Pages

October 28, 2016

Wananchi wa Mundarara wajitolea ujenzi wa Daraja

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo akimkabdihi Mkuu wa Shule ya Sekondari  Engaranaibo  Mwl. Petro Sabatho Tsh 500,000 kwa ajili ya  kuchangia ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule hiyo wakati wa ziara yake inayoendelea katika Wilaya ya Longido.
  Viogozi wa Chama na Serikali Mkoa wa Arusha pamoja na wananchi wa kijiji cha Olgira Kata ya Mundarara wakielekea kwenye eneo la ujenzi wa daraja ambalo linajengwa kwa nguvu za wananchi.
   Hili ndilo daraja ambalo wananchi wa Kata ya Mundarara wamejitolea fedha na nguvu zao kuhakikisha ujenzi wa daraja unakamilika na kufanya barabara zinazounganisha vijiji vyao kupitika kipindi chote cha mwaka.
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (aliyeko kwenye mtaro) akishiriki ujenzi wa daraja la chini linalojengwa na wananchi wa Mundarara.
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (katikati) akihamasisha wananchi waendelee kuchangia ujenzi wa daraja la Mundarara ili liweze kukamilika kwa wakati.
 Wanawake wa Jamii ya Kimaasai maarufu kama Siangiki walijitokeza barabarani kumlaki Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakati wa ziara yake wilayani Longido.
1Mabinti wa jamii ya kimaasai maarufu kama Selengeni pia walishirki mapokezi ya Mkuu wa Mkoa wakati wa ziara ya kazi wilayani Longido.


Nteghenjwa Hosseah - Longido 

Wananchi wa Kijiji cha Orgirah Kilichopo Kata ya Mundarara Tarafa ya Engarenaibor Wilayani Longido wamelazimika kutumia nguvu zao binafsi kujenga daraja la chini kwa ajili lengo la kuunganisha mawasiliano ya barabara kati ya kata hiyo na kata ya Gelai.

Aidha wamelalamikia kero ya maji tangu mwaka 2013 hadi leo hii hakuna maji yanayotoka kwenye mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) unaolenga kusaidia vijiji vitano kwenye kata hiyo.

Wakiongea na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye anaendelea na ziara yake kwenye wilaya hiyo jana, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Orgirah, Mathayo Laizer alisema mradi huo wa daraja ni muhimu kwao kwani unafungua fursa za kimaendeleo katika kata mbili za Mundarara na Gelai.

Alisema mradi ulianza mwaka jana na walipata michango mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo ambayo ilitoa Sh. 400,000, Ofisi ya Mkurugenzi Sh, 640,000 na wananchi walichanga Sh, milioni 5.3 lakini ili waweze kukamilisha ujenzi wa daraja hilo wanahitaji mifuko ya saruji 135 pamoja na ndono za kuweka kingo pembeni ya daraja hilo zenye thamani ya Sh milioni 2.9

Naye Esther Mathayo alimuomba Rc, Gambo kuwasaidia kutatua kero ya maji katika kata hiyo ambayo ipo kwenye mradi wa benki ya Dunia tangu mwaka 2013 lakini hadi leo wananchi wanatembea umbali mrefu kutafuta maji hayo kwaajili ya matumizi mbalimbali.

Alisema awali mradi huo uliofadhiliwa na benki ya dunia ulilenga kusaidia vijiji vitano na ulijengwa katika kata hiyo zaidi ya miaka minne iliyopita lakini cha ajabu kwenye chanzo cha maji hakukuguswa na baadhi ya miundombinu imeharibika iliyokwisha wekwa awali sehemu mbalimbali na hawajui ni kwanini umekwama.

Baada ya wananchi kutoa kero zao, Rc Gambo aliwapongeza wananchi hao kwa ujenzi wa daraja hilo la chini kwa kutumia nguvu zao wenyewe kwa kuleta maendeleo ikiwemo kufungua njia za mawasiliano kati ya sehemu moja na nyingine.

"Nawapongeza kwa kazi hii mliyojitolea kwaajili ya kutatua changamoto ya usafiri lakini pia natoa rai kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido, Juma Mhina kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa mradi huu wa maji kama ni fedha watenge kwenye bajeti ya halmashauri hiyo ili wananchi wanywe maji "

Pia aliweza kuchangia mifuko ya saruji 30, pamoja na kufanya harambee na kuchangisha zaidi ya Sh, milioni 1 kutoka kwa watumishi wa sekta mbalimbali alioambatana nao ili daraja hilo liweze kukamilika,awali Gambo kwa kushirikiana na Mkuu wa wilaya hiyo, Daniel Chongolo waliingia ndani ya kingo za daraja hilo kwaajili ya kusaidiana na wananchi kuweka mawe kwenye msingi wa daraja pamoja na wananchi wa kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...