WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka huu wa fedha Serikali
imetenga sh. bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete
yenye urefu wa kilomita 109.4 kwa kiwango cha lami.
Ametoa
kauli hiyo jana (Ijumaa, Januari 20, 2017) wakati akizungumza na
viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete alipowasili katika kata ya
Mtamba wilayani hapa akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.
Waziri
Mkuu amesema usanifu wa kina wa barabara ya Njombe-Makete kwa ujenzi wa
kiwango cha lami umekamilika hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na
subira.
Amesema
barabara nyingine inayotarajiwa kujengwa ni ya kutoka Makete hadi Mbeya
kupitia Isyonji yenye urefu wa kilomita 96 ambayo imetengewa sh.
milioni 50 kwa ajili ya kufanyiwa usanifu.
Waziri
Mkuu amesema wananchi waendelee kushirikiana na Serikali kwani
imedhamiria kuwatumikia kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili
katika maeneo yao.
Aidha,
Waziri Mkuu amewataka wahandisi wa wilaya hiyo kuhakikisha
wanawasimamia vizuri wakandarasi wanaojenga miradi mbalimbali katika
halmashauri zao kuhakikisha kama viwango vinalingana na thamani halisi
ya fedha zinazotolewa.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa Idara katika halmashauri
kupambana na vitendo vya rushwa na wahakikishe watumishi hawatowi
huduma kwa kuomba rushwa.
“Kwanza
watumishi watambue kwamba rushwa ni dhambi. Pia kiutumishi ni makosa
makubwa hivyo wajiepushe na vitemdo hivyo,” amesema.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Makete Bi. Veronica Kessy amesema kujengwa
kwa barabara hizo kwa kiwango cha lami kutaimarisha ukuaji wa uchumi wa
wilaya hiyo na Mkoa wa Njombe kiujumla hivyo wananchi kupata tija.
“Mfano
barabara ya kutoka Makete hadi Mbeya kupitia Bulongwa, Iniho, Kikondo
na Isyonje itasaidia wilaya kufunguka hivyo kurahisisha usafirishaji wa
mazao ya misitu kama mbao,” amesema.
Hata
hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema barabara hii pia itaunganisha Wilaya
hiyo na kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Songwe hivyo watapata fursa
ya kuanzisha kilimo cha maua. Awali walishindwa kulima maua kwa sababu
hakukuwa na usafiri wa uhakika.
Awali
Waziri Mkuu alitembelea shamba la mifugo la Kitulo linalomilikiwa na
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lenye jumla ya Ng’ombe 750 wakiwemo
ndama 61, majike 212, mitamba 273, madume 21, na madume wadogo 183.
Shamba hilo linazalisha wastani wa lita 450,000 za maziwa kwa mwaka kutokana na ng’ombe 123 wanaokamuliwa.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa sh. bilioni 1.4 kati ya
sh. bilioni 1.8 zilizotengwa katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya
uendelezwaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Amesema
ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ya mwaka 2015/2020 ya kuwa na zahanati katika kila kijiji, kituo
cha afya katika kila kata, hospitali katika wilaya na hospitali za rufaa
kwa kila mkoa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Januari 21, 2017) wakati
alipotembelea eneo la mtaa wa Wikichi inapojengwa hospitali hiyo akiwa
katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.
Amesema
lengo la ujenzi wa hospitali hiyo ni kuhakikisha mwananchi anaanza
kupata huduma za afya katika eneo lake na anapokuwa na tatizo kubwa
ndipo atakwenda hospitali ya wilaya na kisha hospitali ya rufaa ya mkoa.
“Hospitali
hii ikikamilika itawapunguzia wananchi gharama za kusafiri umbali mrefu
kwa ajili ya kufuata huduma za rufaa. Sasa hakutakuwa na sababu ya
kwenda Iringa, Mbeya wala Ruvuma huduma zote zitakuwa zinapatikana hapa
hapa Njombe,” amesema.
Amesema
ujenzi huo utakapokamilika Serikali itapeleka fedha za ununuzi wa dawa
na vifaa tiba. “Hatuwezi kukosa fedha za kununulia vifaa tiba na dawa
kwani ni moja ya majukumu yetu,”.
“Mheshimiwa
Rais Dkt. John Magufuli ameahidi kuwahudumia na kuwatumikia wananchi
wote bila ya kujali uwezo wao, itikadi zao za kidini na kisiasa na hapa
ndiyo maana ya ahadi hiyo ya Serikali ya kuwahudumia. Watu wote watakuja
kutibiwa hapa,” amesema.
Akitoa
taarifa ya ujenzi mradi wa hospitali hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa
Njombe, Bw Jackson Saitabau amesema kukamilika kwa ujenzi wa hospitali
hiyo kutawapunguzia wananchi gharama kubwa za kufuata huduma za rufaa
katika mikoa ya jirani.
Amesema
ujenzi wa hospitali hiyo ulianza katika eneo hilo lenye ukubwa wa
takribani ekari 70 katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, ambapo kiasi cha
sh. 953.705 zilitengwa kati yake sh. milioni 236.575 zilitumika kwa
ajili ya ulipaji wa fidia.
“Hospitali
hii inajengwa kwa awamu na tulianza na jengo la wagonjwa wa nje (OPD)
ambapo gharama za mradi ni sh. bilioni 3.2 huku gharama za mtaalamu
mshauri ni sh. milioni 114.160. Mradi ulianza Julai 23, 2016 na
unatarajiwa kukamilika Januari 26, 2018,” amesema.
Amesema
kuwa hadi sasa kazi ya ujenzi huo imekamilika kwa asilimia 40 na
mkandarasi ameshalipwa sh. milioni 892.963 sawa na asilimia 28 ya
gharama za mradi na mtaalam mshauri amelipwa sh. milioni 51.50.
Naye
Mbunge wa Jimbo la Njombe, Mheshimiwa Edward Mwalongo ameishukuru
Serikali kwa kuwawezesha kupata hospitali ya Rufaa ya mkoa huo na
amewaomba wananchi waendelee kuiunga mkono Serikali na washiriki
kikamilifu katika kuilinda miundombinu hiyo.
Pia
Waziri Mkuu amezindua Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe
iliyojengwa katika Kata ya Igwachanya pamoja na kupokea taarifa ya
ujenzi wa Ofisi hiyo pamoja na kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi
wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe.
Aidha,
Waziri Mkuu amewataka watumishi wa halmashauri hiyo ambao wananshi nje
ya eneo wilaya hiyo wawe wamehamia ifikapo Februari 15 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment