Akizungumza juzi katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, Lissu alisema chama kitaendelea kushusha mjeledi kwa wanachama na viongozi wake watakaobainika kwenda kinyume na maadili na katiba ya chama.
Lissu ambaye alikuwa akielezea uamuzi uliochukuliwa dhidi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, alisema Chadema ni chama cha siasa na siyo taasisi binafsi, hivyo ni lazima katiba yake iheshimiwe.
“Chadema ni chama cha siasa na siyo taasisi binafsi, na kwa kuwa sisi ni chama cha siasa, tuna katiba, tuna kanuni, miongozo na kuna vikao halali,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa lengo la chama ni kusimamia maadili ya chama ili isije ikajengeka tabia kwamba kuna baadhi ya watu ambao wako juu ya chama na hata wakifanya kosa lolote wanachukuliwa hatua.
“Lazima chama kiwe kikali kuhakikisha hakuna mtu ambaye anakuwa mkubwa kuliko chama, kwani tukishindwa kusimamia hilo itakuwa siyo chama cha siasa,” alisema.
Lissu alisema uamuzi uliochukuliwa dhidi ya Zitto na wenzake ulifikiwa baada ya kuonyana na kurekebishana ndani ya chama kushindikana na hivyo hatua iliyobakia ni kuchukua maamuzi magumu.
“Hadi tumefikia hatua hiyo tumekanyana, tumerekebishana na kuonyana ndani ya chama, lakini wapo baadhi ya watu wanajiona ni wakubwa kuliko chama, wanajiona wao ndio chama sasa ikifika hapo lazima chama kiangushe mjeledi,” alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment