Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tarehe 26 Januari, 2016. Katika kikao hicho Bi. Mindi alizungumza kuhusu tuzo za ubunifu zilizotolewa na Umoja wa Afrika (AU) kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mamlaka ya Mapato Tanzania ambazo zilikuwa miongoni mwa taasisi zilizoshindanishwa na kuibuka washindi.Pia alitumia fursa hiyo kuwaarifu waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika unaoendelea nchini Ethiopia-Addis Ababa na Mkutano wa Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Februari, 2017.
Kutoka kushoto ni Bw. Felix Tinkasimile Meneja wa Mradi wa Mfumo wa Forodha wa TANCIS, kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA, Bi. Sarah Kibonde kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Bw. David Nghambi kutoka Mamlaka hiyo
Bi. Sarah akizungumza kuhusiana na tuzo iliyotolewa kwa SSRA ambapo alieleza wameshinda Tuzo hiyo katika kipengele cha utunzaji data ambapo wamekuwa wakishirikiana na taasisi za Serikari zinashughulika na umma katika masuala mbalimbali kama Mamlaka ya Vitambulika, Mamlaka ya Mapato na RITA.
Bw. Richard Kayombo akizungumzia tuzo hizo ambapo aliishukuru Wizara ya Mambo ya Nje kwa uratibu na kutambua umuhimu wa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato kwa umma katika kuboresha utendaji na kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Bi Mindi akimkabidhi Bi. Sarah kombe la ushindi kwa niaba ya Wizara. Bi. Kibonde aliipokea zawadi hiyo kwa niaba ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Meneja wa Mradi wa Mfumo wa Forodha wa TANCIS kutoka TRA akipokea zawadi ya cheti cha ushindi kutoka kwa Bi. Mindi Kasiga.
Picha ya pamoja ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje, TRA na SSRA.
Taarifa
kuhusu Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na
Malawi, Tuzo za AU kwa SSRA na TRA na Mkutano wa AU-Addis Ababa
Mkutano
wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya
Tanzania na Malawi umepangwa kufanyika mjini Lilongwe, Malawi tarehe 03
hadi 05 Febuari 2017. Mkutano huo utawakutanisha viongozi na wataalamu
wa sekta mbalimbali kutoka Tanzania na Malawi.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt.
Augustine P. Mahiga (Mb), anategemewa kuongoza ujumbe wa Tanzania
katika mkutano huo. Aidha, Uongozi wa Mkoa wa Mbeya ambao umekuwa
ukishiriki katika vikao vya maandalizi, unategemewa kushiriki katika
mkutano huo.
Lengo
la mkutano huu ni kujadili na kutathmini hatua zilizofikiwa katika
utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Tatu wa JPCC
uliofanyika Tanzania, tarehe 24 hadi 30 Juni, 2003.
Miongoni
mwa mafanikio yaliyofikiwa kwenye utekelezaji wa makubaliano ya
mikutano iliyopita kwa upande wa Tanzania ni pamoja na; Kuanzishwa kwa
mradi wa Kituo cha Huduma za Pamoja Mipakani (One Stop Border Post –
OSBP) katika mpaka wa Kasumulu/Songwe ambao umefikia katika hatua
nzuri; Idara za Uhamiaji, Polisi na Forodha za nchi zetu mbili
zinaendelea kushirikiana katika kutoa huduma na kudhibiti abiria na
mizigo katika maeneo ya mpakani.
Pia,
Mamlaka ya Bandari Tanzania imeruhusu Mamlaka za Malawi kuwa na maeneo
yao katika bandari zetu, kwa ajili ya kuhifadhia mizigo na bidhaa
nyingine zinazopitia nchini kabla ya kwenda Malawi.
Aidha,
mkutano huo utatoa fursa kwa nchi zetu mbili kujadiliana na kukubaliana
kuhusu maeneo mapya ya ushirikiano. Miongoni mwa maeneo hayo (kwa
upande wa Tanzania) ni pamoja na: Kuanzisha ushirikiano katika sekta ya
usafiri wa majini, ambapo mbali na faida za kiuchumi, safari hizo
zitaimarisha mwingiliano wa watu na kupunguza tofauti zilizopo. Kwa
hivi sasa Serikali inajenga meli tatu, mbili kwa ajili ya kusafirisha
mizigo na moja kwa ajili ya abiria.
Maeneo
mengine ni kuanzisha Mkataba wa ushirikiano katika Sekta ya Usafiri wa
Anga (BASA); Kuanzisha mfumo wa kurahisisha ufanyaji biashara kwa ajili
ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo hasa katika maeneo ya mpakani;
Kuanzisha ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira na masuala ya afya
ikiwemo magonjwa ya mlipuko hususan maeneo ya mipakani; na Kuanzisha
ushirikiano katika sekta ya elimu ya vyuo vikuu na vyuo vingine vya
amali.
Tangu
kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya
Tanzania na Malawi nchi hizi mbili zimeshafanya vikao vinne vya Tume
hiyo. Kikao cha mwisho kilifanyika hapa Dar es Salaam, Tanzania tarehe
24 hadi 30 Juni, 2003 na kuhudhuriwa na viongozi na wataalam wa sekta
mbalimbali kutoka nchi zetu mbili.
Wakati
huohuo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga kwa niaba ya
Wizara amekabidhi tuzo kwa wawakilishi wa taasisi za Mamlaka ya
Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Bi. Sarah Kibonde na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo baada ya kuibuka
washindi wa Tuzo zilizotolewa na Umoja wa Afrika (AU).
Akipokea
kombe baada ya kuibuka mshindi kwenye kipengele B kuhusu “Innovative
Partnership in Service Delivery for its National Social Security
Collaborative Database Bridging Project" Bi. Kibonde alisema kuwa
ushindi huo ni chachu ya taasisi yao kufanya vizuri zaidi katika kutoa
huduma bora kwa wananchi wote kwa ujumla.
Naye
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Bw. Kayombo ambaye taasisi
yake imefanikiwa kushika nafasi ya pili kipengele C kuhusu "Tanzania
customs Integrated System" ameushukuru Umoja wa Afrika kwa kuandaa
mashindano hayo ambayo ni muhimu katika kujenga uwazi kwenye eneo la
ulipaji kodi.
Pia
ameushukuru Ubalozi wa Tanzania kwa kupokea Tuzo hizo kwa niaba yao na
kuishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki kwa
kukabidhi ushindi huo kwao.
Katika
hatua nyingine, Bi. Kasiga alizungumzia juu ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi
wa Umoja wa Afrika (AU Summit) unaotarajiwa kufanyika Jijini Addis
Ababa, Ethiopia tarehe 30 na 31 Januari, 2017. Mkutano huo umetanguliwa
na kikao cha Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu na Maafisa Waandamizi
kilichofanyika tarehe 22 hadi 24 Januari, 2017 na kufuatiwa na kikao cha
Baraza la Mawaziri kilichoanza tarehe 25 hadi 27 Januari, 2017.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 26 Januari, 2017
No comments:
Post a Comment