Polisi
jijini Dar es Salaam wamelazimika kutumia mabomu kulitawanya kundi la
vijana zaidi ya 300 wanaojiita 'Mbwa Mwitu' lililokuwa limewavamia
wananchi na kupora mali kwenye nyumba na maduka.
Wakizungumza
na gazeti hili, wakazi wa Mtaa wa Kigogo Mkwajuni, wilayani Kinondoni
ambapo vurugu hizo zilitokea, walisema kuwa vijana kadhaa walifika
mtaani hapo juzi Alhamisi saa 9:00 alasiri na kudai kuwa walipewa kibali
cha kupiga muziki wa mnanda katika Barabara ya Mwembejando.
Muda mfupi
baada ya kuanza kuimba na kucheza muziki, kundi hilo lilifunga barabara
ya mtaa huo, huku vijana wengine kutoka sehemu mbalimbali za wilaya hiyo
wakizidi kuelekea katika eneo hilo.
"Kwa mara
ya kwanza jana (juzi) niliona watu wanne wamepakizana kwenye bodaboda,
wote walikuwa wanafuata mnanda. Sijui huo muziki una nini ukipigwa
unakusanya sana watu," alisema Mjumbe wa Serikali ya Mtaa, Ramadhan
Liganduka.
Akizungumza
kwenye ofisi ya Serikali ya Mtaa, mjumbe huyo alisema kuwa alishtushwa
na kundi la vijana lililokuwa likiingia mtaani kwake kwenda kwenye
muziki wa mnanda ambao umepigwa marufuku, ndipo alipompigia simu Ofisa
Mtendaji wa mtaa huo, Magreth Mpinge.
"Nilimpigia
simu nikwamwambia ninasikia mnanda unapigwa, hali siyo salama huko.
Niliwapigia simu hata majirani na wapangaji wangu nikawaambia hali siyo
nzuri wasijiamini sana, huo muziki huwa unaambatana na fujo," alisema.
Alisema
baada ya kupigiwa simu, Polisi walifika katika eneo hilo saa 2:15 usiku
wakati huo tayari vijana hao walikuwa wameshaanza kupora mali kwenye
maduka na kwa wapita njia.
Mmoja wa
wakazi walioshuhudia tukio hilo, Humphrey Massawe alisema kuwa wakati
muziki ukiendelea baadhi ya vijana walikuwa wakitumia nafasi hiyo kupora
simu za watu waliokuwa wanakwenda kucheza muziki, jambo
lililowalazimisha watu kuanza kufunga maduka kwa hofu.
"Jana
(juzi) hapa ilikuwa kama Sudan, watu walituvamia wengi kama 300 hivi,
sura zao ni ngeni walikuwa wanapora mali kwenye maduka.
"Mimi
niliambiwa na mwenzangu kuwa watu wanavamia maduka huko chini, kwa hiyo
nifunge duka langu, lakini niliogopa kutoka nje nifunge kwa sababu
milango inafungwa kwa nje," alisema Massawe.
Aliongeza
kuwa polisi walipofika katika eneo hilo walichukua vyombo vyote vya
muziki na kuondoka navyo, pia waliwakamata baadhi ya wakazi mtaani hapo.
Mtendaji wa mtaa huo, Magreth alisema kuwa hakuna mwenyeji
aliyejeruhiwa, lakini kijana mmoja anayedhaniwa kuwa ni mmoja wa vijana
hao alipigwa na kuumizwa wakati wa purukushani hizo.
"Ni
mapema mno kujua jina la huyo kijana na sehemu alikotoka, ndiyo kwanza
tunaendelea kufuatilia. Wale huwa hawaendi hospitali, waende huko
wakakamatwe?" alihoji.
Magreth alisema kuwa watu kadhaa wanashikiliwa na Polisi wakiwamo waliotoa umeme utumike kupiga muziki, ambao haukuwa na kibali.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera
Senso, alisema vimeibuka vikundi mbalimbali vya vijana jijini Dar es
Salaam vinavyojulikana kama Mbwa Mwitu, Watoto wa Mbwa au Panya Road,
ambavyo vimekuwa vikijihusisha na uporaji, unyang'anyi wa kutumia nguvu
na kujeruhi watu.
Senso
alisema, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Abdulrahman Kaniki
amewaagiza makamanda hususan wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
kuhakikisha wanavitafuta vikundi hivyo popote vilipo, kuwakamata na
kuwafisha katika vyombo vya sheria.
"Naibu
IGP amekemea vikali vikundi hivyo na kuvitaka kuacha tabia hiyo mara
moja, kwani vitendo hivyo ni vya kihalifu na vinatakiwa kukemewa na kila
mtu katika jamii.
"Aidha,
amewataka wananchi kuondoa hofu na badala yake watoe ushirikiano kwa
kutoa taarifa za vikundi hivyo katika vituo vya Polisi ili zichukuliwe
hatua za haraka," alisema.
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment