WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo kuhakikisha eneo la Kisarawe II linakuwa na umeme wa
uhakika ili kuwezesha viwanda na wananchi wa eneo hilo kupata nishati
hiyo.
Alitoa
agizo hilo jana jioni (Jumanne, Januari 3, 2017) wakati alipotembelea
kiwanda cha Milkcom kinachozalisha bidhaa za maziwa na kiwanda cha
Watercom kinachozalisha maji vilivyoko katika kata ya Kisarawe ii
wilayani Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.
“Waziri
wa Nishati ahakikishe eneo hili linapata umeme wa uhakika ili
kuviwezesha viwanda hivi kufanyakazi vizuri jambo litakaloongeza
uzalishaji. Pia wananchi wanaoishi katika maeneo haya nao watanufaika na
upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema amefarijika na jitihada za muwekezaji huyo za kuungamkono
mkakati wa Serikali ya awamu ya Tano wa kuifanya Tanzania kujenga uchumi
wa viwanda utakaoliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kipato cha kati
ifikapo mwaka 2025.
Awali,
Msemaji wa Viwanda hivyo, Aboubakar Faraj akisoma taarifa ya viwanda
hivyo kwa Waziri Mkuu alisema moja ya changamoto zinazowakabili ni
pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika jambo linasababisha kupanda
kwa gharama za uzalishaji.
“Punde
umeme unapokatika tunalazimika kutumia majenereta kwa muda mrefu. Hii
husababisha ongezeko la gharama za uzalishaji ambazo huumiza kiwanda kwa
sababu haiwezekani kumtwisha mzigo huu mlaji,” alisema.
Faraji
alisema changamoto nyingine ni miundombinu ya barabara ambayo
usababisha wateja wengi kushindwa kufika kwenye viwanda hivyo kwa
urahisi, hivyo aliiomba Serikali kuwatatulia kero hilo.
Aliongeza
kuwa kwa sasa viwanda hivyo vimeajiri watu zaidi ya 1,800, ambapo
alisema endapo Serikali itawahakikishia upatikanaji wa umeme na barabara
wataongeza ajira kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2018.
Mapema Waziri
Mkuu alizindua wodi ya wazazi katika Zahanati ya Kisarawe ii
iliyojengwa kwa ufadhili wa kampuni ya mafuta ya Oilcom. Wodi hiyo yenye
vyumba vitatu itawapunguzia akinamama kusafiri umbali mrefu kutuata
huduma hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
No comments:
Post a Comment