Mkuu wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Peter Toima Kiroya kushoto akishiriki sherehe ya unywaji wa maziwa ikiwa ni mojawapo ya hatua ya makuzi kwa vijana mkoani Manyara hivi karibuni.
Na Lucy Ngowi.
KATIKA kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, watu mbalimbali wameendelea kujitokeza kwa ajili ya kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa siasa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Miongoni mwa watu hao yupo Mkuu wa Wilaya ya Kakonko iliyopo Kigoma, Toima Kiroye ni miongoni mwa watu waliotangaza nia ya kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Simanjiro, Arusha. Kiroye anasema anawania nafasi hiyo ya kuwa mbunge kwa kuwa alipokuwa katika wilaya moja ya nje na nyumbani yaani Simanjiro, alikuwa analinganisha utendaji wa serikali kule aliko, wilaya anazoziongoza na huko nyumbani alikotokea.
Uzeofu katika kazi nje na ndani ya wilaya hiyo umemwezesha kubainisha mambo mawili. Mosi katika utendaji na uwajibikaji wa watumishi wa serikali na katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo na matokeo yake. Sababu ya pili ni kiwango cha chini cha maendeleo katika jimbo la Simanjiro ikilinganishwa na maeneo ambayo ameongoza na amesimamia shughuli za maendeleo.
“Ninakosimamia wamekuwa wakitenda kazi za serikali na maendeleo yamekuwa bora zaidi tofauti na nyumbani kule ninakotoka. Ninakoongoza yako juu, nyumbani yako chini,” anasema Kiroye. Anatolea mfano wa wilaya ya Ukerewe ambako alikuwa mkuu wa mkoa, kwamba aliweza kufanya kazi ya ujenzi wa shule za sekondari za kata za wananchi karibu kila kata katika kipindi cha mwaka mmoja.
Pia katika wilaya ya Kakonko aliko sasa, katika kipindi kifupi tangu wilaya hiyo ianzishwe ambapo awali ilikuwa kama kijiji hivi sasa tayari ina msingi.
“Ina ofisi za kuanzia kazi, tumepata wawekezaji, tumevutia taasisi za fedha wameanzisha benki zao. Pia wananchi wameshiriki kwa hali na mali kujenga wilaya yao kwa kutoa michango yao, kwa kutoa matofali, mawe na mchanga. anasema kutokana na uongozi wake, wananchi wamekuwa wakijitolea kwa hali na mali nakutekeleza miradi ya maendeleo, ujenzi wa ofisi za kijiji, serikali, shule, zahanati na ujenzi wa visima vya maji,” anasema Kiroye.
Anatoa mfano wa ujenzi wa visima vitatu ambavyo vilijengwa bila msaada wa Serikali, pia wamejenga jengo la benki ambalo liko katika hatua za mwisho. Hali duni katika wilaya yake inampa msukumo wa kugombea ubunge ili aweze kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Vile vile anatoa mfano katika wilaya nyingine aliyoiongoza ya Ludewa mkoa wa Njombe ambako aliweza kufungua barabara na kusimamia vizuri ambayo ilitoka Ludewa mjini kwenda Lupingu, nyingine ilitoka Luganga mpaka Masimavalafu, hivyo alisimamia kuimarisha mawasiliano kwa njia ya barabara.
Anasema akichukua mifano hiyo anaamini kuwa kumbe uongozi ni kitu cha muhimu sana kwani unaweza kuleta mabadiliko kwa kutumia rasilimali zilizopo kugeuza hali ya maisha ya watu. “ Simanjiro ambako ni nyumbani kwangu , serikali inapeleka fedha za miradi ya maendeleo pamoja na wataalamu lakini hakuna mabadiliko..... hali za wananchi bado ni duni,” anasema.
Simanjiro kuwa rasilimali za kutosha kama madini kama tanzanite, wanyamapori, mifugo ya kutosha, ardhi ya kutosha, maji ya mto Pangani na upatikanaji wa maji ya ardhini lakini bado kuna shida ya maji na wananchi wanaishi maisha duni.
“Pamoja na utajiri huo Simanjiro imeendelea kuwa masikini na watu wameendelea kuwa duni sana. Ninaamini tukiwa na uongozi mzuri, bora wenye sifa zinazotakiwa katika uongozi, unaweza kutumia rasilimali hizo kuleta maendeleo na maisha ya watu yakawa bora,” anasema.
Anasema hali hiyo inasababishwa na uongozi mbaya hivyo akifanikiwa kuwa kiongozi atatumia rasilimali zilizopo wilaya humo na kuhamasisha wananchi kuharakisha maendeleo.
Anasisitiza kuwa, maendeleo duni yanasababishwa na kukosekana kwa uongozi bora unaoweza kudhibiti migogoro mingi inayoikumba wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na migogoro ya ardhi, mashamba, mifugo na kilimo, wanyamapori na kila eneo la matumizi ya ardhi lina mgogoro.
