Valentine Strasser alipata kuwa Rais wa Sierra Leone. Wakati akiingia
madarakani aliweka rekodi ya kuwa kiongozi mwenye umri mdogo kuwahi
kutokea. Hata sasa, hakuna taifa ambalo limewahi kupata Mkuu wa Nchi
mwenye umri chini ya miaka 25 ili avunje rekodi ya Strasser.
Aprili 29, 1992, Strasser akiwa kijana mwanajeshi mwenye umri wa miaka
25, aliwaongoza wanajeshi wenzake kuvamia Ikulu ya Sierra Leone,
wakamteka aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Saidu Momoh,
wakamlazimisha kukimbia, naye akatorokea Conakry, Guinea.
Baada
ya Momoh kutorokea Conakry, Strasser alijitangaza kuwa Rais wa Sierra
Leone. Maisha yakabadilika, alishakuwa Mkuu wa Nchi, kwa hiyo hakutaka
kuishi kwenye nyoyo za Wasierra Leone.
Hakulipa malimbikizo ya
mishahara ya wanajeshi na watumishi wengine wa umma. Alifuja almasi ya
Sierra Leone, kwa vile jina lake ni Valentine, basi sikukuu ya
Valentine’s Day akaifanya kuwa sherehe ya kitaifa yenye mapumziko.
Strasser alikuwa na mbwembwe nyingi, mwaka 1993 katika mkutano wa Wakuu
wa Serikali katika nchi za Jumuiya ya Madola, uliofanyika Limassol,
Cyprus, alitinga kwa mbwembwe akiwa amevaa suruali ya jeans na fulana
yenye maandishi Sunny Days in Cyprus (Siku za Jua Kali Cyprus).
Alikuwa mtu wa starehe, vurugu nyingi kwa wanawake, aliua watu wasio na
hatia. Strasser alisahau kuwa ipo siku uongozi hautakuwa kwenye mikono
yake, na ambacho kinaweza kumfaa ni kuishi ndani ya mioyo ya watu ili
wamtetee na kumpigania baadaye.
Januari 16, 1996, Strasser
alipinduliwa na msaidizi wake, Brigedia Jenerali Julius Maada Bio.
Strasser akakimbilia Uingereza, akajiunga na Chuo Kikuu cha Warwick,
kilichopo mjini Coventry, akaanza masomo ya sheria, akasema anataka awe
wakili ili awatetee Waafrika.
Mwaka mmoja wa masomo, Strasser
aliishiwa fedha, akaacha chuo. Maisha Uingereza yakawa magumu,
akakimbilia Gambia nako kukawa pagumu, mwisho akarudi Sierra Leone,
mjini Grafton, Mashariki ya Mji Mkuu wa nchi hiyo, Freetown.
Kazi
ya kwanza ambayo Strasser aliifanya ikawa kuanzisha kichuo kidogo cha
kufundisha kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Maisha ya chuo yakamshinda.
Baada ya kila kitu kwenda kombo,
Strasser alirudi nyumbani kwa mama yake mzazi na kuishi kwenye banda la
uani. Hata sasa, akiwa na umri wa miaka 49, anakunywa pombe za kienyeji
mtaani. Hana hadhi yoyote kama kiongozi mkuu wa nchi mstaafu.
Strasser anaishi kama mtu tu mtaani. Mlevi na hakuna anayemjali. Hana
mtu wa kumtetea wala kumpigania kwa sababu hakuishi kwenye nyoyo za
watu. Strasser ndiye Mkuu wa Nchi wa zamani, anayeishi kimaskini kuliko
wote duniani.
Ukiwa kiongozi na kugeuka kituko kama Strasser
inawezekana kabisa. Ishi vibaya na watu wasikupende, akija mtawala
ambaye hatakutambua kama mkuu uliyepita, unaweza kuishi maisha ya hovyo
kama ombaomba mtaani au mnywa gongo uliyeshindikana.
Jifunze sasa
kwamba ukiishi vizuri kama kiongozi, hata baada ya kutoka au kutolewa,
jamii itakuenzi, itakupenda, kukupigania na kukutetea ukiwa nje ya
ulingo na hutaishi vibaya. Ukiishi vibaya, utakuwa na mwisho mbaya kama
Strasser.
|
No comments:
Post a Comment