Afisa Habari wa Umoja wa Mataifa nchini (UNIC), Usia Nkhoma Ledama
akisoma hotuba ya ufunguzi wa warsha ya Kitenge X Africa X Volunteerism
(KAV) kwa niaba ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa
nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP),
Alvaro Rodriguez.
Vijana nchini hususani wanaomaliza masomo ya vyuo wametakiwa
kujijengea tabia ya kufanya kazi zinazokuwepo pindi wamalizapo masomo
yao na isiwe mpaka kazi inayoanza na maslahi makubwa.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Afisa Habari wa kituo cha
Habari cha Umoja wa Mataifa (National Information Officer-UNIC), Bi.
Usia Nkhoma- Ledama aliyemwakilisha Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez katika warsha iliyozikutanisha taasisi
mbalimbali zinazofanya kazi kwa kujitolea za vijana.
Bi Ledama, alisema kumekuwepo na kundi kubwa la vijana ambao
wamekuwa wakihitimu masomo yao lakini hawajishughulishi na kazi yoyote
lakini kuna wanaweza kutumia fursa zilizopo hata kwa kuanza kwa
kujitolea na kupitia kwenye kazi hiyo akajifungulia milango ya
mafanikio.
Ameongeza kuwa, Vijana wengi wamekuwa wakihitaji kazi ambazo zina
maslahi makubwa pindi tu wanapoanza kazi kwa kipindi kifupi wapate
maisha mazuri bila kutambua kuwa wanahitaji kufanya kazi kwa bidii na
maisha mazuri ndiyo yanafuata.
“Ukitaka maisha mazuri lazima ufanye kazi kwa bidii sio unataka
uanze kazi upange nyumba ya vyumba vitatu na ipo sehemu nzuri, ununue
gari Mark X na mengine mazuri lakini lazima ufanye kwanza kazi,
“Vijana mnatakiwa kutambua kuwa ajira ni ngumu kupatikana hata kwa
kuanza kufanya kazi kwa kujitolea bila malipo unaweza kuwa na juhudi na
mwisho wa siku unakuwa na maisha mazuri,” alieleza Bi Usia Nkhoma
Ledama.
Afisa Habari wa Umoja wa Mataifa nchini (UNIC), Usia Nkhoma Ledama
akizungumza jambo katika warsha ya Kitenge X Africa X Volunteerism
(KAV).
Na kuongeza kuwa vijana wengi wasomi hawajui faida za kuanza kwa
kujitolea kuwa kunampa uzoefu na zaidi katika kuhudumia jamii kwa
shughuli mbalimbali ambazo zinakuwa na kusudi za kuelimisha jamii kuhusu
mambo mengi kwao pia kupata elimu mpya.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya
Vijana, Bi. Esther Liwa amezishauri taasisi za vijana kuwa na utaratibu
wa kutoa elimu kwenye maeneo ya wazi ili kupata nafasi ya kukutana na
vijana wengi zaidi.
Alisema kuna kundi kubwa la vijana walio mtaani hivyo kufanya kwao
maonesho ya wazi watapata nafasi ya kutoa elimu kwa vijana walio mtaani
ambapo nao hawajapata elimu kuhusu kujiunga na taasisi hzio kwa
kujitolea.
Aidha, aliwataka vijana kutumia vitu vilivyo na asili ya Tanzania
kama utambulisho wao kama jina la warsha hiyo lilivyokuwa Kitenge –
Africa – Volunteerism (KAV).
Afisa Mipango wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kujitolea (UNV),
Stella Karegyesa akizungumza na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali (hawapo
pichani) kuhusiana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika lake
wakati wa warsha hiyo.
Baadhi ya vijana walioshiriki katika warsha ya Kitenge - Africa -
Volunteerism (KAV) iliyokuwa na lengo la kuhamasisha kazi za kujitolea
miongoni kwa vijana, wa kwanza katika mstari wa mbele ni Mkurugenzi
Msaidizi Maendeleo ya Vijana, Bi. Esther Liwa.
Warsha hiyo iliwakutanisha zaidi ya wanafunzi 100 wa vyuo vikuu
walishiriki katika tukio hilo, wakajifunza na kuoneshwa kufurahishwa na
kuhamasika na vijana wenzao wanaofanyakazi za kujitolea ambapo
iliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kujitolea (UNV) ikiwa na
lengo la kuhamasisha masuala ya kujitolea miongoni mwa vijana ambapo pia
ililihusisha shindano la vazi la kitenge na kujitolea (KAV), tukio hilo
ni kuhamasisha ili watu watambue kwamba suala la kujitolea ni sawa na
jambo la kila siku kama kuvaa vazi la kitenge.
Mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kujitolea
(UNV), (kulia) akitoa maelekezo kwa mmoja wa vijana aliyohudhuria katika
warsha ya Kitenge X Africa X Volunteerism (KAV) iliyokuwa na lengo la
kuhamasisha kazi ya kujitolea miongoni kwa vijana.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Vijana wa Shirika la Umoja wa Mataifa
(YUNA), Arafat Bakar akitoa maelezo kuhusu YUNA inavyofanya kazi kwa
jamii ya Tanzania na hususani vijana katika warsha ya Kitenge X Africa X
Volunteerism (KAV).
Mkurugenzi Mtendaji wa Young Tanzanian for Community Prosperty,
Alfred Magehema akitoa maelezo kuhusu taasisi yake na jinsi taasisi yake
inavyofanya kazi katika kuisaidia jamii.
Mmoja wa Maafisa wa Raleigh Tanzania, Rose Mmbaga akitoa ufafanuzi
kuhusu taasisi yao jinsi ilivyoanza, wanavyofanya kazi na mafanikio
waliyoyapata mpaka sasa.
Meneja wa Taasisi ya AIESEC Tanzania, Onome Ahorituwere akitoa
ufafanuzi kuhusu kazi zinazofanywa na taasisi hiyo katika warsha ya
Kitenge X Africa X Volunteerism (KAV).
Pichani juu na chini baadhi ya vijana walioshiriki katika warsha
ya Kitenge Africa Volunteerism (KAV) iliyokuwa na lengo la kuhamasisha
kazi za kujitolea miongoni mwa vijana hao.
Washiriki wa warsha ya Kitenge X Africa X Volunteerism (KAV), wakiwa katika picha ya pamoja.
No comments:
Post a Comment