OPERESHENI KIMBUNGA BALAA TUPU.
Na Theonestina Juma, Bukoba
Kampeni ya
kitaifa ya kuwaondoa wahamiaji haramu nchini iliyopewa jina la “Operesheni
Kimbunga” awamu ya pili ambayo inaendelea katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya
Ziwa, imewanasa majambazi watano wanaojishughulisha na biashara ya kuuza silaha
zinazotoka nchi jirani na kuziingiza nchini.
Naibu Kamishna wa operesheni
hiyo, Simon Sirro, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari
Mjini Bukoba, mkoani Kagera, kuhusu maendeleo ya operesheni hiyo.
Alisema
hadi sasa, majambazi 88 wamekamatwa miongoni mwao, watano wanaojihusisha na
biashara ya kwenda nchini Burundi kununua silaha kwa sh. 300.000 na kuziingiza
nchini na kuziuza kuanzia sh. milioni moja.
“Majambazi watatu wamebainika kusambaza silaha kwa wateja hapa
nchini na majambazi wote ni Watanzania, jambazi mmoja alikuwa akifanya biashara
ya kuuza mbuzi nchini Burundi.
“Baadaye alipoona biashara hiyo hailipi,
aliwashawishi Watanzania wenzake kufanya biashara ya kuuza silaha ambayo ndiyo
inawalipa hivyo kuanza biashara hiyo,” alisema kamanda Sirro bila kutaja majina
ya majambazi hao.
Alisema operesheni hiyo awamu ya pili, ilianza Septemba 21
hadi Oktoba Mosi mwaka huu ikiwa na mafanikio makubwa ambapo wahalifu 529
walikamatwa na wahamiaji haramu 425 katika Mikoa ya Geita, Kigoma na
Kagera.
Aliongeza kuwa, walioruhusiwa kwa uamuzi wa mahakama ni 159,
waliorudishwa makwao kwa hiari 122, walioachiwa huru 39 na wanaoendelea kuhojiwa
hadi sasa 105.
Kamanda Sirro alisema, watu watano wanashikiliwa kwa tuhuma
ya kuwatorosha na kuwahifadhi wahamiaji na majangili 11 ambapo silaha mbalimbali
23 zimekamatwa.Silaha hizo ni pamoja na bunduki aina ya SMG, bastola, magobole
18, magazine mbili, bomu la kutupwa kwa mkono pamoja na sare moja ya Jeshi la
Burundi.
Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro alisema ng’ombe 2,220
wamekamatwa, 103 wanamilikiwa na Bw. Kalemela George, wilayani Biharamulo ambaye
mahakama imetoa amri ya kutaifishwa baada ya kuwaingiza katika Hifadhi ya Taifa
Biharamulo kinyume cha sheria.
“Natoa wito kwa wafanyabiashara wa nyama mjini
Bukoba,kwenda kuwanunua kwa ajili ya kuchinja na kuuza, hatua ya kutaifisha
mifugo ni nzuri...kesi nyingine za mifugo bado tunafanya utaratibu wa
kuzifikisha mahakamani,” alisema.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambaye pia ni
Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali mstaafu Issa Njiku, alisema operesheni hiyo
bado inaendelea pia itakuwa endelevu.
No comments:
Post a Comment