Wananchi Wa
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni wamehamasishwa kujiunga na mfuko wa afya ya
jamii CHF ili kupunguza gharama za matibabu na kuwa na uhakika wa kupata
matibabu wakati wote pindi huduma ya Afya inapohitajika.
Hayo
yalisemwa na Afisa Tawala Wilaya Bi. Upendo Magashi alipokuwa kwenye
kampeni ya uhamasishaji wa wananchi kujiunga na kuwa wanachama wa
mfuko wa afya
ya jamii wa hiari CHF ili kupunguza
gharama za matibabu, uliobeba kauli mbiu ya KUKU MMOJA MATIBABU MWAKA
MZIMA.
Aliwaeleza
wananchi kuwa, kuku mmoja anayegharimu shilingi 10000, anaweza kusaidia kaya
moja yenye watu sita kujiunga na mfuko wa Afya ya jamii CHF, ambao watapata matibabu
bure kwenye vituo vya Afya kwa ngazi ya Wilaya mwaka mzima. Aliwataka waratibu
wa mfuko wa Afya CHF, Wataalamu wa afya, na viongozi mbalimbali kuendelea kutoa
elimu na kuwahamasisha wananchi ili kuweza kuwasaidia juu ya umuhimu wa mfuko huo
ikiwa ni pamoja na kujibu hoja zao kwa
kuzitafutia ufumbuzi.
Mganga Mkuu
wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni
Bw.Credianus Mgimba aliwaeleza wananchi kuwa faida mojawapo kubwa ya kujiunga
na mfuko wa CHF ni kusaidia upatikanaji wa dawa za kutosha kwenye vituo vya huduma za afya. Wanachama wakiwa wengi
itasaidia uwepo wa dawa za kutosha kwani fedha itakayokusanywa itakuwa nyingi
itakayosaidia upatikanaji wa dawa mbalimbali na wanachama wakiwa wachache tatizo la
upungufu wa dawa halitakwisha.
Aidha wananchi walielezwa kuwa kuwa kuna thamani
kubwa sana wakiwa wanachama wa mfuko wa afya ya jamii hasa kwa kaya zisizojiweza kwani husaidia
katika kipindi kigumu iwapo mgonjwa atakosa fedha za matibabu. kwa kutumia kadi
ya CHF ataweza kupata matibabu tofauti
na kutokuwa mwanachama hali ambayo wakati mwingine hupelekekea hata mtu
kupoteza uhai kwani wananchi wengi hawana
uwezo wa kujigharamia matibabu. Lengo ni kuhakikisha kila mwananchi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni anakuwa
na uhakika wa huduma ya afya.
Wananchi walisisitizwa pia kuwahudumia wazee
kwani kumekuwa na changamoto za huduma ya Afya kwa wazee hasa linapokuja suala
zima la matibabu. Wameelezwa kuwa ili
wazee waweze kuhudumiwa kila kijiji kinapaswa kuchangia laki mbili (200,000)
ili iweze kusaidia dhana ya huduma bure ya afya kwa wazee ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa dawa zinazolenga wazee peke. Mpango huo umepitishwa na baraza la
madiwani lililofanyika mwisho mwa mwezi wa kumi na moja hivyo utekelezaji wake unatarajiwa
kuanzia januari mwaka 2017.
Faida za mfuko huo wa
Afya ya jamii CHF ni pamoja na kupunguza gharama kama za kufungua faili,
kumuona daktari na kununua dawa hauta kuwepo hali itakayopelekea uhakika wa
afya kwa familia nzima.
Mpaka sasa
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ina kaya wanachama 22,532 wa mfuko wa afya ya jamii CHF, Malengo
ni kufikia kaya wanachama 26,152 ifikapo
June 2017. Uhamasishaji huo ulifanywa kwenye kata saba za Halmashauri ya Wilaya
ya Handeni ambapo mwananchi aliyejiunga siku ya uhamsishwaji alitengenezewa na
kupewa kadi papohapo. Kata hizo ni Segera, Kiva, Kabuku, Komkonga,Kang’ata, Mkata
na Kwamsisi.
Kampeni hii
inaongozwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya na ni
endelevu lengo likiwa ni kuwafikia wananchi wote wa Halmashauri ya
Wilaya ya Handeni. Awamu ya kwanza imemalizika.
...............................
Alda Sadango
Afisa Habari,Halmashauri
ya Wilaya Handeni.
Afisa Tawala Wilaya Bi. Upendo Magashi akizungumza na wananchi wa Kata ya Kabuku kuhusu faida za CHF
Bi.Upendo Magashi akitoa mfano kwa kumzawadia mmoja wa wananchi wa kata ya Segera elfu kumi iliyomuwezesha kujiunga na CHF
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Credianus Mgimba akizungumza na wananchi wakati wa uhamasishaji
Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Bw. Salumu Masokola akiwaeleza wananchi umuhimu wa mfuko wa afya ya jamii CHF.
Mwenyekiti kamati ya Elimu, Afya na Maji Bw. Joel Mabula akiwahamasisha wananchi wakati wa kampeni hiyo
Mratibu wa mfuko wa Afya ya jamii CHF wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Godfrey Vedasto akiwaeleza wananchi faida za CHF.
baadhi ya wananchi walioshiriki kampeni ya uhamasishaji wa CHF
No comments:
Post a Comment