Pages

March 17, 2016

TUSHIRIKIANE KUTOKOMEZA UKEKETAJI KWA WATOTO WA KIKE-UMMY MWALIMU

 Mhe Waziri Ummy  Mwalimu akibadilishana mawazo na washiriki wa majadiliano kuhusu ukeketaji.
 Waziri  Mwalimu akibadilishana  mawazo na Waziri  mwenzie Sicily Kariuki kutoka  Kenya
 Mhe. Waziri wa Afya.Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumzia uzefu wa Tanzania katika kukabiliana na tatizo la  ukeketaji akiwa na wazungumzaji wengine katika Meza Kuu, kutoka kushoto ni Mke wa  Rais wa Burkina Faso Bi. Sika Bella Kabore,  Bw. Benoit Kalasi (UNFPA), Bi.Emma Bonino Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje Italia.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Mhe. Peter Serukamba akifuatilia majadiliano kuhusu tatizo la  ukeketaji  na  adhari zake wa afya na maendeleo ya mtoto wa kike na mwanamke.
 Wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi nao wakifuatilia majadiliano  yaliyovutia washiriki wengi kuhusu madhara  yatokanayo  na ukeketaji na namna gani  jamii inatakiwa kushirikiana kutokoza tatizo hilo. 
Sehemu ya washiriki wa Mkutano na majadiliano  kuhusu utokomezaji wa vitendo vya ukeketaji na uhusiano wake na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu. Mkutano huu  uliandaliwa kwa pamoja na Wakilishi za  Kudumu za Tanzania, Burkina Faso, Italy, Iran, UNFPA na UNCEF.
Na Mwandishi Maalum, New York
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ( Mb)  amesisitiza   kuwa ni  kwa ushirikiano baina ya Serikali  na  jamii ndipo tatizo la ukeketaji  kwa watoto wa kike na wanawake litakapoweza kutokomezwa.
Akaongeza kwamba, serikali  inaweza kutunga sheria nyingi  za kukabiliana na tatizo hilo  lakini kama jamii yenyewe  kuanzia ngazi  ya familia isipotoa ushuriano wa dhani itachukua muda mrefu kwa tatizo hilo kutokomezwa. Alikuwa akizungumza wakati wa majadiliano ya mkutano wa  kuhusu  utokomezwaji  vitendo vya ukeketaji kama sehemu  muhimu ya utekelezaji wa Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030.
Waziri Ummy Mwalimu alikuwa mmoja wa  wazungumzaji wakuu  katika  mkutano  huo  uliowahusisha  Mke wa Rais wa  Burkina Faso, Bibi. Sika Bella Kabore, Mawaziri na  Asasi za Kiraia na uliandaliwa kwa pamoja  na Wakilishi za kudumu za Tanzania,  Italy, Iran, Burkina Faso,UNFPA na UNICEF, ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 60 wa Kamisheni  ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Wanawake.
Na kwa sababu hiyo, Waziri  Ummy Mwalimu, amerejea kutoa wito kwa watanzania wote kwa  katika ujumla wao   wakiwamo wazee wa kimila, viongozi wa dini na vijana wakiume    kutoa ushirikiano kwa  serikali na wadau wengine ili hatimaye tatizo hilo ambalo   linaelezwa  kuwa  siyo tu lina madhara makubwa kiafya na kisaikolojia lakini pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
“Tunatakiwa kufanya kazi kwa  pamoja na katika umoja  wetu, serikali peke yake haitaweza kulimaliza tatizo hili, ambalo  imefikia mahali  sasa  wazazi kwa kuongopa mkono wa sharia wanaamua kuwafanyia ukeketeji watoto wa kike katika umri  mdogo sana” Akaeleza Waziri.Akasema  , Tanzania  imebaini  uelimishwaji na  majadiliano  yanayohusisha familia na vijana wakiume ni muhumu katika kuchangiza juhudi za serikali katika  kukabili ukeketaji.
“Tunawaelimisha  pia vijana wa kiume ili waelewe madhara ya ukeketaji kwa sababu wao ni wadau wakubwa kama waume watarajiwa. Lakini pia tunawaelimisha wasichana ambao wengine huamua kufanyiwa ukeketaji kwa hofu ya kutokuja olewa”. Amesema Waziri.
Akasema Tanzania imeshukuru  kwamba tatizo  la Ukeketaji  limepewa umuhimu na nafasi katika Ajenda mpya ya Maendeleo  endelevu , ambapo katika lengo namba tano  linalohusu Usawa wa Kijinsia, linaeleza zaidi  umuhimu kumalizwa kwa vitendo vyote vibaya kama vile   ndoa za utotoni, ndoa za kulazimishwa na  ukeketaji ifikapo mwaka 2030. 
 Naye  Mke wa Rais wa Burkina Faso, Bi. Sika Bella Kabore akizungumza katika  mkutano huo amesema kuwa  tatizo la ukeketaji  ni  la kimila na kitamaduni maeneo ambayo ameyataja kwamba yatanakiwa kufanyiwa kazi ya ziada   ili kumaliza tatizo  hilo. 
“Tukiweza kulimaliza tatizo hilo  tutakuwa pia  tumefanikiwa  katika kutetea  haki  za wanawake na watoto wa kike lakini pia tutamaliza ukatili dhidi ya wanawake, ukeketaji hauna nafasi katika Dini au Imani  yoyote ile” Akasisiza Bi. Sika Bella Kabore.
Naye   Dr. Lina Kilimo kutoka  Kenya,  yeye kwa  upande wake amesema tatizo la  ukeketaji si la  Afrika au Asia  peke yake bali ni la dunia nzima na kwamba kwa kuingizwa katika   Agenda 2030 imedhihirisha wazi  kwamba  bila msukuko  na ushirikiano kutoka  pande zote itakuwa kazi kulimaliza tatizo hilo.
Kwa upande wake Dr. Morissanda Kouyate  katika mchango wake amesema, ifikie mahali viongozi   wasione aibu kulizungumzia hadharani  tatizo  na madhara ya  ukeketaji na kwamba hakuna tena muda wa kusubiri.  Madhumuni ya mkutano  huu pamoja na mambo mengine  yalikuwa ni kwa wajumbe wanaoudhuria mkutano wa 60 wa  Kamisheni kuhusu hali ya Wanawake, kubadiliana uzoefu, changamoto  pamoja na  kujifunza mbinu ambazo nchi nyingine zinatumia kusukuma mbele jitihada za kutokomeza  vitendo vya ukeketaji.
Inaelezwa kwamba Zaidi ya wanawake na watoto milioni 200 duniani kote wamefanyiwa ukeketaji , Afrika,  Mashariki ya Kati, Asia,  Latin America,  Ulaya, Amerika ya Magharibi  Australia na New Zeland. Kumalizwa  kwa vitendo vya  ukeketaji ni moja ya  hatua muhimu katika kufanikisha malengo mengine ya maendeleo endelevu yakiwamo yanayohusu upatikanaji  wa elimu bora,  huduma za afya , ajira zenye hadhi na ukuaji wa uchumi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...