Kiroye anasema migogoro hiyo inakuzwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa, hivyo anatafuta nafasi ya kuongoza ili kumaliza migogoro yote na kurudisha hali ya amani. “Sisi tutakuwa ni watu wa mapambano milele. Nikaona hapo panataka muafaka. Hiyo hali inaleta uadui na uhasama miongoni mwao na kudhoofisha ule mwendelezo ama utaratibu mzima wa maisha ambao unakuwa wa kujenga,” anasema Kiroye.
Vile vile anasema katika wilaya hiyo kumetokea mpasuko wa miongoni mwa jamii kwa kuwa uongozi wa kisiasa umewagawa watu na kuleta matabaka.
Ni kama kwenye familia baba na mama wanagawa watoto hawapendani, wanachukiana, wanasemana kila siku. Kutokana na hali hii nikaona tunahitaji kiongozi ambaye atavunjavunja na kutupia mbali hali hiyo ni lazima kujenga upendo na maelewano, umoja na mawasiliano,” anaeleza Kiroye.
Mkuu huyo wa wilaya anasema tofauti na wilaya alizowahi kuziongoza ama anayoongoza hivi sasa hakuna mgogoro wa aina yoyote. “Kusema kweli nataka kwenda kuwa kiongozi ambaye ataunganisha watu na kuchochea mabadiliko ya fikra tofauti walizonazo ili kusudi wafanane na kuona ni wa moja wa kujenga sio kubomoa. Hivyo watu wa Simanjiro wanaona serikali haipo, wanajifanyia mambo yao wenyewe,” anasema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kiroye anasema, kitu kingine kinachomsukuma ni kwamba hivi sasa tupo kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa lakini kule Simanjiro ni kama huo mfumo haupo, kwani kuna chama kimoja tu cha Mapinduzi. “Chama hiki kikabadilika kikawa ni mali ya mtu na kikundi kidogo cha watu. Na wanachama wengine wanatumika kama chambo. Wamewekwa pembeni hawana maamuzi, hawasikilizwi na yeyote, kinachofanyika ni kile kilichoamriwa na watu wachache,” anasema.
Anaongeza kuwa, chama kimekuwa kikifanya maamuzi kwa maslahi binafsi sio ya wanachama. “Ninataka nikabadilishe huo mfumo, tukichukue chama chetu kutoka mikononi mwa mtu tuwarudishie wenyewe,” anasema. Pia anasema kwa watu wa Simanjiro kumekuwepo na usiri, kwani hawaambiwi ama kushirikishwa taratibu zozote za jinsi serikali yao inavyofanya kazi.
“Lazima tufike mahali tuwe wawazi. Hiki ni kitu kinatakiwa kibadilishwe. Hivyo hakujawahi kufanyika uchaguzi wa chama au serikali ya mitaa kihalali na haki,” anasema. Anahoji hivi makao makuu hayaoni mambo hayo? Kilio cha wanasimanjiro hakiwafikii? Anasema wana Simanjiro wanaona hakuna tofauti wanahoji hivi hii nchi imepata uhuru?
Hivyo kutokana na hali hiyo, anataka kuwa mbunge ili awakomboe wananchi waondokane na mambo hayo, wataondokana nayo kupitia uongozi bora. Hivyo anataka kuwa chanzo cha mabadiliko. Anasisitiza kuwa hata kama atachaguliwa mbunge mpya katika eneo hilo atakuwa anaanza kitu kipya kwa sababu kipindi chote hakuna kilichofanyika.
Kiongozi mpya ataanza kujenga misingi katika kila jambo. Kwa hiyo ubunge sio kitu cha kukimbilia katika jimbo hilo kwani ni kazi ngumu ila lazima ajaribu ili endapo atapata awe mkombozi wao. Akieleza historia yake kwa ufupi, Kiroye anasema ni mwana CCM na kwamba amekuwepo katika chama hicho tokea akiwa mwanafunzi wa sekondari miaka ya mwanzoni mwa 80.
Si hapo tu bali hata alipokuwa akisoma Chuo Kikuu alikuwa mwana CCM hai katika Umoja wa Vijana chuoni hapo, pia aliwahi kuwa katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM-UVCCM, chuoni hapo. Hivyo baada ya kumaliza masomo na kuanza kazi akawa anagombea uwakilishi kwenye chama katika ngazi mbalimbali.
Amewahi kuwa mjumbe katika Kamati ya Siasa Wilaya na Mjumbe Mkutano Mkuu wa Taifa. Anasema kutokea katika nyadhifa hizo ndipo alipopata uteuzi wa kufanya kazi anayoifanya sasa ambayo ni ya kada wa Chama Cha Mapinduzi ndani ya dola. Kiroye anasema aliteuliwa kushika nafasi ya ukuu wa wilaya tokea mwaka 2002 mpaka sasa.
Amehudumu na kutumikia nafasi hiyo katika wilaya mbalimbali nchini. Anasema kuwa ana elimu ya chuo kikuu. Ana shahada mbili. Ya kwanza ya elimu ya pili ni shahada ya uzamili katika sayansi ya jamii. Ameoa na ana watoto wanne. Wawili wa kike na wawili wa kiume.
No comments:
Post a Comment