Dirisha la usajili katika ligi ya Tanzania linatarajiwa kufungulia
hivi karibu, na baadhi ya vilabu vimeanza harakati za kuimarisha vikosi
vyao.
Wakati kukiwa na taarifa kwamba klabu ya Yanga imemtema mshambuliaji
Jaja kutoka Brazil, leo hii klabu hiyo imesema kwamba kiungo mkabaji
raia wa Brazil Emerson De Oliveira Neves Rouqe anatarajiwa kuwasili siku
ya jumanne mchana jijini Dar es salaam kwa ajili ya majaribio katika
klabu ya Young Africans na endapo atafuzu moja kwa moja atajiunga na
mabingwa mara 24 wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Emerson mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anachezea timu ya
Bonsucesso FC iliyopo ligi daraja la pili nchini kwao Brazil, msimu
uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Poland katika timu ya
Piotrkow Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili nchini humo.
Ujio wa Emerson kuja kufanya majaribio nchini unakuja kufuatia
mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil pia Geilson Santos “Jaja”
kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda kwao Brazil na kutoa taarifa
kwamba hataweza kurejea tena nchini kutokana kukabiliwa na matatizo ya
kifamilia.
Awali ilikua familia ya Jaja ije nchini katika kipindi cha mapumziko,
lakini waliomba yeye Jaja ndio aende Brazil na mara baada ya kufika
huko matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo yamepelekea kushindwa
kurejea nchini kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao kwa ajili ya
kutatua matatizo hayo.
Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Young Africans kubakia na
wachezaji wanne tu wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima,
Hamis Kizza na Andrey Coutinho hivyo endapo Emerson atafuzu atakua
anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kimataifa
Endapo Emerson atafuzu majaribo pamoja na vipimo atajiunga na kikosi
cha kocha mbrazil Marcio Maximo katika nafasi ya kiungo mkabaji ikiwa ni
sehemu ya kuboresha timu kuelekea kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom
pamoja na mashindano ya kimataifa.
Aidha kikosi cha Young African baada ya kuwa mapumzikoni kwa
takribani wiki mbili, kinatarajiwa kuanza mazoezi siku ya jumatatu
katika Uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo wa Nani
Mtani Jembe pamoja na mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
bara.
No comments:
Post a Comment