi watazifikia”,
alisema Dkt. Mahenge.
Mhandisi
Migodi toka Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Nyasa,
Godfrey Wandibha anaeleza kuhusu suala la bei ya makaa yam awe na suala
la agizo la Mhe. Rais la kumpatia mmiliki wa kampuni ya Dangote eneo la
kuchimba madini hayo ambapo amesema kwamba, tayari alishapatiwa leseni
kwa ajili ya kuanza kuchimba.
“Dangote
yeye kwa sasa anatakiwa kukaa na mtu ambaye alikuwa mwenye lile eneo ili
kukubaliana baadhi ya mambo ambayo ni ya kawaida ili akishayakamilisha
aanze uchimbaji lakini suala la kupewa eneo tayari lilishakamilika kama
Rais alivyokuwa ameagiza”, alisema Wandibha.
Awali
agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alilitoa mapema Januari 6,
2017 mara baada ya kupokea taarifa na kutembelea katika mgodi wa Ngaka
ili kuona shughuli za uzalishaji katika eneo hilo.Aidha, Waziri Mkuu
aliitaka kampuni hiyo ya TANCOAL Energy kutimiza masharti ya mkataba
iliouingia na Serikali mwaka 2008.
Kampuni
ya TANCOAL iliundwa Aprili 3, 2008 na kampuni tanzu ya Atomic Resources
Limited, ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama Pacific Corporation
East Africa (PCEA) na kwa sasa inaitwa Intra Energy (T) Limited, ambayo
hisa zake ni asilimia 70 na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lenye
asilimia 30 ya hisa.
No comments:
Post a Comment