Pages

January 16, 2014

MISRI WAIPITISHA KATIBA MPYA

  Maafisa wa Tume ya Uchaguzi wakihisabu kura za maoni mjini Cairo, Misri. 



WAPIGA kura nchini Misri wameiunga mkono kwa kiasi kikubwa katiba ambayo inafungua njia kwa mkuu wa majeshi kupigania urais, ingawa idadi ya waliojitokeza kupiga kura hiyo inatajwa kuwa kipimo muhimu cha umashuhuri wake.
 

Magazeti yanayomilikiwa na serikali yameisifu kura hiyo, ambapo gazeti la Al-Akhbar la hivi leo limetoka na kichwa kikubwa cha habari kisomekacho: "Watu wanasema Ndiyo", huku gazeti jengine la Al-Ahram likiandika kuwa asilimia 90 ya wapiga kura imeipitisha katiba mpya.

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi, Jenerali Abdel-Fattah Othman, zaidi ya asilimia 50 kati ya wapiga kura milioni 53 wa Misri walishiriki kwenye kura hii ya maoni. Mwanzoni jeshi lilikuwa linatazamia kupata asilimia 33.

"Kura zinaendelea kuhesabiwa. Matokeo yaliyopatikana hadi sasa yanaonesha kuwa waliojitokeza kupiga kura ni zaidi ya asilimia 55. Wapiga kura walioipitisha kura ya maoni wanaweza kuzidi asilimia 95." Amesema Jenerali Othman wakati akizungumza na kituo cha televisheni cha Al-Hayat.

Kiasi cha asilimia 95.8 cha waliopiga kura zao katika mji wa kusini wa Sohag waliikubali katiba hiyo, kwa mujibu wa kituo cha al-Hayat, ambacho kiliwanukuu maafisa wa uchaguzi, ambapo katika mji wa pwani wa Suez ni asilimia 98.

Matokeo yaliyotarajiwa


Muungaji mkono wa katiba mpya akiinua vidole viwili kuashiria ushindi katika Uwanja wa Tahrir.

Kwa ujumla, matokeo haya ya awali ambayo yanatolewa na vyombo vya habari ambavyo aidha vinamilikiwa na serikali au vinaunga mkono jeshi, yanaonesha kuwa asilimia 90 ya wapiga kura imeunga mkono katiba hiyo, ambayo serikali iliyowekwa madarakani na jeshi inasema inatoa uhuru zaidi wa kujieleza na haki za wanawake.

Hata hivyo, matokeo haya yalitarajiwa tangu awali, baada ya kundi la Udugu wa Kiislamu, ambalo sasa serikali imeliweka kwenye orodha ya taasisi za kigaidi, kuigomea kura hiyo.

Pia hakukuwa na kampeni yoyote ya maana kuwashajiisha watu kupiga kura ya hapana. Wanaharakati kadhaa waliopiga kampeni hiyo walikamatwa na polisi.

Sisi afuatilia idadi ya wapigakura


Mkuu wa majeshi, Jenerali Abdel-Fattah al-Sisi (mwenye miwani, mbele).

Maafisa wa serikali wamesema kwamba mkuu wa majeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Sisi, ambaye alimpindua rais wa kwanza kuchaguliwa kwenye uchaguzi huru na wa haki, Mohamed Mursi, hapo mwezi Julai mwaka jana, anafuatilia kwa karibu idadi ya waliojitokeza kupiga kura.

Sisi amesema yuko tayari kugombea ikiwa kutakuwa na uungwaji mkono wa kutosha, na kura hii ya maoni iliyokamilika jana ni kipimo cha kwanza.

Msemaji wa jeshi aliwashukuru wapiga kura kwa kile alichokiita "kujitokeza kwa wingi katika mapambano ya kishujaa ya kura ya maoni."

Siku ya Jumanne, ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya kupiga kura, mapambano kati ya wafuasi wa Mursi na wapinzani wao na polisi, yalisababisha mauaji ya watu tisa.

Na ingawa jana, Jumatano, ilimalizika bila taarifa za mauaji, wizara ya mambo ya ndani inasema iliwakamata kiasi cha watu 444 kwa kuandamana na kuharibu vituo vya kupiga kura.

Matokeo rasmi yanatarajiwa siku ya Jumamosi.DW

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...