Pages

December 24, 2016

WACHIMBAJI WA MADINI YA JASI NCHINI WAMETAKIWA KUUNDA UMOJA

Mkurugenzi wa mgodi wa Jasi wa Kwanza Kilwa Mining Products, Mwalimu Zuberi (kushoto) akizungumza jambo. Kulia ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akimsikiliza wakati wa ziara yake mgodini hapo.
Madini ya Jasi yakiwa yamelundikwa kandokando ya barabara kuu yakisubiri soko.

Wachimbaji wa madini ya Jasi kote nchini wametakiwa kuhakikisha wanaunda Umoja ili kuwa na uchimbaji wenye tija.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipofanya ziara katika machimbo ya madini ya Jasi Mkoani Lindi na kuzungumza na wachimbaji wa madini hayo mkoani humo.

Alielezwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji hao ikiwemo ukosefu wa vifaa vya uchimbaji madini, ubovu wa miundombinu ya barabara hususan kipindi cha masika ambapo zinakuwa hazipitiki ikizingatiwa kuwa machimbo husika yapo mbali na barabara kuu, kutokuwa na taarifa zakutosha za kijiolojia za maeneo husika, soko la kusuasua pamoja na malipo duni.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa mgodi wa Kwanza Kilwa Mining Products, Mwalimu Zuberi alisema mgodi wake unao uwezo wa kuzalisha kiasi cha tani 15,000 kwa mwezi lakini kutokana na mahitaji, unazalisha tani 5,000 tu.
Aliongeza kuwa, kwa upande wa Tanzania soko limekuwa likisuasua kwani wanunuzi wake walio wengi ambao wengi wao ni kampuni za saruji tayari wanao mzigo wa kutosha na hivyo hawahitaji mzigo mwingine kwa sasa.
“Nimezitembelea Kampuni nyingi za saruji ambazo tunaziuzia Jasi, lakini kwa sasa karibu zote hazihitaji mzigo mwingine hivyo tunazalisha na kusogeza mzigo kandokando ya barabara kuu ili kutakapokuwa na mahitaji tunapeleka,” alisema.
Mbali na hilo, Zuberi alisema suala la malipo limekuwa na usumbufu. “Unapeleka mzigo leo lakini inachukua hadi miezi minne ndiyo unalipwa,” alisema.
Zuberi alisema hivi sasa wachimbaji wa jasi mkaoni humo wanauza madini hayo nje ya nchi ikiwemo Congo, Rwanda, Malawi, Msumbiji na Zambia.
Waziri Muhongo alisema baadhi ya changamoto zinatokana na wachimbaji kutokuwa wamoja na hivyo aliwaasa kuhakikisha wanaunda Umoja wa wachimbaji wa Jasi Tanzania ili kuwa na kauli moja wakati wa kusimamia maslahi yao jambo ambalo pia alisema litakuwa ni suluhu kwa baadhi ya changamoto ikiwemo ya bei na masoko.
Aliwaasa kuaminiana, kupendana na kuepuka ubinafsi ili kuwa na uchimbaji wenye tija. “Ili mfaidi matunda ya uchimbaji wa Jasi ni vema mkaachana na umimi, mfanye shughuli zenu kwa kushirikiana na hili litawezekana mtakapounda Umoja wenu,” alisema.
Aliongeza kuwa Umoja uwe ni maalumu kwa wachimbaji wote wa madini ya Jasi kutoka Mikoa yote ambayo madini husika yanachimbwa ili kuwa na maamuzi ya pamoja hususan kwenye masuala ya bei, masoko na kubadilishana uzoefu wa shughuli husika.
“Kwa hapa nchini, si Lindi peke yenu ndiyo mnachimba Jasi lakini po mikoa mingine kama Singida na Dodoma ambapo pia kuna madini haya tena kwa wingi kuliko hapa; hivyo ni vema mkashirikiana,” alisema.
Aidha, baada ya kutembelea migodi mbalimbali ya madini hayo mkoani Lindi, Waziri Muhongo alisema kuwa alichobaini ni kwamba baadhi ya wachimbaji wanafanya shughuli zao kwa kubahatisha bila kuwa na taarifa sahihi za kijiolojia.
Aaliuagiza Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Tiafa (STAMICO) kufika kwenye maeneo husika na kufanya vipimo ‘geological mapping’ kuchambua wingi wa madini yaliyopo kwenye migodi husika na vilevile kufanya tathmini za mara kwa mara za ubora wa madini hayo.
Mbali na hilo, Profesa Muhongo alisema Serikali kupitia Kamati Maalum inayoshughulika na masuala ya madini ya Jasi na Makaa ya Mawe iliyo chini ya Uenyekiti wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe itahakikisha inakuwa na mikakati madhubuti ya kumaliza changamoto zilizopo.
Vilevile alisema Kamati hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine, itafanya tathmini ya kubaini soko la Jasi nchini na nje ya nchi. “Ni muhimu tuelewe mahitaji yaliyopo na yatakayokuwepo siku zijazo kwani matumizi ya madini ya Jasi yameongezeka na yanaendelea kukua,” alisema.
Profesa Muhongo alifanya ziara kwenye machimbo hayo ili kujionea shughuli za uchimbaji wa madini ya Jasi mkoani humo pamoja na kuzungumza na wachimbaji ili kubaini changamoto zinazowakabili kwa ajili ya ufumbuzi.
Waziri Muhongo anaendelea na ziara yake ya siku 14 ya kukagua shughuli za uchimbaji madini pamoja na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya nishati ya umeme nchini.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...