Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole (katikati) akizungumza katika mkutano wa utekelezaji wa ilani ya chama hicho Kata ya Monduli Mjini ambapo alionya watu kuacha kumfuatafuata Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa. Kulia ni katibu wa Uenezi Mkoa, Isack Joseph na kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Reuben Ole Koney. Picha na Mussa Juma
Arusha. Mpasuko ndani ya CCM unazidi kuongezeka baada ya viongozi wa chama hicho Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Monduli kuibuka na kukemea ‘siasa za vitisho na hofu’ dhidi ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole, akiambatana na Mwenyekiti wa Wilaya ya Monduli, Reuben Ole Kuney na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Isaack Joseph alieleza kuchoshwa na kauli za vitisho dhidi ya Lowassa zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa chama hicho, wakati wanachama wote ni sawa na hakuna mwenye ukubwa mithili ya tembo wa kumtisha mwenzake.
Kauli ya kiongozi huyo, imekuja siku mbili baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kukemea vitendo vya rushwa kwa watu wanaotaka kuwania urais na kuiagiza Kamati ya Maadili ya chama hicho inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula kuwashughulikia.
Akizungumza katika mkutano wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi katika Kata ya Monduli Mjini ambao pia ulienda sambamba na maadhimisho ya miaka 37 ya CCM, Nangole alisema wanachama wote wa CCM wana haki sawa na hakuna wa kuogopwa kama tembo, wala mdogo wa kunyanyaswa kama sisimizi, ili mradi hakuna ambaye anavunja sheria na taratibu za chama hicho.
“CCM ni yetu sote, hakuna mtu wa kuogopwa kama tembo wala sisimizi, mimi binafsi sijaona kosa alilofanya Lowassa hadi sasa. Kwa nini wanamfuatafuata na kumshambulia kupitia vyombo vya habari?” alihoji Nangole.
Alisema anawashangaa baadhi ya viongozi kuanza kutoa kauli za kumshambulia Lowassa na kumtishia kumpeleka katika Kamati ya Maadili ya chama hicho kwa tuhuma kuwa, ameanza kampeni za urais, jambo ambalo sio kweli, kwani tangu mwaka 1993 amekuwa akiendesha harambee mbalimbali na amekuwa akifanya sherehe kila mwaka nyumbani kwake.
“Nakumbuka Rais Jakaya Kikwete mwenyewe alihudhuria sherehe nyumbani kwa Lowassa mwaka 2006 na alimpongeza kwa sherehe hiyo kwa kuwaalika marafiki zake wengi na kupokea mwaka mpya, lakini nashangaa sasa sherehe yake kuwa nongwa,” alisema Nangole.
Alisema anaamini kuna ajenda ya siri dhidi ya Lowassa, kwani hata makada wengine wa chama hicho wameonyesha nia ya kuwania urais, lakini hakuna ambaye anawasema.
“Kwani hatujuani? Tunajuana, wapo wanaopita wanasema hawajaoteshwa wanangoja kuoteshwa, wengine wanasema afya zao nzuri na wanaweza kuongoza miaka mitano, wengine wamesambaza kalenda nchi nzima na wengine wanapigiwa kampeni na viongozi wa juu wa chama, lakini hakuna anayesemwa zaidi ya Lowassa,” alisema Nangole.
Nangole alisema wao wanajua taratibu za chama, hivyo hawawezi sasa kuanza kampeni kabla ya muda mwafaka.
Alisema Tanzania ni ya watu wote na waliongia CCM ni kutokana na kuwa na imani ya chama hicho, hivyo hakuna sababu za ubabe na baadhi kujiona bora zaidi ya wengine.
Alisema Lowassa tangu mwaka 1993/4 alipokuwa waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, alianza utaratibu wa harambee kusaidia wazazi waliokuwa na watoto wanaokosa nafasi ya shule na kuanzisha mifuko na alikuwa akienda kanisani na misikitini, iweje leo iwe nongwa?
“Mungu amempa uwezo akisimama watu humfuata nyuma katika kusaidia wanyonge, yeye ana nguvu za Mungu, nadhani hiyo ndiyo inamletea taabu. Sasa mimi niulize kuna kamati za maadili sawa, tangu mwaka 1993 ameanza harambee leo wanasema ameanza kampeni?” alihoji Nangole.
Alisema Lowassa amekuwa akisaidia kila pembe ya nchi katika nyumba za ibada na hafanyi kampeni, kwani hao wanaosaidiwa siyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM.
Amshambulia Malecela
Alisema anamheshimu sana Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, John Malecela na alidhani angetumia busara zake kumsaidia Rais Kikwete ili kukabiliana na matatizo ya kijamii kuliko kuibua suala la fulana za kuashiria Lowassa ameanza kampeni.
“Tuna matatizo ya ajira, elimu, afya, ajali, rais anahangaika usiku na mchana, ningedhani huyu mzee mwenye umri mkubwa ameongoza nchi kama Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa CCM, angemshauri Rais kwani tuna matatizo mengi kuliko fulana. Mimi nadhani busara zake zingesaidia taifa kuliko fulana ambazo hata wanamichezo wanapewa. Nimesikitika sana,” alisema Nangole.
Nangole amekuwa mwenyekiti wa tatu wa CCM mkoa kujitokeza hadharani na kutoa matamshi ya kutetea kinachoelezwa kama mienendo ya Lowassa.
Wengine ni Khamis Mgeja wa Shinyanga na Mgana Msindai wa Singida wanaoungana na wabunge, John Komba wa Mbinga Magharibi na Beatrice Shellukindo wa Jimbo la Kilindi.
Lowassa asiwe na hofu
Kwa upande wake ole Kuney alisema anashangaa watu wanaomshambulia Lowassa bila sababu za msingi hasa kuhusiana na mbio za urais ambazo hata hajatangaza.
“Mbona watu wengi wanasema wanataka kugombea na wanajulikana, mbona hawasemwi. Tunamwomba Lowassa asiwe na hofu awapuuze hawa watu, wanatapatapa kama wafamaji,” alisema Ole Kuney.
Alisema lazima ijulikane Lowassa ana watu, ana marafiki wa kila aina, kwa hiyo akizunguka na wajasiriamali hakuna tatizo.Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment