Pages

January 7, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ATEMBELEA MGODI WA MAKAA YA MAWE YA NGAKA WILAYA YA MBINGA MKONI RUVUMA



*Aahidi kutuma Gavana, CAG, Msajili wa Hazina kufanya ukaguzi
*Asema Serikali haitaruhusu uagizaji wa makaa hayo kutoka nje ya nchi
*Autaka uongozi wa kampuni uimarishe teknolojia ili kuongeza uzalushaji

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa atamtuma mara moja Msajili wa Hazina aende kufanya uchunguzi wa kina na wa kijinai (forensic investigation) ili kijiridhisha kama mapato na matumizi ya kampuni ya TANCOAL ni halali.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Januari 6, 2017) mara baada baada ya kupokea taarfa na kutembelea mgodi huo ili kuona shughuli za uzalishaji zikoje.

Waziri Mkuu amesema atamwagiza pia mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili apitie mahesabu ya kampuni tangu mwaka 2011 walipoanza uzalishaji. “Mbali CAG, itabidi Gavana wa Benki Kuu naye aangalie utumaji wa fedha uliokuwa ukifanywa kama ulifanyika kwa halali,” amesema.

Katika maswali aliyoyauliza Waziri Mkuu, alitaka kujua ni kwa nini kampuni hiyo haijalipa gawio kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambao ni mbia (asilimia 30) na kampuni ya Intra Energy Limited (asilimia 70) licha ya kuwa imekuwa ikifanya uzalishaji wa makaa ya mawe na kuyasafirisha kwenye viwanda hapa nchini na nje ya nchi.
“Taarifa zenu zinaonyesha kuwa mmepata kila mwaka lakini rekodi nilizonazo zinanionyesha kuwa mwaka 2013 mlipanga kuzalisha tani 50,000 na mkauza zaidi ya hapo. Mkagzi wa hesabu anasema kampuni imepata, hii itawezekanaje?” alisema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Bw. Mlingi Mkucha.
“Desemba 2013 mliuza tani 39,000 kwa wamiliki wa viwanda vya nguo, pia mliuza tani 2,000 kwa kampuni ya saruji ya Zambia, Novemba 2013 mliingia makubaliano ya kuuza tani 165,000 kwa kampuni ya saruji ya Kitanzania na ziliuzwa. Mbona financial statement zenu zinasema mwaka huo nao mlipata hasara?”
“Mnasema gawio (dividend) hutolewa baada ya mtu kutangaza faida. Mbona mlivuka lengo lakini mkatangaza kuwa kamouni imepata hasara katika mwaka huo wa fedha?”
Waziri Mkuu alimbana Bw. Mkucha aeleze ni kwa nini akiwa mwanasheria wa NDC aliruhusu kuwepo kwa mkataba unaotoa mwanya kwa kampuni ya TANCOAL kulipia gharama za menejimenti kwa wakurugenzi ambao wako Australia wakati hawahusiki na utendaji wa kila siku wa TANCOAL hapa nchini.
Pia alihoji ni kwa nini aliyekuwa Mkurugenzi wa NDC, Bw. Gideon Nassari alikuwa ni mjumbe wa Bodi ya TANCOAL na mjumbe wa Bodi ya Intra Energy Corporation ya Australia huku akiwa ni Mtendaji Mkuu wa NDC. “Wewe ulikuwa mwanasheria wa NDC na ulilijua hilo lakini hukuona taabu ya kiutendaji katika hilo? Au ulishindwa kusema kwa sababu alikuwa ni bosi wako?”
Waziri Mkuu amemtaka Bw. Mkucha aupeleke mikataba huo kwa MwanasheriA Mkuu wa Serikali ili aupitie upya na hasa kipendgele cha kufungua akaunti za NDC kwa kutumia kanuni za Australia na suala la utaratibu wa gawio kwa wanahisa ambapo kifungu kilichopo kinaipa Bodi ya TANCOAL mamlaka ya kuamua kutoa au kutokutoa kwa wanahisa.

“Kipengele kama hiki kwenye mikataba kinazuia ninyi kupata gawio, na ndiyo maana hesabu zao kila mwaka zimekuwa zinasoma hasara na ninyi mnaona sawa tu huku Serikali ikiendelea kukosa mapato yake,” amesema.

Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa kampuni ya TANCOAL uongeze uzalishaji ili iweze kukidhi mahitaji ya ndani kwani makampuni mengi yamebaini gharama kubwa iliyopo kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na sasa yanahitaji makaa ya mawe kwa uzalishaji.
“Nimetembelea mgodi na kujiridhisha kuwa makaa ya mawe yapo ya kutosha. Uongozi wa kampuni mmesema mashine ziko bandarini Mtwara, lipieni mkamilishe taratibu ili mashine na mitambo yenu vije kusaidia kuongeza uzalishaji,” amesema.
“Nirudie wito wa Serikali kuwa hatutaruhusu uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje ya nchi na kwa maana nyingine tumewaongezea wigo wa soko lakini ninyi mnakosa teknolojia ya uchimbaji makaa kwa wingi. Fanyeni haraka kuleta hivyo vifaa vilivyoko bandarini,” alisisitiza.
Akiwa kwenye mgodi huo, Waziri Mkuu alielezwa kuwa kampuni hiyo imepanga kuongeza uzalishaji na kufikia tani 60,000 kutoka tani 2,500 za sasa. Hivi sasa, uchimbaji kwenye mgodi wa Ngaka unafanyika kwenye eneo la Mbalawala na Mbuyura ambayo yana mashapo (deposits) ya tani milioni 423.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, JANUARI 6, 2017.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Tancoul Bwana Mark McAnderew  wakati alipotembelea mgodi wa makaa ya mawe ya Ngaka unaomilikiwa na kampuni ya Tancoul uliopo wilayani Mbinga  kushoto kwa waziri mkuu ni Mwenyekiti wa bodi ya NDC Dr Samuel Nyantahe
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Mlingi Mkucha wakati alipotembelea mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka unaomilikiwa na kampuni ya Tancoul uliopo wilayani Mbinga  kushoto kwa waziri mkuu ni Mwenyekiti wa bodi ya NDC Dr Samuel Nyantahe
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Ofisa Rasilimali watu wa kampuni ya Tancoul Ms  Pendo Mweli wakati alipotembelea mgodi wa makaa ya mawe unaomilikiwa na kampuni ya Tancoul uliopo Ngaka wilayani Mbinga  Mkoani Ruvuma
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe unavyofanywa nakampuni ya Tancoul katika mgodi wa Ngaka uliopo wilayani Mbinga  kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la maendeleo la taifa NDC Dr Samuel Nyantahe.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia mkaa wa mawe ulivyo
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ameongozana na mkuu wa mkoa wa Ruvama Mhandisi Mahenge pamoja naviongozi mbalimbali walipokuwa wanatemmbelea mgodi wa Ngaka

Picha na Chris Mfinanga

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...