Pages

April 12, 2017

SERIKALI NA SEKTA BINAFSI KUENDELEZA USHIRIKIANO ILI KUKUZA UCHUMI


Baadhi ya viongozi mbalimbali wa Serikali wakifuatilia kwa makini maelezo ya wadau wa Sekta Binafsi wakati wa mkutano maalum wa Serikali na Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Philip Mpango akihutubia Jumuiya ya wadau wa Sekta Binafsi katika mkutano maalum wa Sekta hiyo na Serikali iliokuwa na malengo ya kuweka mazingira bora ya uhusiano na ushirikiano mwema katika kukuza uchumi wa nchi na kuiwezesha Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo 2025.

Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Philip Mpango akisisitiza jambo mbele ya wadau wa Sekta Binafsi katika mkutano maalum wa Sekta hiyo na Serikali iliokuwa na malengo ya kuweka mazingira bora ya uhusiano na ushirikiano mwema katika kukuza uchumi wa nchi na kuiwezesha Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Philip Mpango akimsikiliza mdau wa Sekta Binafsi, Bw. David Mwaibula kabla ya kupokea kitabu cha utafiti wa masuala ya Sekta hiyo, katika mkutano kati ya Serikali na Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Dkt. Reginald Mengi akizungumza na wadau kutoka Serikalini na Sekta Binafsi ambapo ameiomba Serikali iwaamini wawekezaji wazawa kwa maendeleo ya Taifa na kuongeza kuwa Taifa lolote haliwezi kujengwa na wageni.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, akifuatilia kwa makini mijadala namna ya kuboresha uhusiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi, mkutano uliofanyika ukumbi wa Serengeti, Hazina, Mjini Dodoma.

Kamishna wa Bajeti, Bi. Mary Maganga na Kamishna wa Sera Bw. Adolf Ndunguru, wote kutoka Wizara ya Fedha na mipango, wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizotolewa kuhusu umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika kukuza maendeleo ya nchi, wakati wa mkutano ulioandaliwa na Serikali ili kupata maoni ya Sekta Binafsi katika masuala mbalimbali.

Wadau kutoka Sekta Binafsi, Mohamed Bajwa (kulia) na Richard Ngalewa, wakiwa katika mkutano uliotishwa na Serikali ili kujadili namna Sekta Binafsi na Serikali vinavyoweza kushirikiana kukuza maendeleo ya nchi kupitia uwekezaji.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Kabwe Zuberi Zitto, akisikiliza kwa makini mada iliyokuwa ikitolewa kuhusu umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza uchumi nchini wakati wa mkutano kati ya Serikali na Sekta hiyo, uliofanyika Mjini Dodoma, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda akihitimisha mkutano wa Serikali na Sekta Binafsi kuhusu masuala ya uwekezaji nchini, uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-(WFM).
 
 
 

Na Benny Mwaipaja-Wizara ya Fedha na Mipango.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekutana na Taaasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) kwa lengo la kujadili namna ya kuboresha mazingira ya biashara nchini na kukuza uchumi ili kuiwezesha Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda.

Mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Philip Mpango pamoja na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji (MB), Mh. Charles Mwijage ulifanyika mkoani Dodoma katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Katika mkutano huo Serikali ilipata nafasi ya kusikiliza baadhi ya changamoto ambazo zinaikabili Sekta hiyo na kuahidi kuandaa namna bora ya kuzitatua kwa manufaa ya Taifa.Akizungumza katika mkutano huo Dkt. Mpango alisema kuwa mkutano huo umelenga zaidi katika kuboresha mahusiano na uaminifu kati ya Sekta Binafsi nchini na Serikali.

“Sekta Binafsi na Sekta za Umma inabidi zifanyekazi kwa pamoja kwa maendeleo ya Taifa, niwaombe wafanyabiashara mtoe taarifa za watumishi wa Umma wasio waadilifu ili kuondoa hali ya kutoaminiana”, alisema.Dkt. Mpango aliongeza kuwa Serikali inaahidi kutatua kero mbalimbali zinazoikabili Sekta hiyo hususani suala la utitiri wa kodi na marejesho ya kodi ili kupunguza maumivu kwa wafanyabiashara na kukuza uchumi wa nchini.

Alisema kuwa Serikali inafarijika kufanya mazungumzo na Sekta Binafsi na inatambua ushiriki wake katika maendeleo ya nchi, hivyo itajenga utaratibu wa kufanya mazungumzo ya namna hiyo angalau kila robo mwaka.Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Dkt. Reginald Mengi aliwaomba viongozi wa Serikali kuwaamini wawekezaji wazawa kwa maendeleo ya Taifa na kuongeza kuwa Taifa lolote haliwezi kujengwa na wageni.

Alisema kuwa mkutano huo uwe mwanzo mpya wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta hiyo kwani hivi karibuni kulikuwa na hali ya kutoaminiana kati yao kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wachache kukosa uaminifu.“Huu ni mwanzo mpya wa kuachana na zile habari za kutoaminiana, habari za kuona wadau wa Sekta Binafsi ni wakwepa kodi na wala rushwa, Serikali inabidi ianze kuizungumzia vizuri hii Sekta kwa maendeleo ya nchi”, alisisitiza.

Aidha, Mwenyekiti huyo alizungumzia namna ambavyo Sekta hiyo imekuwa ikiridhishwa na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano licha ya kuwapo na changamoto mbalimbali.Mkutano huo ulitoa nafasi kwa baadhi ya wajumbe ambao ni wadau wa Sekta binafsi na viongozi wa Serikali kutoa maoni yao ya namna ya kuboresha biashara na kukuza uchumi wa nchi.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango.
12/04/2017.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...