Pages

March 24, 2016

MAMLAKA YA HALI YA HEWA YAADHIMISHA KILELE CHA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIA KWA KUPANDA MITI

Jumuiya ya kimataifa ya hali ya hewa duniani kote inaadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani, ikiwa ni Siku ya kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) tarehe 23 Machi 1950. Tanzania pamoja na wanachama wengine 190 wa Shirika hili inaungana na jumuiya ya kimataifa kusherehekea siku hii kwa kuonesha mchango wa huduma za hali ya hewa katika kulinda usalama wa jamii.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa mnamo Desemba, 1999 baada ya Serikali kuchukua uamuzi wa kuboresha utoaji wa huduma kwa sekta mbali mbali muhimu chini ya sheria ya Wakala wa Serikali No. 30 ya 1997. Kabla ya TMA huduma hizi zilikuwa zikitolewa na iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa (DoM) chini ya iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi. 

Katika kusherehekea Siku ya Hali ya Hewa Duniani ni desturi kuwa na kaulimbiu ya maadhimisho ya kila mwaka, hivyo kwa mwaka huu kaulimbiu ya maadhimisho haya ni “ Joto kali, Ukame, Mafuriko; Kabiliana na Mabadiliko”-“Hotter, Drier, Wetter - Face the Future’.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi akiwa sambamba na baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, wakipanda miti katika eneo la TMA lililopo Sinza (kituo cha Simu 2000). Zoezi hili limefanyika katika maeneo ya mikoa yote nchini kupitia Ofisi za TMA na Wakala wa Misitu Tanzania Tarehe 23 Machi 2016.

 Kaulimbiu hii ni ya muhimu kwa kipindi hiki ambacho jamii nyingi nchini Tanzania na kwingineko duniani wanakabiliana na matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa joto kupita wastani na kubadilika kwa mifumo na misimu ya mvua. Hali hii ni dhahiri kwani jamii zetu nyingi zimeathirika kwa namna moja au nyingine kutokana na matukio haya ya hali mbaya ya hewa ambayo tafiti za kisayansi zimeyahusisha na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
  
Katika miongo ya hivi karibuni, mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri mifumo ya asili na ya kibinadamu katika nchi nyingi. Mabadiliko ya matukio ya hali mbaya ya hewa ya muda mfupi na mrefu nidhahiri na hali hii inakaribia kuzoeleka na kuwa kama wastani mpya wa hali ya hewa katika nchi nyingi ikiwa pamoja na Tanzania. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi akipanda mti katika eneo la TMA lililopo Sinza (kituo cha Simu 2000). Zoezi hili limefanyika katika maeneo ya mikoa yote nchini kupitia Ofisi za TMA na Wakala wa Misitu Tanzania Tarehe 23 Machi 2016.

Katika miaka ya hivi karibuni Tanzania imeshuhudia athari za maafa yanayosababishwa na mabadiliko haya ya hali ya hewa yakiwa na sura mbalimbali. Mfano, tokea maadhimisho ya siku ya hali ya hewa ya mwaka uliopita tumeshuhudia matukio yaliyosababisha maafa yaliyotokana na mafuriko kwa mfano Mikoa ya kati ya nchi ambapo baadhi ya watu walipoteza maisha pamoja na mifugo na uharibifu wa mali. 

Tafiti za kisayansi na upimaji wa hali ya hewa zinaonyesha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yameendelea kuwa changamoto kubwa na inapasa kuangaliwa kwa makini na nchi zote. Joto la anga na bahari linaendelea kuongezeka, kuyeyuka kwa barafu kwa maeneo ya milima mirefu na yale ya ncha za dunia, kuongezeka kwa kina cha bahari na matukio ya hali mbaya ya hewa yamekuwa yakirudia mara kwa mara na kuongezeka makali. 

Kwa upande wa Tanzania, madhara yaliyokwisha kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa uchache ni pamoja na ongezeko la joto, mafuriko ya mara kwa mara, ukame, mabadiliko ya misimu ya mvua, kuzama kwa baadhi ya visiwa vidogo vidogo, mmomonyoko wa kingo za bahari kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari, kupungua kwa barafu katika mlima Kilimanjaro, kupotea kwa baadhi ya viumbe hai, kuongezeka kwa magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa kama vile malaria hata kwa maeneo ambayo hayakuwahi kuwa na matukio ya magonjwa haya. 

Ripoti za Jopo la Kimataifa la Tafiti za Kisayansi za Mabadiliko ya Hali ya Hewa  “Intergovernmental Panel on Climate Change (IPCC)” zinaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa kabisa shughuli za kila siku za binadamu zimechangia katika mabadiliko ya hali ya hewa na kuwa gesi joto kama vile “Carbon Dioxide- CO2” zimeendelea kuongezeka kufikia viwango vya juu kabisa katika historia ya mwanadamu. 

