Wajumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakitia saini Rasimu ya Pili ya Katiba juzi.
Rasimu hiyo itakabidhiwa leo kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein,
Karimjee, Dar es Salaam. Picha ya mtandao.
KWA UFUPI
·
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawasilisha
Rasimu ya Pili kwa Rais, baada ya hapo itavunjwa kwa mujibu wa sheria
·
Swali la nini kilichomo katika Rasimu ya Pili
ya Katiba Mpya litajibiwa leo wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba
itakapokabidhi rasimu hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar,
Dk Ali Mohammed Shein.
Dar es Salaam. Swali
la nini kilichomo katika Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya litajibiwa leo wakati
Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapokabidhi rasimu hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete
pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Rasimu inayosubiriwa kwa hamu na wananchi wa kada zote itatolewa
ikiwa imepita miezi saba tangu tume hiyo ilipotoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba
ambayo ilijadiliwa na kuboreshwa katika Mabaraza ya Katiba yaliyoketi kuanzia
Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya
wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotangazwa Juni 4, mwaka huu.
Hafla ya kukabidhi rasimu hiyo itafanyika leo saa 6.00 mchana
katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na asasi mbalimbali.
Baada ya kukabidhi rasimu hiyo ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba itavunjwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Warioba ndiye
atakayesoma rasimu hiyo kwenye Bunge Maalumu la Katiba linalotazamiwa kuanza
vikao vyake Februari, mwakani.
Alipoulizwa nini kilichoongezwa au kupunguzwa katika rasimu
hiyo, Jaji Warioba alisema: “Siwezi kueleza kama kuna kilichoondolewa au
kurekebishwa... kesho (leo), Watanzania watapata fursa ya kujua mapendekezo ya tume,
wasubiri.”
Baadhi ya mambo yanayosubiriwa kwa hamu kujua kama yamefanyiwa
marekebisho au la kwenye Rasimu Mpya ni pamoja na mfumo na muundo wa Muungano,
umri wa kugombea urais, wabunge kutokana na mikoa, umri wa kugombea urais na
mengine.
Serikali Tatu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia Rasimu ya Kwanza
ilipendekeza kuundwa kwa Serikali Tatu na alipokuwa akizungumzia hilo wakati
akitangaza Rasimu ya Kwanza, Jaji Warioba alisema uamuzi huo ulifikiwa kwa kuwa
yalikuwa ni maoni ya wananchi walio wengi.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilizua mjadala mkubwa kwani chama
tawala, CCM, kilipinga na kuweka bayana kwamba kinataka muundo wa Muungano
uendelee kuwa wa Serikali mbili.
Vyama
vya upinzani kwa upande wake, viliunga mkono pendekezo hilo la muundo wa Serikali
Tatu huku CUF kikienda mbali zaidi kwa kutaka Zanzibar ipewe mamlaka ya kuwa na
dola kamili.
Katika Rasimu ya Kwanza ilipendekezwa mambo saba tu ndiyo
yabakie kwenye mamlaka ya Muungano.
Mambo hayo ni pamoja na Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki
Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa na Ushuru wa bidhaa na mapato
yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mambo hayo, ilipendekezwa na Tume hiyo kuwa chini ya
wizara ambazo zitaongozwa na mawaziri wakazi ambao hawatatokana na wabunge
kwani watatakiwa kuchaguliwa nje ya taasisi hiyo.
Kurejeshwa kwa
jina la Tanganyika
Baada ya kutolewa kwa Rasimu ya Kwanza, mjadala mwingine
ulioibuka hasa baada ya kupendekezwa kwa muundo wa Muungano kuwa wa Serikali
Tatu ni hatua ya Tume kuendelea kutumia jina la Tanzania Bara.
Baadhi ya wadau walikosoa pendekezo hilo wakitaka jina la
Tanganyika litajwe katika Katiba badala ya Tanzania Bara.
Katika Rasimu ya Kwanza, Tanzania Bara na Zanzibar
zilihesabiwa kuwa washirika wa Muungano.
Ikiwa Serikali tatu zitarudishwa swali linakuja kama
Tanzania Bara itatumia jina la Tanganyika ambalo ililitumia kuanzia mwaka
1961 hadi 1964 ilipoungana na Zanzibar.
Kufutwa kwa
wadhifa wa Waziri Mkuu
Rasimu ya kwanza ilipendekezwa kufutwa kwa wadhifa wa
Waziri Mkuu kwenye Serikali ya Muungano na badala yake kupendekeza kuwapo kwa
Rais na Makamu wake.
Baadhi ya wadau walihoji juu ya usimamizi wa kazi za kila
siku za Serikali jukumu ambalo kwa sasa lipo kwa Waziri Mkuu.
Suala hilo nalo lilizusha mjadala mkali wakati wa
mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.
Mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza yalitaka moja ya sifa za
mgombea urais kuwa miaka 40 lakini baadhi ya wanasiasa, hasa vijana, wametaka
umri huo ushushwe hadi miaka 35.
Wagombea binafsi
Jambo jingine lililopendekezwa katika Rasimu ya Kwanza ni
kuwapo kwa mgombea binafsi kuanzia ubunge hadi urais.
Hilo halikuwa na mjadala mkubwa miongoni mwa wadau mbalimbali
kutokana na ukweli kwamba ni jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda
mrefu na wananchi.
Muundo wa Bunge
la Muungano
Rasimu ya Kwanza ilipendekeza kuwa wabunge watakuwa 75.
Kwa maana ya 50 kutoka Tanzania Bara, 20 kutoka Zanzibar
na watano kutoka kundi maalumu ambao watateuliwa na Rais kwa ajili ya kuwatetea
watu wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza, wabunge wa
kuchaguliwa watagombea kupitia mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Rasimu ya kwanza ilipendekeza kuwa kila mkoa utachagua
mbunge mmoja wa kike na wa kiume ili kuleta uwiano na kupendekeza kufutwa kwa
viti maalumu suala ambalo lilizua mjadala.
Haki za Binadamu
Moja ya mambo ambayo yaliibuka mjadala ni haki za
binadamu. Katika Rasimu ya Kwanza, ilipendekezwa kuundwa kwa Tume ya Haki za
Binadamu itakayokuwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wasiozidi
saba.
Lakini wadau wengi waliotoa maoni yao walitaka sheria
kandamizi 40 za Tume ya Nyalali zisiwepo katika Katiba Mpya.
Mambo mengine
Kuhusu madaraka ya Rais, Tume hiyo ilipendekeza katika
Rasimu yake ya Kwanza kwamba yabaki kama yalivyo hasa kwa uteuzi wa viongozi wa
ngazi za juu, pia ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi.
Katika Rasimu hiyo ya Kwanza, pia ilipendekezwa kusiwepo
na uchaguzi mdogo, isipokuwa kama nafasi hiyo itaachwa na mgombea binafsi
lakini kama ni wa kutoka katika chama cha siasa, ijazwe na mtu kutoka chama
chake.
Kuhusu Tume ya Uchaguzi, Tume hiyo ilipendekeza katika
Rasimu ya Kwanza kwamba jina la Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), libadilishwe
na iitwe Tume Huru ya Uchaguzi.
Rasimu hiyo, ilipendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu
(Supreme Court), majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani watateuliwa na
Rais, baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment