Baadhi ya Madiwani wa halmashauri ya Jiji la Arusha kupitia Chadema wakizungumza na wananchi hivi karibuni. |
Arusha. Hatimaye Jeshi la Polisi wilayani Arusha
limeruhusu mikutano ya hadhara ya Mbunge wa Arusha (Chadema), Godbless Lema
baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo kuingilia kati.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Arusha, Lebaratus Sabas alithibitisha jana kuruhusiwa kwa mikutano hiyo
licha ya kuizuia awali baada ya kujiridhisha na hali ya kiusalama.
Uamuzi wa polisi
unakuja baada ya Lema kushikilia msimamo wa kuendelea na mikutano akisema
sababu zilizotolewa na polisi hazikuwa na mashiko.
Polisi ilizuia
mikutano ya Lema aliyetoa taarifa Aprili 17, mwaka huu, baada ya CCM kuomba
kufanya mikutano siku mbili baada ya taarifa yake, ikitaja siku na maeneo
hayohayo ya mbunge huyo.
Awali, Mkuu wa Polisi
Wilaya (OCD) Arusha, Giles Muroto aliyezuia mikutano hiyo, pia alitaja hofu ya
mlipuko wa bomu kama sababu nyingine ya kuzuia mikutano ya Lema.
Jana asubuhi, Mkuu wa
Mkoa wa Arusha alikaririwa na kituo cha Radio 5 cha Arusha akiliagiza jeshi la
polisi kutathmini hali ya usalama na kumruhusu Lema kutimiza wajibu wake wa
kibunge kwa kukutana na wapiga kura wake kupitia mikutano ya hadhara.
“Pamoja na polisi
kutaja sababu za kuzuia mikutano ya hadhara Arusha, tutawashauri , wafanye
tathmini kuruhusu mikutano ya mbunge ili atimize wajibu wake wa kibunge,”
alikaririwa Mulongo.
Hata hivyo, Mulongo alikiri Jiji la Arusha
kuwa katika hali tete na hofu kutokana na tukio la mlipuko wa bomu kwenye Baa
ya Arusha Night Park, Aprili 13, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment