- Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana ofisini kwake kuwa maandamano yaliyopangwa kufanywa na Chadema leo yamepigwa marufuku kwa maelezo kuwa madai yao bado yanashughulikiwa.
Arusha. Jeshi la Polisi mkoani
Arusha linamtafuta Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na watu
wengine watatu ili kuhojiwa kuhusu malalamiko ya vurugu zilizotokea
kwenye mikutano ya kampeni za uchaguzi wa kiti cha udiwani Kata ya
Sombetini wiki iliyopita ambapo watu kadhaa walijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alisema jana ofisini kwake kuwa maandamano yaliyopangwa kufanywa na
Chadema leo yamepigwa marufuku kwa maelezo kuwa madai yao bado
yanashughulikiwa.
Kamanda Sabas aliwataja baadhi ya wanachama kuwa
wanatafutwa kwa ajili ya mahojiano kuwa ni Anold Kamde na wengine
akiwataja kwa jina moja moja ambao ni Frank na Daudi.
“Nimepiga marufuku maandamano kwa vyama vyote,
tunataka mji wa Arusha uwe na utulivu ili wanaofanya kampeni waendelee
na wanaofanya kazi wasibughudhiwe. Ninamtaka Lema afike kwa Kamanda wa
Upelelezi wilaya ahojiwe,” alisema Sabas
Kwa upande wake, Godbless Lema alisema kuwa hana
taarifa ya kutafutwa polisi kwa ajili ya mahojiano na kama anahitajika
basi utaratibu ufatwe wa ili aweze kuhojiwa.
“Ninachofahamu ni wanachama wetu watatu ambao
Ofisi ya Kamanda wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha ilinitaka niwape
taarifa zao kuwa walikuwa wanahitajika kwa mahojiano,” alisema Lema
Chadema wilaya ya Arusha ilipanga kufanya
maandamano wakitaka polisi iwakamate watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM
wanaofanyia vurugu na kuwaumiza wanachama wao kwenye mikutano yao ya
kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Sombetini.
Hata hivyo, Lema alisema baada ya mashauriano na
Polisi, wamesogeza mbele hadi kesho Alhamisi kwa kuwa baada ya
kuwasilisha barua yao ilibainika kuwa CCM nao waliomba kufanya maandano
yao leo Jumatano. Kamanda Sabas alisema wanachama kadhaa wa CCM
wanaolalamikiwa na Chadema kuhusu vurugu hizo wameshahojiwa na
wanahitaji kuwahoji wanachama watatu wa Chadema pamoja na Lema kutokana
na malalamiko ya wafuasi wa CCM ambao wanadai kufanyiwa fujo na wafuasi
wa Chadema.Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment