Pages

October 9, 2016

MADEREVA BODABODA TABATA KIMANGA JIJINI DAR ES SALAAM WAWALALAMIKIA POLISI KWA RUSHWA


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar, Simon Sirro
Na Dotto Mwaibale

WAENDESHA Pikipiki maarufu kama bodaboda wa Tabata Kimanga jijini Dar es Salaam wamewalalamikia askari polisi kwa kuwakamata na kuwadai ya rushwa kwa nguvu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mtandao wa www.habari za jamii.com  walisema kuwa askari hao wamekuwa ni kero kubwa kwao lakini wanashindwa cha kufanya baada ya kupeleka malalamiko yao kwa wahusika bila kuchukuliwa hatua.

"Sisi waendesha bodaboda wa kituo cha Kamene hapa Tabata Kimanga tunanyanyasika sana  na hawa askari wanakuja usiku wakiwa wamevaa nguo za kiraia na kutukamata na tunapotaka watuoneshe vitambulisho vyao inakuwa umetenda kosa utachukuliwa mzobemzobe na kubambikiwa makosa" alisema mmoja wa waendesha boda boda hao ambaye jina lake tumelihifadhi.

Alisema wakiwakamata hawawapeleki kituo cha Polisi Tabata bali uwapeleka Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Tabata Kimanga ambapo pana baa moja na kuwataka wanunuliwe kitimoto na kupewa rushwa na na wakibishiwa dereva husika ubambikiwa makosa zaidi ya matano na kutakiwa kulipa faini ya sh.30,000 kwa kila kosa.

Mwendesha bodaboda mwingine alisema kuwa askari hao wamekuwa wakiwavizia katika maeneo ya kwa Swai, Mbuyuni na barabara ya Chang'ombe.

Alisema makosa yao makubwa ni kutokuwa na kofia ngumu, kusahau leseni nyumbani lakini wakiwaeleza hawapewi nafasi ya kujitetea badala yake ulazimishwa kutoa rushwa.

Dereva huyo aliongeza kuwa kibaya zaidi wakifikishwa kituoni na pikipiki ikikaa siku tatu wakienda kuichukua ukuta betri, vioo na mafuta yameibwa na wakiuliza wanasema hawakuandikishiana hivyo wasilalamike.

Aliongeza kuwa malalamikio yao wamekuwa wakiyawasilisha kwa wakuu wa polisi wa kituo hicho kupitia mikutano yao mbalimbali lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya askari hao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna Msaidizi (ACP), Salum Hamdun alipopigiwa simu ili kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana baada ya simu yake kuita kwa muda mrefu bila ya kupokelewa.


No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...