Kuendelea kutegemea vyanzo vya nishati vinavyozalisha kwa wingi gesi joto hizi kama ilivyo sasa kutasababisha joto la dunia kuendelea kupanda zaidi na ifikapo mwishoni mwa karne hii hali ya joto inaweza kuongezeka kufikia digrii 4 kwa kipimo cha Celsius juu ya wastani kulinganisha na joto wakati wa kabla ya mapinduzi ya viwanda. Kuzuia ongezeko la joto kuwa chini ya digrii 2 bado ni jambo linalowezekana ila inahitaji upunguzaji wa haraka wa gesi joto hizi. Hali ilivyo sasa wastani wa joto wa kila muongo mmoja umekuwa na joto zaidi kulinganisha na uliopita.

Takwimu za hali ya joto la wastani la dunia zinaonyesha kuwa, kipindi cha mwaka 2011 hadi 2015 kimekuwa na joto kali zaidi kulinganisha na vipindi vingine tokea kuanza kwa vipimo hivyo katika miaka ya 1800. Kwa ujumla ongezeko la joto linahusishwa na kuongezeka kwa gesi joto. Mwezi Disemba 2015 wakati wa Mkutano wa kimataifa wa ishirini na moja (21) ambazo zilijadili mabadiliko ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nayo “(Twenty First Conference of Parties (COP 21))” uliofanyika Jijini Paris, Ufaransa, nchi za dunia kwa kauli moja walikubaliana kupitisha makubaliano ya Paris “ Paris Agreement”. 
Makubaliano haya yanalenga kupunguza uzalishaji wa gesi joto kwa kiasi kikubwa. Haya ni makubaliano ya kihistoria ambayo yanazilazimu nchi zote za dunia kuwa na mpango na juhudi mahsusi kupambana na janga la mabadiliko ya hali ya hewa kwa pamoja kulingana pia na kiwango cha uzalishaji wa gesi joto wa kila nchi, yaani “common but differentiated responsibilities”. 

Tunapojiandaa kukabiliana na hali ya baadae ya mabadiliko haya ya hali ya hewa, kila mmoja wetu ana mchango na jukumu la kufuatilia kwa karibu, kuelewa na kukabiliana na hali ya hewa ilivyo leo na itakavyokuwa siku zijazo. Tuendelee kuelimishana kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nayo wakati huo huo tukiendelea kutekeleza sera ambazo zitatusaidia sasa na siku zijazo. 

Sambamba na jitihada hizi jumuiya ya hali ya hewa ya kimataifa kupitia Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorologica Organization-WMO) inatekeleza programu kama ile ya Global Framework for Climate Services (GFCS) yenye lengo la kuwezesha jamii kukabiliana vilivyo na kuchangamkia fursa zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa hususani kwa zile jamii zilizo katika hatari ya kuathirika zaidi.

Serikali yetu inaendelea kujenga uwezo wa kufuatilia kwa karibu mifumo ya utabiri wa hali ya hewa ya muda mfupi na mrefu ambapo taarifa hizi zitasaidia katika kutoa maamuzi mbalimbali na kuandaa sera kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Taarifa na huduma zinazotokana na utabiri wa muda mrefu wa hali ya hewa utaongeza uwezo wa kumaliza au kukabiliana na mabadiliko haya pamoja na kuleta maendeleo endelevu, hivyo kutufanya kuwa mahali pazuri zaidi katika juhudi za kukabiliana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile mvua nyingi kupita wastani, mafuriko na ukame; pia itasaidia wakulima kupanga vema shughuli zao za kilimo; kuongeza usalama wa usafiri wa maji na anga.

Kwa kuzingatia maendeleo haya, ni rai yangu kwa kila mwananchi kutimiza wajibu wake katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake na hivyo tutakuwa tumetoa mchango mkubwa katika kuleta usalama na ustawi wa kila mwananchi wa Taifa letu.

Mabadiliko ya hali ya hewa yanatufanya tushindwe kuwa na uhakika wa mustakabali wetu, hata hivyo jambo moja ni dhahiri kuwa jamii yetu inalo jukumu la kugeuza hali hii, si kwa ajili yetu pekee bali kwa vizazi vijavyo pia. Maamuzi tunayofanya sasa yana matokeo makubwa na yanaweza kubadilisha hali ya baadae ya dunia tunamoishi. Changamoto hizi ni kubwa ila fursa zilizopo za kubadilisha hali ya mambo ni nyingi pia.

Wakati tunaadhimisha siku hii, nawasihi wadau wote wa hali ya hewa katika sekta mbalimbali kujihusisha zaidi katika kuelewa na kufuatilia masuala ya hali ya hewa na mabadiliko yake ili kuweza kuchukua hatua stahiki za kujikinga na kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa kufanya hivyo tutasababisha mazingira tunayoishi yaendelee kubaki katika asili yake na yenye kuvutia kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo.

Nawatakia madhimisho mema na yenye mafanikio ya siku ya  Hali ya Hewa Duniani.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...