BAADA ya
matukio ya harusi ya Jumamosi iliyopita natoa onyo ole wake
atakayeniomba mchango wa harusi, sitaki utani. Labda kwanza nikueleze
jinsi tulivyopata misukosuko sana kwenye uchangiaji wa ile harusi, maana
siku hizi hakuna pa kukimbilia, kila asubuhi unaamshwa saa kumi na
mbili na meseji kwenye simu;
“Ndugu
rafiki na jamaa wa familia ya Pingapinga inakukumbusha kuwa harusi ya
mtoto wao imekaribia hivyo mchango wako unahitajika”, baada ya wiki
meseji huwa kali zaidi;“Siku zinaisha kwa nini hautoi mchango, unajua
familia ya Pingapinga ina shughuli ya harusi ya mtoto wao, toa upesi au
la usitulaumu.”
Basi
hizi meseji zilikuwa nyingi kuliko zile za kampuni yangu ya simu
inayobuni namna ya kunitoa mkwanja kila wiki. Hatimaye nikatoa faini,
maana nisiite mchango, maana mchango haulazimishwi.
Sasa
Jumamosi ndiyo ikawa siku ya harusi, kadi nililetewa mapema ,
nikahakikisha koti langu la kuendea harusini nalicheki vizuri, maana
haya makoti yanayokaa kabatini miezi ni muhimu kucheki vizuri maana
unaweza kukuta panya kazalia kwenye mfuko halafu wakatimka kutoka
kwenye makazi yao wakati uko katikati ya kucheza mduara wa harusi.
Kweli
tukaingia ukumbini viti vilikuweko swafi, meza zimepambwa kwa maua na
MC alitukaribisha kwa maneno mengi yaliyojaa vichekesho visivyochekesha,
au vichekesho vingine vimesharudiwa na kila MC hapa mjini halafu akawa
analazimisha watu wapige vigelegele!
Yote
bure watu walikuwa wamenuna maana hakukuwepo na dalili ya hata chupa
moja ya kinywaji, ila ahadi kibao zikawa zinatolewa na MC, mara ‘Roli la
bia linakuja toka breweries, mara shampeni leo inatoka Ufaransa kwa
helikopta.”
Ghafla
wahudumu waliovalia vikofia kichwani wakapitisha sambusa mojamoja kwa
kila mtu, wakisindikizwa na MC akituhamasisha tule tufurahi na bwana
harusi. Kwa kweli hela yangu ikaanza kuniuma, kwanza nililazimishwa
kulipa, halafu sioni chochote hawa jamaa vipi?
Wakati
ukumbi mzima ukiwa umeendelea kununa utadhani kikao cha msiba, MC
akatuambia eti bwana harusi ana machache kabla ya kutuaga kwenda
kupumzika na mkewe. Pamoja na kisirani tulikuwa na hamu kumsikia mshenzi
huyu anataka kusema nini.
Bwana
harusi akasimama hata suti aliyovaa ilikuwa haijamkaa sawasawa, akakohoa
kidogo akaanza, “Asante MC, kwanza naomba nimshukuru Mungu kwa kumuumba
mke wangu, kwa hilo Mungu uko juu, kiukweli hapa nimepata mke mtulivu,
mpole asiye na makeke, yaani najisikia nina bahati sana.
“Naomba
niwashukuru wakwe zangu kwa kukubali kupokea robo tu ya mahari na
kuruhusu ndoa hii ifanyike. Pia nishukuru kwa zawadi zao za kitanda,
godoro, kabati na makochi asante sana. Naomba nimshukuru baba mwenye
nyumba wangu kwa kukubali niwe na deni la kodi ya mwaka ili kufanikisha
harusi hii, mzee upo juu.
“Naomba
nitoe shukrani kwa bosi wangu kwa kunipa likizo fupi ili nikamilishe
shughuli hii, pia wafanyakazi wenzangu kwa zawadi yenu ya jiko la gesi.
Namshukuru mke wa kaka yangu kwa kutuazima gauni la harusi, na kaka
yangu kwa suti hii niliyovaa. Natoa shukrani kwa mtengeneza keki,
nitairudisha keki kwako kesho kama tulivyokubaliana.
“Nawashukuru
wazazi wangu kwa kuja na kikundi cha ngoma toka kijijini, kweli
kimeziba pengo la burudani katika harusi hii. Naishukuru kamati ya wazee
wa kanisa kwa kufanikisha kumshawishi mke wangu aolewe na mimi, niwape
aksante kwa akina mama jirani kwa kuja na sambusa mlizokula toka makwao
ili kufanikisha harusi hii, mradi harusi hii ni furaha tupu. “MC wewe ni
rafiki yangu nashukuru kwa kukubali tulipane kidogokidogo aksante
sanaaaaa!
No comments:
Post a Comment