Serikali imepata gawio la shilingi Bil. 23 kutoka Kampuni tatu za NMB Bank PLC, Puma Energy na Tiper (T) ikiwa ni faida iliyotokana na biashara iliyofanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016, ambazo imewekeza hisa zake kati ya asilimia 31 na 50.
Mfano wa hundi zenye thamani ya kiasi hicho cha fedha zimekabidhiwa kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, katika Ofisi za Hazina Ndogo Mjini Dodoma, leo Juni 9, 2016
Kampuni ya kwanza kukabidhi gawio (dividends) ni Puma Energy, inayojihusisha na biashara ya kuuza mafuta, ambayo serikali ina hisa zake asilimia 50 iliyokabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi Bil. 4.5 (Bilioni 4 nukta 5) baada ya kampuni hiyo kupata faida ya shilingi Bil. 9 katika kipindi kinachoishia Desemba mwaka jana
Kampuni ya Tiper (T) inayofanya biashara ya uhifadhi wa mafuta (storage), ambayo serikali ina hisa ya asilimia 50 pia, imekabidhi gawio la shilingi Bil 2.0 (Bilioni 2 nukta 0) na kufuatiwa na Benki ya NMB PLC, iliyomkabidhi Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango, hundi kifani yenye thamani ya shilingi Bilioni 16.5 (Bilioni 16 nukta 5)
Serikali imepata kiasi hicho cha fedha kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inayosimamia Mashirika, Taasisi za Umma na Kampuni zenye hisa na serikali.
Akizungumza baada ya kupokea hundi hizo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amezishukuru kampuni hizo kwa kuiwezesha serikali kupata kiasi kikubwa cha fedha zitakazotumika kuwahudumia wananchi.
"leo ni siku yangu ya furaha sana kwa kupata kiasi kikubwa cha fedha kiasi hiki ikiwa ni siku moja tu tangu niwasilishe Bajeti Kuu ya Serikali Bungeni hapa Mjini Dodoma" aliongeza Dkt. Mpango
Amemwagiza Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru, kuhakikisha kuwa kampuni zote ambazo serikali ni mbia zianze kulipa gawio kwa serikali na kuacha visingizio vya kutangaza kupata hasara kila mwaka wakati hawafungi biashara zao.
"Naomba vyombo vinavyohusika na ukusanyaji wa mapato ya serikali pamoja na Msajili wa Hazina kuzifuatilia na kuzikagua kampuni ambazo serikali ina hisa ili kubaini ukweli ni kwanini hazitoi gawio zikisingizia kupata hasara kwenye biashara wakati hawafungi biashara hizo" Alisisitiza Dk. Mpango
Dk. Mpango pia amevitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi, ili kubaini mianya ya upotevu wa mafuta bandarini na kuagiza wale wote walihusika na upotevu huo wachukuliwe hatua.
" Haiwezekani wajanja wachache wanafaidika halafu wananchi wanyonge wanalala chini hospitalini, Nilisema jana na leo narudia yeyote anayetukwamisha kwenye maendeleo ni msaliti lazima washughulikiwe kwa mujibu wa sheria bila huruma,” alisema.
Awali Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, amezipongeza kampuni hizo kwa kutoa gawio hilo na kumhakikishia Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Philip Mpango, kuwa gawio litaongezeka kwa kasi kubwa katika miaka ijayo ili kuiwezesha serikali kuwa na uwezo zaidi wa kuwahudumia wananchi.
“Mwaka 2014 tulipata gawio la Sh bilioni 3 kutoka Kampuni ya PUMA Energy, mwaka huu tumepata bilioni 4.5 ni matarajio ya Serikali kwa mwendo huu mwakani tunaweza kupata bilioni 6" alisema Dkt. Kalemani.
Alitoa wito pia kwa kampuni nyingine zenye ubia na Serikali ambazo hazitoi gawio zianze sasa kutoa akieleza kuwa mantiki ya gawio ni kwamba kampuni inafanya kazi na inapata faida, inapokuwa haitoi gawio mantiki yake ni kwamba kampuni inafanya kazi haipati faida.
“Lakini ni vigumu kuamini kama kampuni hazipati faida kwa mfululizo wa miaka 10 na inafanya kazi, sisi tunaamini wanapata faida, na zipo kampuni nyingi ambazo si busara kuzitaja hapa zinadai kupata hasara kila mwaka,” alisema.
Kuhusu upotevu wa mafuta bandarini, Dk. Kalemani alisema tatizo hilo hivi sasa limedhibitiwa, baada ya Serikali kuanzisha chombo maalumu kinachoratibu na kudhibiti upotevu huo.
Alikuwa akijibu changamoto iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Puma Energy, Dkt. Ben Moshi, aliyeelezea kuwa katika kipindi cha mwaka 2014/2015 kampuni hiyo imepata hasara ya Dola za Marekani milioni 1.4 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 2.5 kutokana na upotevu huo wa mafuta.
Kwaupande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Tiper (T), inayojihusisha na uhifadhi wa mafuta, ambapo amesema tangu mwaka 2010, kampuni hiyo imetoa gawio la shilingi Bil. 6.4 kwa serikali na kuahidi kuwa gawio hilo litaongezeka siku za usoni.
Naye Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker, amesema kuwa benki yake inajisikia fahari kubwa kugawa faida iliyopata katika biashara zake kwa mbia wake ambaye ni serikali.
Amesema kuwa pamoja na serikali kuwa mbia kwa hisa ya asilimia 31.8, lakini pia ni mteja mkubwa wa benki hiyo ambayo hurudisha faida ya uwekezaji kwa wananchi kupitia gawio hilo na kutoa wito kwa watanzania kuitumia benki hiyo kuweka amana na kukopa
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ambaye ametoa wito kwa wawekezaji wakiwemo wale wanaofanya biashara zao kwa kushirikiana na serikali kufanyakazi zao kwa uaminifu kwa kutangaza faida wanazopata kihalali ili serikali iweze kupata mapato yake yatakayosaidia kuboresha maisha ya wananchi
Naye Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru, ameahidi kuyafuatilia na kuyasimamia mashirika yote ya umma na yale ambayo serikali imewekeza, ili kuhakikisha kuwa hawakwepi kulipa gawio ili kuiwezesha serikali kupata mapato yake
Imetolewa na
Benny Mwaipaja
Kaimu Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru, akifafanua jambo wakati wa Hafla fupi ya serikali kukabidhiwa Hundi za Mfano zenye thamani ya shilingi Bilioni 23 kutoka kwa Kampuni za Puma Energy, Tiper (T) na NBC Bank PLC, ambazo imewekeza hisa zake, katika ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Puma Energy Dkt Ben Mosha, akizungumza Jambo wakati wa Hafla fupi ya serikali kukabidhiwa Hundi za Mfano zenye thamani ya shilingi Bilioni 23 kutoka kwa Kampuni za Puma Energy, Tiper (T) na NBC Bank PLC, ambazo imewekeza hisa zake, katika ukumbi wa Hazina Mini Dodoma
Naibu Waziri wa Nishati na Mdini Dk. Medard Kalemani, akizungumza jambo wakati wa Hafla fupi ya serikali kukabidhiwa Hundi za Mfano zenye thamani ya shilingi Bilioni 23 kutoka kwa Kampuni za Puma Energy, Tiper (T) na NBC Bank PLC, ambazo imewekeza hisa zake, katika ukumbi wa Hazina (Treasury Squire) Mjini Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango(Mb), (Katikati) akimwelekeza jambo Msajili wa Hazina Laurence Mafuru, wakati wa Hafla fupi ya serikali kukabidhiwa Hundi za Mfano zenye thamani ya shilingi Bilioni 23 kutoka Kampuni za Puma Energy, Tiper (T) na NBC Bank PLC, ambazo imewekeza hisa zake, katika ukumbi wa Hazina (Treasury Squire) Mjini Dodoma
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb) akizungumza jambo wakati wa Hafla fupi ya serikali kukabidhiwa Hundi za Mfano zenye thamani ya shilingi Bilioni 23 kutoka Kampuni za Puma Energy, Tiper (T) na NBC Bank PLC, ambazo imewekeza hisa zake, katika ukumbi wa Hazina (Treasury Squire) Mjini Dodoma
No comments:
Post a Comment