Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
akisalimiana na Naibu Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Mhe.
Lulu Msham Abdalla wakati alipofika kutembelea Kiwanada cha Matrekta
huko Mbweni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja leo,(katikati) Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Mhe. Hamad Rashid Mohamed.
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukiendeleza
Kiwanda cha Matrekta Mbweni, kwa lengo la kuimarisha sekta ya kilimo pamoja na
sekta nyengine za ufundi hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho akiwa amefuata
na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi pamoja na watendaji wakuu wa Serikali
wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Abdulhamid Yahaya Mzee.
Katika maelezo yake
Dk. Shein alisema kuwa ziara hiyo aliyoifanya akiwa na viongozi wengine wa
Baraza la Mapinduzi na Watendaji Wakuu wa Serikali ni ushauri wake wa kuwataka
viongozi hao washiriki pamoja ili wapate kujua muelekeo, hatma, nyenzo,
wafanyakazi, mambo yanayohitajika pamoja na changamoto zilizopo.
Akiwa katika ziara
yake ya mwanzo ya kikazi tokea kuingia mwaka mpya wa 2017, Dk. Shein alisema
kuwa tokea kuanzishwa Kiwanda hicho mnamo mwaka 1966 haikupiga hatua kubwa
licha ya juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali kwa mashirikiano ya Serikali
ya China na baadae mnamo mwaka 1980 Serikali ya Uholanzi kuziunga mkono ikiwemo
kukijengea uwezo wa kiufundi na kiutawala.
Dk. Shein alisema kazi
ya kikiendeleza Kiwanda hicho si ndogo lakini akimnukuu shujaa wa Ufaransa Napoleon Bonaparte,
aliekuwa kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya mwaka
1799 alivyosema kuwa “Tulikwenda, Tukaona na Tukashinda”, basi anaamini mafanikio yatapatikana baada ya
ziara hiyo.
“Tumekuja, tumeona na
tutashinda lakini kubwa ni mashirikiano ya pamoja kati ya Serikali na wafanyakazi
wa Kiwanda hichi...tujiandae kubwa lijalo”,alisema Dk. Shein.
Hivyo, Dk. Shein
alisisitiza kuwa kazi ya kukiendeleza Kiwanda hicho ni ya Serikali peke yake
bali inahitaji mashirikiano makubwa kutoka kwa wafanyakazi wa Karakana hiyo
kwani hilo linatasidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lilolokusudiwa.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa Serikali inaweza kufanya wajibu wake katika kuhakikisha Kiwanda hiyo
inarudi katika uhalisia wake lakini bila ya mashirikiano ya wafanyakazi wa
karakana hiyo lengo halitofikiwa.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa yeye na ujembe aliofuatana nao wameona waliyoyaona katika kiwanda
hicyo zikiwemo changamoto zilizopo pamoja na zile za wafanyakazi wake na
serikali itafanya juhudi ya kuangalia nini kitafanyika na baadae taarifa rasmi itatolewa.
Hata hiyo, Dk. Shein
alisisitiza haja ya kutofanya kazi kwa mazoea kwa kuutaka uongozi na wafanyakazi
wa Kiwanda hicho kuyaweka vizuri mazingira ya Kiwanda hicho pamoja na kuviweka vifaa vichakavu katika
utaratibu maalum ambapo licha ya changamoto zilizopo lakini Kiwanda hicho kinaweza
kuvutia iwapo hatua hizo zitachukuliwa.
Nae Waziri wa Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohammed alitoa shukurani za pekee kwa
Rais Dk. Shein kwa ziara yake hiyo ya mara ya pili katika Kiwanda hicho na
kueleza jinsi Dk. Shein anavyofanya maamuzi yake kwa mashirikiano kati yake na
wasaidizi wake na hakurupuki katika hilo.
Waziri Mohammed
alisema kuwa juhudi za makususdi zimekuwa zikichukuliwa na Wizara yake katika
kuhakikisha wakulima wanatatuliwa changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na
kuwalimia mashamba yao kwa kutumia matrekta ambapo katika msimu huu tayari
asilimi 87 ya mabonde yameshalimwa licha ya uhaba wa vitendea kazi huku
akieleza changamoto ya Taasisi kama hiyo kuwa Kitengo.
Nao wafanyakazi wa Kiwanda
hicho katika risala yao iliyosomwa na Mkuu wa Kitengo cha zana za Kilimo,
Mohammed Omar Mohammed walisema kuwa wanajivunia ujio wa Rais kwa mara ya pili
katika kipindi cha takriban miaka mitatu kwa lengo la kujali kazi ambazo Karakana
hiyo inazitekeleza.
Mkuu huyo wa kitengo
alieleza historia ya Karakana hiyo, hali
halisi ya sasa , majukumu yake ya
kuratibu kazi zote zinazohusiana na zana za kilimo huku wakieleza kuwa kiwanda
hicho kinatoa huduma za kiufundi kwa zana zote za kilimo za Serikali na za
wateja binafsi pamoja na huduma za ufundi ambazo haziusiani na zana za kilimo
kwa taasisi za Serikali.
Wakieleza miongoni mwa
majukumu ya Kiwanda hicho ni pamoja na kuendesha mafunzo ya amali ya kiufundi
ya nadharia na vitendo kwa vijana ambao wanapenda kupata ujuzi wa kiufundi hasa
kwenye fani za umeme na umakanika kwa muda wa miaka miwili.
Sambamba na hayo,
wafanyakazi hao walieleza changamoto mbali mbali zinazowakabili Kiwandani hapo ambapo mapema Dk. Shein
aliitembelea Kiwanda hicho na kupata maelezo kutoka kwa Wakuu wa Vitengo ambao walieleza changamoto
zilizopo ambapo nayeye alitumia fursa hiyo kuuliza masuala kadhaa.
Mnamo mwaka 1966, Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipata msaada wa matrekta 50 kutoka Jamhuri ya Watu wa
China pamoja na majembe yake ya kuchimba na kuburuga kwa lengo la kuwapunguzia
mzigo wakulima ambao walikuwa wakilima kwa kutumia jembe la mkono.
No comments:
Post a Comment