Baadhi ya bidhaa zilizoteketezwa na Maofisa wakaguzi wa TFDA wilayani Sikonge.
Maofisa
wakaguzi wa TFDA kanda ya kati wakijiandaa kuteketeza bidhaa zilizoisha
mda wake ikiwemo vinywaji wilayani Sikonge (picha na Allan Ntana).
Na Allan Ntana, Sikonge
MAMLAKA
ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kati imefanikiwa kukamata na
kuteketeza bidhaa mbalimbali za chakula, vinywaji, dawa za binadamu na
mifugo, vipodozi na vifaa tiba vilivyoisha muda wake na vingine feki
vyenye thamani ya zaidi ya sh mil.5 katika halmashauri ya wilaya ya
Sikonge mkoani Tabora.
Akisoma
taarifa ya ukaguzi mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo hapo juzi
Afisa Mkaguzi wa Chakula Kanda ya Kati Sifa Chamgenzi alisema ukaguzi
huo ulilenga kuangalia ubora na usalama wa dawa za binadamu na mifugo,
uwepo wa vipodozi vilivyopigwa marufuku na bidhaa zingine zilizoisha
muda wake wa matumizi.
Alisema
lengo la TFDA ni kufuatilia utekelezaji wa sheria na.1 ya mwaka 2003 ya
chakula, dawa na vipodozi kwa wauzaji na wasindikaji wa vyakula na dawa
na kuongeza kuwa zoezi hili lililenga kutekeleza mpango kazi wa Mamlaka
hiyo wa kufuatilia ubora na usalama wa bidhaa hizo kwa mtumiaji.
Ukaguzi
huo uliofanyika tarehe 20-29 Januari 2015 uliongozwa na Maafisa
wakaguzi wawili kutoka TFDA Kanda ya Kati Fredrick Luyangi na Sifa
Chamgenzi ambao waliungana na wakaguzi wenyeji wawili toka Ofisi ya
Mkurugenzi Idara ya Afya na askari polisi wanne wilayani Sikonge na
jumla ya majengo 118 yanayojihusisha na biashara ya chakula, vinywaji,
dawa, vipodozi na vifaatiba yalikaguliwa.
Katika
ukaguzi huo baadhi ya maduka yalikamatwa na vipodozi vilivyopigwa
marufuku vikiwa na uzito wa kilo 164.4 na thamani ya sh 1,856,000/- na
katika maduka ya vyakula walikamata vyakula vilivyoisha muda wake vyenye
uzito wa kilo 825.5 vikiwa na thamani ya sh 2,720,000/-
Na
katika maduka ya dawa za binadamu na mifugo walikamata jumla ya kilo 37
za dawa zilizoisha mda wake na feki zenye thamani ya sh 1,200,000/-.
Aidha
katika ukaguzi huo kiasi cha sh 1,580,000 kilipatikana kutokana na ada
za usajili wa maduka ya biashara ya chakula ambapo 40% ya kiasi hicho
sawa na sh 632,000 inabakia katika halmashauri kwa ajili ya kufanya kazi
za TFDA.
Akizungumzia
mambo waliyoyabaini wakati wa ukaguzi huo, Chamgenzi alisema ukaidi na
uelewa mdogo wa sheria na.1 ya mwaka 2003 wa kulipa ada na tozo husika
kwa baadhi ya wafanyabiashara wa maduka ya chakula, dawa na vipodozi
bado ni tatizo sambamba na kutotoa ushirikiano kwa Afisa wakaguzi.
Aidha
uwepo wa dawa bandia (feki) zilizoondolewa sokoni, dawa na vyakula
vilivyoisha muda wake, kukosekana feni za kutunzia dawa katika stoo ya
kituo cha afya Kitunda, maduka ya dawa za kilimo kuuza dawa za mifugo
kinyume cha sheria, utunzaji mbovu na mlundikano wa dawa zilizoisha muda
wake, viwanda na mashine za unga kuwa katika makazi ya watu ni miongoni
mwa yaliyobainika.
Wakaguzi
hao pia hawakuridhishwa na hali ya machinjio ya halmashauri hiyo kukosa
uzio, kutokuwa na chanzo cha maji cha kuaminika na sakafu kuwa na
mashimomashimo hali iliyosababisha kutuama kwa maji na damu na hivyo
kuhatarisha afya za walaji, hivyo wakamwagiza mkurugenzi wa halmashauri
hiyo Shadrack Mhagama kufanyia kazi mapungufu hayo kwani yanarekebika,
jambo ambalo aliliafiki na kuahidi kutekeleza mara moja.
No comments:
Post a Comment