Na Benedict Liwenga-Maelezo.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai (Mb) amefanya mabadiliko ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge ili kuzingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuunda Kamati hizo mwezi Januari 2016.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Ofisi ya Bunge Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ambapo imeelezwa kuwa, mabadiliko hayo, yamefanywa chini ya Kanuni ya 116(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayompa Spika Mamlaka ya kuteua Wabunge kuunda Kamati Mbalimbali za Bunge.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kufuatia mabadiliko hayo ambayo baadhi yake yamehusu Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au wote wawili, Kamati za Kudumu za Bunge zilizoathirika na mabadiliko haya zitawajibika kufanya Uchaguzi wa viongozi kwa mujibu wa kanuni ya 116 (10).
Baadhi ya Kamati ambazo zimeathirika na mabadiliko hayo na ambazo zitawajibika kufanya uchaguzi kwa viongozi ni zikiwemo; Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambayo itahitaji kupata Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wapya, Kamati ya Nishati na Madini ambayo itahitaji kupata Mwenyekiti mpya, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma itahitaji kupata Mwenyekiti mpya, Kamati ya LAAC ambayo pia itahitaji kupata Makamu Mwenyekiti mpya na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo itahitaji kupata Makamu Mwenyekiti mpya.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza pia mabadiliko hayo kwenye kamati zote yanaanza mara moja ambapo orodha ya wajumbe waliobadilishwa imeshatolewa na Ofisi hiyo na kusambazwa katika vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment