Pages

August 7, 2016

Serikali ya Brazil yaonyesha nia ya kufanikisha azma ya Rais. Dkt. Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente, wakati Balozi huyo alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente (Kushoto), akisaini Kitabu cha Wageni ofisini kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia), alipomtembelea Waziri na kufanya naye mazungumzo kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili hususan katika uwekezaji kwenye sekta ya nishati.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kushoto), akimsikiliza kwa makini Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente (Kulia), wakati Balozi huyo alipomtembelea Waziri Ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kufanya mazungumzo naye kuhusu masuala ya uwekezaji katika sekta za nishati na madini. Wengine pichani ni Maafisa wa Wizara waliohudhuria mkutano huo.

Na Veronica Simba

Serikali ya Brazil imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati nchini hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia maji na mabaki ya miwa. Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente, alipomtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake na kufanya mazungumzo naye.

Balozi Puente alimweleza Profesa Muhongo kuwa nchi yake inao ujuzi na uzoefu wa kutosha katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali hususan maji.

Alisema, Brazil ingependa kuchangia kufanikisha azma ya Rais John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.

“Kutekeleza mchakato wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda, unahitaji umeme mwingi unaotokana na vyanzo mbalimbali. Ni bahati nzuri kwamba Tanzania inazo njia za kufanikisha azma hiyo,” alisema.

Alisema kuwa, nchini Brazil, kuna Kampuni kubwa zenye uzoefu wa muda mrefu unaofikia miaka 20 hadi 40 katika kazi hiyo, ambazo huzalisha umeme wa maji nchini mwao na hata nje ya nchi.

Pia, alitaja eneo jingine ambalo nchi yake ina nia ya kuwekeza kuwa ni uzalishaji wa umeme unaotumia mabaki ya miwa ambayo aliielezea kuwa chanzo kizuri cha nishati safi.

Balozi Puente alisisitiza kuwa, Brazil ikiwa ni nchi inayozalisha miwa kwa kiwango kikubwa duniani, itasaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya nishati kwa kuzalisha umeme unaotokana na mabaki ya miwa kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Kwa upande wake, Waziri Muhongo, akimjibu Balozi Puente, alikiri kuwa kuwa Brazil ina ujuzi, uzoefu na uwezo mkubwa hususan katika maeneo ambayo Balozi aliyataja na hivyo akamwambia nchi hiyo inakaribishwa kuwekeza Tanzania kwa kufuata masharti na utaratibu uliowekwa na Serikali.

Akizungumzia zaidi kuhusu utaratibu wa uwekezaji, Waziri Muhongo alieleza kwamba Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara yake, inabadilisha utaratibu wa kupokea wawekezaji katika sekta husika.

Alisema, kunaandaliwa utaratibu maalum utakaokuwa wa wazi na kuruhusu ushindani kwa wenye nia ya kuwekeza kwa malengo ya kupunguza au kuondoa kabisa mazingira ya rushwa na muda mrefu unaotumika katika majadiliano pasipo sababu za msingi.

Profesa Muhongo alifafanua zaidi kwamba, Serikali itaweka mazingira mazuri zaidi ya ushindani kwa kuandaa maelezo ambayo pamoja na mambo mengine yatabainisha aina mbalimbali za vyanzo vya umeme vilivyopo nchini pamoja na maeneo vilipo.

Alisema, Kampuni zenye nia ya kuwekeza zitakaribishwa kupendekeza viwango vya bei vitakavyotumika kuuza umeme utakaozalishwa na zitashindanishwa, ambapo washindi wachache watachaguliwa kwa ajili ya majadiliano kabla ya kuingia mkataba wa uwekezaji husika.

“Kwa hivyo, tunaandaa kabrasha maalum litakalokuwa na maelezo husika na litakuwa tayari mwezi wa Septemba mwaka huu. Kabrasha hilo lenye maelezo litatumika kama mwongozo wa ushindanishaji maombi mbalimbali ya uwekezaji hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kwa uwazi,” alisisitiza.

Alivitaja vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na gesi asilia, makaa ya mawe, maji, jua, upepo, jotoardhi, mawimbi ya bahari pamoja na nishati mbadala. Waziri Muhongo alisema kuwa maelezo hayo maalum yatasambazwa kwa wadau mbalimbali wa sekta husika wakiwemo wale wote wenye nia ya kuwekeza ikiwa ni pamoja nan chi ya Brazil kupitia Ubalozi wake hapa nchini.

“Kwa kutumia Kabrasha hilo maalum lenye maelezo husika, wewe Balozi utaweza kuwashawishi wafanyabiashara kutoka nchini kwako kutoa mapendekezo ya uwekezaji ambayo yana vigezo vyote muhimu vinavyoshawishi wapate fursa husika za uwekezaji katika sekta ya nishati,” Profesa Muhongo alimweleza Balozi Puente.

Kuhusu Mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, ambao pia Brazil imeonesha nia kuwa ingependa kuwekeza kwa kushirikiana na Tanzania; Profesa Muhongo alisema Serikali itaweza kulisemea hilo baada ya kipindi cha miezi takribani 45 kupita, ambapo mambo yote ya kisheria kuhusu Mradi huo yanatarajiwa kuwa yamekamilika.

Aidha, Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuomba nafasi za masomo nchini Brazil kwa wanafunzi wa kitanzania katika ngazi za Shahada za Uzamili na Uzamivu katika sekta ya Nishati hususan Mafuta na Gesi, kwa kuzingatia kuwa Brazil imeendelea sana katika sekta hiyo.

“Ninyi mnazo Taasisi bora kabisa za Utafiti duniani. Mnafanya vizuri sana katika maeneo mbalimbali.”

Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, Brazil ni miongoni mwa nchi Tano (5) bora duniani zinazozalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu kwa sababu umeme mwingi wanaozalisha unatokana na maji, kutoka katika Mito mikubwa waliyonayo.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...