Pages

February 8, 2017

BODI YA STAMICO YAJIPANGA KUFUFUA MGODI WA MAKAA YA MAWE KIWIRA COAL MINE


BODI ya Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) limesema limejipanga kuhakikisha linafufua shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa Kiwira coal mine uliosimama kwa zaidi ya miaka nane.
Hayo yalibanishwa katika Ziara ya Wajumbe wa Bodi ya STAMICO katika migodi ya Kabulo na Kiwira iliyoko Wilaya ya Ileje mkoani Songwe iliyofanyika juzi kwa lengo la kujionea hali ilivyo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Alexander Muganda alisema bodi iliundwa Julai mwaka jana na imefanya zioara ya kutembelea miradi yote iliyochini ya Stamico ili kuona namna ya kuiendesha kwa manufaa.
Alisema kuhusu Mgodi wa Kiwira na Kabulo, Bodi imeona jinsi itakavyoweza kuishauri Menejimenti ili iweze kuanza kuchimba makaa yam awe kwa ajili ya kuuza na mpango wa baadaye uwe kuzalisha umeme.
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Stamico, Mhandisi Said Mkwawa alisema bodi imeona mradi ulivyo na jinsi ya kufanya uwekezaji ili shirika liweze kujiendesha kwa tija.
Alisema bodi imegundua kuwa makaa ya mawe katika mgodi wa Kiwira na Kabulo unapatikana juu juu hivyo shirika haliwezi kutumia gharama kubwa ya kuanza uchimbaji na kwamba hadi sasa kuna hazina ya tani milioni 40 hadi 50.
Mjumbe wa Bodi, John Seka alisema nia ya bodi ni kulisaidia shiriuka la Stamico kujiendesha kibiashara kutokana na rasilimali zilizopo na teknolojia zitakazotumika kuwa rahisi.
Awali akisoma taarifa ya Mgodi kwa wajumbe wa Bodi, Kaimu Meneja mkuu wa Mgodi wa Kiwira , Mhandisi Aswile Mapamba alisema katika vipindi tofauti shirika liliunda timu za wataalam ili kufanya tathmini mbali mbali juu ya kufufua mgodi.
Alisema timu hiyo iliona uwezekano wa awali mgodi unaweza kuanza uzalishaji katika kiwango cha awali cha tani 150,000 kwa mwaka kwa makaa ghafi na megawati 6 za umeme.
Alisema timu hizo zilimaliza kufanya tathmini Novemba 2016 na iliangalia hali halisi ya uchakavu wa mitambo muhimu mgodini, kituo cha umeme, kinu cha kusafishia makaa , magari  na makazi.
Aidha Mhandisi Mapamba alitoa wito kwa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika kusaidia kuhakikisha shughuli za upatikanaji wa mtaji na ufufuaji wa mgodi unafanyika katika muda muafaka.
Awali Katibu tawala wa Wilaya ya Ileje, Mary Marco alisema mgodi ulisimama tangu 2008 licha ya kuwa na miundombinu yote inayotakiwa kuendesha mgodi lakini vifaa na mitambo inaharibika kutokana na kutotumika.
Alisema mgodi upo katika Mkoa mpya wa Songwe ambao unategemea rasilimali walizonazo ili kuweza kujijenga hivyo mgodi wa Kiwira ni moja ya mategemeo hivyo kutofanya kazi kunarudisha maendeleo ya Wilaya na Mkoa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa kufunguliwa na kufufuliwa kwa mgodi huo kutasaidia kuongeza ajira kwa wakazi wa Mkoa wa Songwe na Mbeya ikiwa nni pamoja na kuinua uchumi wa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Alisema hivi sasa Serikali inapata hasara ya kuwalipa baadhi ya wafanyakazi ambao wanafanya kazi ya kulinda mitambo ambayo haifanyi kazi jambo ambalo pia linahatarisha hali ya usalama wa mitambo kutokana na uwezekano wa kuanza kuibiwa vifaa.




Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Luten Mstaafu Chiku Galawa akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Madini Tanzania (STAMICO) Balozi Alexandekwake kabla ya kufanya ziara katika migodi ya makaa ya mawe ya Kiwira na Kabulo.


Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Balozi Alexander Muganda akitoa taarifa kwa Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya kuhusu Ziara ya Bodi kutembelea migodi ya Kabulo na Kiwira coal mine


Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Kiwira, Mhandisi Aswile Mapamba akitoa maelezo kwa wajumbe wa bodi ya Stamico kuhusu mgodi wa Kabulo uliopo Ileje mkoani Songwe.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...