Pages

May 9, 2015

JWTZ LAPOKEA TAARIFA ZA ASKARI WAWILI KUUAWAWA NA 16 KUJERUHIWA DRC CONGO.


Kaimu Msemaji wa jeshi hilo, Meja Joseph Masanja.

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limekiri kupokea taarifa za askari wawili waliouawa Mei 5, mwaka huu na wengine 16 kujeruhiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Waliuawa na kikundi cha waasi wa Allied Democratic Forces (ADF), wakiwa wanatekeleza jukumu lao la ulinzi wa amani. Askari hao wa Tanzania ni sehemu ya wapiganaji wa Kikosi Maalumu cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO), walioko kazini nchini DRC.

Kaimu Msemaji wa jeshi hilo, Meja Joseph Masanja alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Dar es Salaam.

Masanja alisema shambulizi hilo lilifanyika DRC Mei 5 saa 12:30 jioni, ambapo askari hao walikuwa miongoni mwa 46 waliokuwa katika jukumu hilo.

Alisema awali Watanzania hao walisafiri kwa ndege kutoka mji wa Abralose kuelekea katika mji wa Mavivi, baada ya kufika katika mji huo, msafara wao ulielekea katika mji wa Mayimayi kwa njia ya barabara wakitumia magari ya kijeshi.

“Wakiwa njiani kuelekea katika mji wa Mayimayi, ndipo msafara wao ulipovamiwa na kikundi kinachodhaniwa kuwa cha waasi wa ADF na magari waliyokuwa wakisafiria yalishambuliwa kwa silaha za kivita, ambapo gari moja liliteketezwa na kusababisha vifo vya askari wawili papo hapo na wengine 16 kujeruhiwa,” alisema Masanja.

Alisema majeruhi hao walipelekwa hospitali kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri. Kuhusu miili ya marehemu kurejeshwa nchini, alisema wanasubiri Umoja wa Mataifa (UN) kukamilisha taratibu zao kwanza.

Vifo vya wanajeshi hao wawili, kumefanya idadi ya wanajeshi wa Tanzania waliouawa miaka miwili iliyopita wakati wakilinda amani nchini DRC kufikia watano mpaka sasa.

Julai 2013 wanajeshi saba wa Tanzania waliokuwa wakilinda amani huko Sudan, waliuawa baada ya kushambuliwa na waasi, ambapo 17 walijeruhiwa vibaya.

Juzi ofisi ya UN nchini ilisema Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon, amelaani mauaji ya wanajeshi hao, pia ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na familia za wapiganaji hao mashujaa wa JWTZ.

Katika tukio hilo, wanajeshi wengine 13 wa DRC walijeruhiwa vibaya huku wanajeshi wengine wanne hawajulikani waliko. Tukio lilitokea mashariki mwa DRC, ambako majeshi ya Tanzania yapo kwenye vikosi vya Umoja wa Mataifa vya Kulinda.

Eneo hilo limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na waasi wa DRC. Shambulio hilo limekuja zikiwa ni siku chache baada ya helikopta iliyokuwa na sehemu ya wanajeshi wa MONUSCO kushambuliwa kwa risasi na wapiganaji wa waasi kutoka eneo hilo.HABARILEO

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...