Kwa ufupi
Awali, wafuasi hao walifika mapema asubuhi katika viwanja vya Mahakama tayari kusikiliza uamuzi huo.
Dar es Salaam.Wafuasi wa
Chadema wanaomuunga mkono aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho,
Zitto Kabwe na wanaounga mkono uongozi wa juu, jana walitwangana tena
muda mfupi baada ya kuondoka eneo la Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es
Salaam.
Tukio hilo limetokea huku Mahakama hiyo
ikiahirisha hadi leo, kutoa uamuzi wa maombi ya Zitto kuzuia kujadiliwa
na Kamati Kuu ya Chadema.
Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014, Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, anaiomba Mahakama iizuie
Kamati Kuu ya Chadema kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu
uanachama wake hadi kesi yake ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Uamuzi wa maombi hayo ulipangwa kutolewa jana na
Jaji John Utamwa ambaye hata hivyo, alisema alikuwa hajamaliza kuandika
uamuzi huo na kuahirisha shauri hilo hadi leo mchana.
Maombi hayo ya Zitto ya zuio la muda la kujadiliwa
na kuchukuliwa uamuzi wowote kuhusu uanachama wake yametokana na kesi
ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya
Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Katika kesi hiyo, Zitto pia anaiomba Mahakama Kuu
imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za kikao cha
Kamati Kuu za kumvua nyadhifa zake zote alizokuwa nazo ndani ya chama
na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake
ya ubunge wa Kigoma Kaskazini.
Mapigano
Baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, wanachama wa
makundi yote waliondoka eneo la Mahakama wakiendelea kuimba na
kushangilia lakini walipofika eneo la Mahakama ya Rufani ghafla walianza
kupigana ngumi na mawe. Baadhi yao walikamatwa na askari kutokana na
vurugu hizo.
Awali, wafuasi hao walifika mapema asubuhi katika viwanja vya Mahakama tayari kusikiliza uamuzi huo.
Ulinzi ulikuwa umeimarishwa na askari polisi
wakiwamo wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliokuwa na silaha
pamoja na mabomu ya machozi walikuwa wametanda.
Pia kulikuwa na askari wa Kikosi cha Mbwa pamoja na gari la maji ya kuwasha.
Licha ya kuwahi, ni wafuasi wachache walioruhusiwa
kuingia ndani ya u`kumbi wa Mahakama tena baada ya kuandikisha majina
yao huku wakitambuliwa na viongozi wao waliokuwapo.
Baada ya idadi iliyokuwa ikihitajika kutimia, wafuasi wengine waliambiwa
wasubiri kutapata taarifa za uamuzi huo baadaye.
Wakiwa wanasubiri, walikuwa wakitambiana kwa maneno na nyimbo.
Kundi la Zitto lilikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kumsifu na
bendera za chama hicho pamoja na ngoma huku likikejeli kundi linalounga mkono
uongozi wa chama hicho.
Baadhi ya mabango yalisomeka ‘Zitto kama Mandela’, ‘Zitto
Mkombozi.’
Baadhi ya maneno waliyokuwa wakiyatamka katika nyimbo zao ni pamoja na `Zitto
Kwanza’, chama (Chadema) baadaye.
Wafuasi wa uongozi nao walikuwa na mabango yaliyosomeka: ‘Hongera Mbowe kwa
ujasiri,’ ‘Kunguru hafugiki’ na ‘Zitto rudisha kadi yetu’.
Awali, kundi linalounga mkono uongozi lilidai kwamba wanaomuunga mkono Zitto
si wanachama halali wa chama hicho, bali wamenunuliwa kwa lengo la kwenda
mahakamani.
Tofauti na siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa maombi ya Zitto, ambayo kundi
linalounga mkono uongozi lilidai kuwa wafuasi wa Zitto wameandaliwa na CCM, jana
liliwatuhumu kuwa wameandaliwa na CUF.
Baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), walisikika
wakilalamika kwa askari kuwa wafuasi hao wametoka mitaani na wengine ni wa
CUF.
CUF wakana tuhuma
Hata hivyo, CUF jana kimekana kuhusika na mgogoro huo unaoendelea Chadema.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Julius Mtatiro alisema jana kuwa kuna taarifa
zimesambaa kuwa CUF kilikuwa kimeandaa vijana wa kwenda mahakamani jana kwa
ajili ya kufanya vurugu.
“Wadau, waandishi wengi wa habari walinipigia nithibitishe ikiwa CUF iliandaa
makundi ya wanachama wakamshabikie ZZK (Zitto) mahakamani leo (jana) hii.
Taarifa ya namna hii pia imeenea mitandaoni.
“Pia viongozi kadhaa wa Chadema wamenipigia kunijulisha kuwa intelijensia yao
imegundua kuwa vijana wa CUF wamepenyezwa na kwamba wamevishwa T-shirt (fulana
za M4C na mapanga,” alisema Mtatiro na kusisitiza kuwa CUF hakijapanga wala
kutuma makundi ya vijana kwenda kumshabikia Zitto.
Alisema ikiwa wanachama wa CUF wameonekana mahakamani itakuwa ni kwa utashi
na matakwa yao.
“Hatujawahi kukutana, kupanga wala kutuma vijana wa CUF wakasimamie upande
wowote katika mgogoro huu.
Wakati wa fukuto la Hamad Rashid na CUF watu wengi tu raia walifika
mahakamani, hatukuhoji na kutafuta vyama vyao, tuliamini ni Watanzania tu,”
alisema Mtatiro na kuongeza:
“Ni vigumu kwa CUF kukataza wanachama wake wasihudhurie kesi maarufu kama ile
ya Babu Seya, Sheikh Ponda, Zitto Kabwe, Samaki wa Magufuli na
nyinginezo.”
Chanzo.Mwananchi
Chanzo.Mwananchi
No comments:
Post a Comment