Pages

February 3, 2015

WAZIRI MKUU AVUTIWA NA SHAMBA LA KAHAWA SONGEA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema amevutiwa sana na kazi iliyofanywa katika muda mfupi kwenye shamba la kahawa la Aviv lililoko kwenye kijiji cha Lipokela, wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma.

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba, eneo kubwa la shamba limepandwa miche ya kahawa na mingine imezaa na imeshavunwa ikilinganishwa na wakati alipofika shambani hapo Julai 2013 na kutembelea tu kitalu cha miche ya zao hilo. 

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Februari 2, 2015) wakati akizungumza na wafanyakazi na menejimenti ya shamba la Aviv baada ya kulitembelea na kukagua miundombuinu ya umwagiliaji wa matone ya maji kwenye shamba hilo.

“Mkuu wa shamba hili, Bw. Medu amenieleza kwamba mpaka sasa, wameshavuna kahawa mara moja na wanatarajia kuvuna tena hivi karibuni; lakini ili waweze kuanza kupata faida ni lazima wavune mara nne.”

“Kilimo kinataka uvumilivu na kinataka uwekezaji mkubwa... ni lazima kiwepo; hata kwa wakulima wadogo ni lazima kiwepo licha ya ugumu wake. Sasa ukisema kilimo ni kigumu na ukaacha kulima wakati una mke na watoto, je hao watakula wapi?”, alihoji. 

Aliwasifu wamiliki wa shamba hilo kwa kuchagua kulima zao la kahawa kwani lina walaji kila mahali ulimwenguni kote. “Wameamua kulima kahawa aina ya Arabica ambayo inakubalika duniani. Uhitaji wa kahawa hii upo kila mahali kwa sababu wanywaji wapo,” alisema.

Waziri Mkuu alisema pamoja na mafanikio hayo, shamba la Aviv linakabiliwa na changamoto ya nishati kwani linahitaji megawati 2.5 ili liweze kuendesha mitambo yake ambayo kwa sasa inatumia mafuta yanayoligharimu fedha nyingi.

Aliwataka wamiliki wa shamba hilo waendelee kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Mapema, akisoma risala ya kampuni ya Aviv, Mkuu wa shamba hilo ambaye pia anasimamia uzalishaji wa zao la kahawa Afrika Mashariki, Bw. Medu Medappa alisema hadi sasa wamekwishalima hekta 1,060 na zote zimekwishawekewa miundombinu ya umwagiliaji wa matone na kati ya hizo, hekta 810 zimekwishapandwa miche ya kahawa.

“Shamba letu lina ukubwa wa hekta 2,000 na hadi sasa tumeshalima hekta 1,060 na zilizobakia ni kwa ajili ya kutunza mazingira na uoto wa asili kwenye vilima vinavyotuzunguka,” alisema.

Alisema hadi sasa wamekwishaajiri wafanyakazi 1,500 kwenye shamba hilo na kutoa mafunzo kwa wakulima wanaoishi vijiji vya jirani. “Pia tumewapatia miche ya bure kaya 673 na kutokana na mafunzo tunayowapa, wanavijiji wameweza kulima kahawa inayoendana na viwango vya kimataifa vya uzalishaji kahawa ambavyo ni miezi 22,” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu akijibu moja ya hoja kwenye risala ya Bw. Medappa iliyohusu eneo la hekta tisa kuchukuliwa na Wakala wa Ujenzi wa Barabara (TANROADS), alisema eneo hilo ni muhimu kwa ujenzi wa barabara za mkoa huo kama ambavyo shamba hilo ni muhimu kwa mkoa huo.

“Lile eneo limetengwa na TANROADS kwa ajili ya kutengeneza kokoto za ujenzi wa barabara. Barabara za lami tunazitaka. Tunahitaji kazi hii iendelee la sivyo barabara zetu zitakufa,” alisema.

Alisema watu wa TANROADS wakimaliza kazi yao, lile eneo litabaki tupu na mwekezaji huyo anaweza kulitumia kadri atakavyoona inafaa kwa sababu liko ndani ya eneo lake.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...