Pages

January 5, 2014

Marando, Profesa Safari watajwa Bunge la Katiba


Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam juzi. Picha na Salhim Shao.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetaja majina ya wanachama wake wanne yaliyopelekwa wa Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuteuliwa kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Akitoa taarifa ya Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika aliwataja waliopendekezwa kuwa ni Profesa Abdallah Safari, Mabere Marando, Nasra Juma Burhan na Method Kimomogoro.
Miongoni mwa hayo yatateuliwa majina ya watakaokuwa Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba linalotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.
Desemba 13 mwaka jana Rais Kikwete alivitaka vyama vya siasa na wadau wengine kupeleka ofisini kwake majina yasiyopungua manne au kuzidi tisa kwa ajili ya kupata majina 201 yanayohitajika kuteuliwa kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Akitoa ufafanuzi kuhusu majina yaliyopelekwa na Chadema, Mnyika alisema kuwa walioteuliwa wana sifa zilizopendekezwa kuangaliwa wakati uteuzi huo.(P.T)
"Marando huyu ni msomi mwenye Digrii ya Sheria na ni wakili wa Mahakama Kuu, Kimomogoro ni msomi wa sheria na ni Wakili wa Mahakama Kuu, Profesa Safari ni msomi mwenye Shahada ya Uzamivu aliyebobea kwenye mambo ya sheria, vilevile ni Wakili wa Mahakama Kuu na mama Burhani ni mwalimu kwa taaluma," alisema Mnyika.
Alibainisha kuwa Kamati Kuu ya Chadema imeazimia kupita nchi nzima kuchukua saini na majina ya wananchi wote walio na sifa za kupiga kura, lakini majina yao hayamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Aliongeza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kutangaza kuwa haitalifanyia marekebisho Daftari la Wapigakura kabla ya upigaji kura ya maoni.
"Chama kimekusudia kukusanya orodha na saini za wananchi ambao wataathirika na hatua hii ya tume na Serikali kuacha kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura," alisema na kuongeza:
"Tutakusanya saini za wananchi ambao ama ndiyo wamefikia umri wa kujiandikisha au walipoteza kadi na hawana utambulisho mwingine na walitaka kujiandikisha kwenye daftari hilo au walihama makazi na walioathirika na suala la ukazi hasa kwa Zanzibar. Tutaanza kazi hiyo ili kuishinikiza Nec na Serikali kuboresha daftari hilo kabla ya kura ya maoni."
Mnyika alisema kwamba taarifa hizo za wananchi zitapatikana kupitia maandamano, programu ya Chadema ni msingi, Operesheni za M4C kwa mujibu wa utaratibu ambao chama kitaeleza baadaye.
Chanzo>Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...