Mazungumzo ya uwezekano wa kuunda serikali ya mseto ya vyama vikuu yanaanza leo mjini Berlin baina ya wajumbe wa vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU na wa chama kikuu cha upinzani SPD.
Mwenyekiti wa chama cha CDU Kansela Angela Merkel na Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani SPD, Sigmar Gabriel
Kabla ya kuanza viongozi wa pande zote wametoa mwito kwa washiriki wa kuuzingatia moyo wa kuwajibika. Kiongozi wa wabunge wa chama cha CDU Volker Kauder amesema sasa umefika wakati wa kufanya mazungumzo ya busara.Bwana Kauder amesema sasa siyo wakati wa kuziendekeza hisia.
Waziri Mkuu wa jimbo la Lower Saxony Stephan Weil kutoka chama cha SPD pia amewataka wote wanaoshiriki kwenye mazungumzo wautambue wajibu wao.
Hii ni mara ya kwanza kwa mazungumzo juu ya uwezekano wa kuunda serikali ya mseto ya vyama vikuu kufanyika baada ya uchaguzi mkuu wa Ujerumani uliofanyika wiki mbili zilizopita. Jumla ya wajumbe 21 wanashiriki kwenye mazungumzo hayo kutoka vyama vya CDU,CSU na chama kikuu cha upinzani SPD.
Mwenyekiti wa chama cha CDU kilichoshinda uchaguzi Kansela Angela Merkel amesema mazungumzo yatafanyika kwa kuzingtia haki. Naye Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel amesema kuwa chama chake kipo tayari kwa mazungumzo hayo.Lakini ameeleza kwamba baraza la chama chake limetamka wazi kwamba halikutoa idhini ya kuzungumzia juu ya kuunda serikali, bali tu juu ya kufanya mazungumzo ya kuyaangalia mawezekano yaliyopo."
Mafanikio ya mazungumzo hayo yatategemea na jinsi masuala ya kila upande yatavyozingatiwa.
Masuala ya utatanishi:
Chama cha SPD kinatetea sera ya kupandisha kodi kwa wenye mapato ya juu.Chama hicho pia kinataka kuwekwa kwa utaratibu wa mishahara ya kima chini kwa wote .Chama cha Kansela Merkel cha CDU kinapinga sera ya kupandisha kodi. Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble anaetoka katika chama cha CDU amesisitiza katika mahojiano kwamba chama chake kinapinga wazo la kupandisha kodi.
Katika juhudi za kuwahimiza viongozi wa vyama kuchukua hatua za kuunda serikali, Rais wa Ujerumani Joachim Gauck mapema wiki hii alifanya mazungumzo ya faragha na viongozi wa vyama vote.
Washirika wa Ujerumani barani Ulaya wanayafuatilia mazungumzo hayo kwa makini wakiwa na hofu kwamba kuchelewa kuundwa serikali nchini Ujerumani kunaweza kuyarudisha nyuma maamuzi muhimu kuhusu hatua za kukabiliana na mgogoro wa madeni barani Ulaya.
No comments:
Post a Comment